Home

Dk. Mengi: Watanzania wanaweza, wajiamini.

Vijana nchini na wananchi kwa ujumla
wametakiwa kujiamini kwamba wanaweza
kufanya makubwa kwa manufaa yao na ya Taifa,
licha ya kuwapo kwa kasumba kwa baadhi ya
vongozi ya kutowaamini Watanzania na badala
yake kuwaamini wageni.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald
Mengi, katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa
washindi wa Shindano alilolianzisha la kubuni
wazo bora la biashara, wa mwezi Aprili mwaka
huu.
Alisema katika jamii kumejengeka utamaduni wa
kuwaamini zaidi watu kutoka nje hasa
wawekezaji kwa kuwapa vipaumbele kuliko
wananchi husika, jambo ambalo linachangia
kukwamisha maendeleo ya nchi na kusababisha
umaskini.
“Tatizo ambalo baadhi ya viongozi linawatesa
mara kwa mara ni kuwa hawawaamini wananchi
wao; wanaamini kuwa watu kutoka nje ndiyo
wanaweza. Na katika uwekezaji, wawekezaji wa
nje ni rahisi kuaminiwa kuliko wa ndani,” alisema
Dk. Mengi.
Dk. Mengi alisema kuna umuhimu viongozi wa
kuwaamini wananchi wao na kuacha kuwakingia
vifua wageni kutoka nje, huku akisistiza kuwa ni
lazima nchi itumie kikamilifu uwezo wake wa
ndani kabla ya kufikiria kutafuta kutoka nje, ili
kujiletea maendeleo endelevu.
Alisema kama kuna Mtanzania anayeshindana na
raia kutoka nje kupata kazi ama kandarasi fulani,
na wote wana sifa zinazolingana, hakuna haja ya
kuona aibu kumpendelea Mtanzania.
Aidha, Dk. alisema Taifa limekumbwa na
saratani yenye sura tatu: rushwa, ubinafsi na
uongo na kuwataka vijana kutafuta dawa za
kutibu saratani hiyo na kutahadharisha kuwa
kama isipopatiwa tiba, Taifa haliwezi kuwa na
amani.
Kuhusu tatizo la umaskini, alisema umaskini wa
nchi unachangiwa na mambo mengi, ikiwamo
wananchi kutoshirikishwa kikamilifu katika
matumizi ya rasilimali za Taifa.
Kiongozi wa jopo la majaji wa shindano hilo,
ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya
Uongozi na Ujasiriamali (IMED), Dk. Donath
Olomi, alisema walipokea twiti 6,500 kutoka kwa
washiriki wa makundi mbalimbali nyingi zikitoka
kwa watu wa mikoani.
Dk. Olomi alisema mshindi wa kwanza wa
shindano hilo anatakiwa kuwa na wazo ambalo
linatekelezeka pamoja na kuanza kulitekeleza.
Aliwataka washiriki kufanya utafiti kabla ya
kubuni mawazo ili kuepuka kurudiarudia mawazo
ambayo tayari yapo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Ibra
Contractors Ltd, Maida Waziri, aliwahamasisha
watu hususan wasichana waunde vikundi ili
kutoa wazo bunifu lenye ubora, huku akisema
ingawa kuna ushiriki wa kuridhisha, lakini ubora
wa mawazo bunifu bado hauridhishi.
Washiriki wawili, Daud Fabian, Mhitimu wa
Sayansi ya Kompyuta na Mhitimu wa Chuo Kikuu
Dar es Salaam, Anthony Mhanda, wamefungana
katika kushinda nafasi ya kwanza kwa Mwezi
Aprili. Kila mmoja alijinyakulia Sh. milioni tano.
Fabian alishinda kwa wazo la biashara
linalolenga kuanzisha mfumo wa ulinzi shirikishi
kupitia mfumo wa simu za mikononi kwa
kuwaunganisha wananchi katika njia moja
itakayotoa taarifa ya uhalifu utakapotokea ili
kuudhibiti. Mhanda alituma wazo la kujenga
maabara ndogo ya kuchakata na kupima ubora
wa asali ya wafugaji na wasindikaji mkoani
Katavi.
Washiriki wengine wanane ambao twiti zao
ziliingia katika 10 bora walizawadiwa shilingi
milioni moja kila mmoja. Washindi hao ni Dafrosa
Katarahiya, Philemon Naman, Salehe Senkondo,
David Dee, Freddy Freddy, Deodatus Mramba,
Mbonea Mpembeni na Yusuph Maglah.
CHANZO: NIPASHE

2 comments: