Na Charles Nazi
Hali ya uchumi duniani imekuwa ngumu si hapa kwetu Tanzania tu bali pia hata katika nchi zilizoendelea. Uwezo wa serikali nyingi duniani hasa wa kutoa huduma kwa watu wake unazidi kupungua kutokana na serikali nyingi kuelemewa na madeni. Matatizo yaliyosababisha hali hii ni pamoja na; kushuka kwa thamani ya pesa, kupanda kwa deni la taifa, ongezeko la watu, kupanda kwa bei ya mafuta,makampuni kufilisika na wafanyakazi kupunguzwa kazini na kukosekana kwa elimu ya ujasiriamali kwa jamii. Hali hii inazidi kuwagusa watu wengi zaidi duniani pengo la masikini na matajiri linazidi kuwa kubwa na tabaka la kati linaanza kutoweka. Hali hii ikiendelea kama ilivyo kutakuwa na matabaka mawili tu duniani yaani matajiri na masikini.  Jee unawezaje kuepuka kuingia katika tabaka la umasikini na kuingia katika tabaka la matajiri? Suluhisho ni kuwa mjasiriamali kwa kujifunza na kutekeleza kwa vitendo mbinu za ujasiriamali.
Watu wengine wamekuwa na dhana potofu kwamba tatizo la umasikini linatokana na ukosefu wa pesa au mitaji peke yake lakini mimi nina mtizamo tofauti, kama tatizo la umasikini lingekuwa ni ukosefu wa fedha kuna matajiri wawili kule Marekani, Donald Trump na Robert Kiyosaki wamesema kwamba wangejitolea kuwagawia watu pesa lakini katika utafiti wao wamegundua kwamba hata ukimpa mtu pesa atatumia zikiisha atarudi tena kuja kuomba, hivyo mbinu hiyo siyo endelevu inamfanya huyu anayeomba kuwa tegemezi na kuzidi kuwa masikini. Kwa hiyo walichukua msemo wa kichina kwamba ukitaka kumsaidia mtu uasimpe samaki ila umpe nyavu na mbinu za kuvua samaki. Vivyo hivyo katika kumkomboa mtu kutoka kwenye umasikini unatakiwa kupatia elimu ya ujasiriamali na namna ya kutumia mbinu hizo.  Kwa hiyo watu hawa pamoja na wanaharakati wengine wa kupambana na umasikini tumeamua kutoa elimu ya ujasiriamali kwa kutumia njia mbali mbali. Kwa maoni yetu pesa haikufanyi wewe kuwa tajiri bali elimu ya ujasiriamali ndiyo inayoweza kukufanya kuwa tajiri. Kama pesa ingekuwa inao uwezo wa kuwafanya watu wawe matajiri kuna miofano mingi tu ya watu ambao walipata bahatinasibu ya mamilioni na wastaafu ambao walipata mafao ya mamilioni ya fedha lakini kwa kukosa elimu ya ujasiriamali wametumia pesa zote na kufilisika.
Kila mtu ana matatizo yake ya kifedha  katika dunia ya sasa kuwa na elimu na kuwa na Shahada ya fani fulani pekee haitoshi unatakiwa kuwa na elimu pia ya ujasiriamali, kutegemea pensheni peke yake ni tatizo, kwani utafiti uliofanyika ni kwamba Wastaafu wengi ambao wanategemea pensheni zao huishiwa ndani ya miaka 5 baada ya kustaafu na kulipwa mafao yao ya mkupuo na zile hela za pesheni wanazolipwa  kidogo kidogo kila mwezi  huwa hazitoshi hata kukidhi mahitaji ya muhimu ya watu hao na kuwafanya waishi katika hali ya umasikini. Sizungumzii hali hii kwa nia ya kuwatisha watu  ila hii ndiyo hali halisi kama ukitaka kuthibitisha maneno haya waulize wazee wastaafu watakwambia kuhusu taabu wanazozipata.
 Watu wengine wamekuwa na mawazo ya kuitegemea serikali iwakwamue katika matatizo yao ya kifedha hayo pia ni mawazo potofu. Serikali haiwezi kukutatulia matatizo yako ya kifedha ila ni wewe mwenyewe ndiyo unaweza kutatua matatizo yako ya kifedha kwa kuchukua hatua kupata maarifa ya ujasiriamali, kubuni shughuli za uzalishaji mali utoaji huduma na biashara.  Bahati mbaya hata wajasiriamali tulionao wamekuwa wakiendesha biashara zao kwa mazoea hivyo kuzifanya zisiwe endelevu. Kama wewe ni mjasiriamali wekeza kwenye maarifa ya ujasiriamali pia ili uinue hali yako ya maisha. Unaweza kujiendeleza kwa kusoma vitabu vya ujasiriamali, kusoma makala kama hizi kwenye magazeti, kuhudhuria mafunzo na semina za ujasiriamali ambazo huwa zinatolewa na watu mbali mbali.
Mtaji mkubwa uliopewa na mwenyezi Mungu ni akili yako. Watu wengi hatutumii vizuri akili zetu katka kufikiria namna ya kutatua matatizo yetu, kwa mfano unapopata tatizo lolote badala ya kufikiria kuhusu tatizo hilo anza kufikiria namna ya kutatua tatizo hilo. Pia kama ukimudu kufikiria namna ya  kutatua matatizo yako basi unaweza kuanza kufikiria namna ya kutatua matatizo katika jamii ukisha jua matatizo yanayoikabili jamii unaweza kutafuta suluhisho na hilo suluhisho unaweza kulifanya likawa fursa ya biashara. Kwa mfano kuna mtu mmoja alikuwa anaishi katika kijiji kimoja katika kutafuta mahitaji yake ya kila siku kama vile sukari, majani ya chai unga wangano nk. alilazimika kutembea umbali wa kilomita 3 kila mara ili kwenda kununua mahitaji yake kijiji cha jirani. Alivyochunguza akagundua kwamba tatizo hili lilikuwa si la kwake peke yake hata wanakijiji wenzake walikuwa wakihangaika kufuata bidhaa hizo kijiji cha jirani kama yeye, ndipo hapo jamaa aliamua kuanzisha duka la rejareja katika kijiji chake, na kwa kweli duka lake liliendelea sana na alipata pesa nyingi.   Ili ufanikiwe kiuchumi maishani unapaswa kuwa mtundu, mbunifu na mtafiti.
Eneo lingine ambalo hatulitumii ni kukagua vipaji vyetu. Mwenyezi Mungu kamjalia kila mtu kipaji chake, wengine ni waimbaji wazuri, wasusi, wasanii, wachekeshaji, washereheshaji, wakimbiaji, wapishi wazuri nk. Jee umewahi kijuliza una kipaji gani? Kama hujui waulize watu wako wa karibu, kama vile baba, mama, kaka, dada, rafiki, mke mume nk. Jee unakitumia kipaji chako ipasavyo kukuletea maendeleo yako kiuchumi? Kwa mfano kama wewe ni msusi mzuri kwa nini usianzishe saluni? Kama wewe una kipaji cha kupika kwa nini usianzishe hoteli? Bahati nzuri sana kipaji chako kinaweza kuwa ndiyo mtaji wako mkuu wa kuendesha biashara yako. Muhimu ukigundua kipaji chako lazima ukiendeleze.
Jee unapaswa kufanya nini ili upambane na tatizo hili la umasikini? Kwanza unapaswa kuwa na shuguli ya kufanya. Inasikitisha kuona watu wazima wanakaa vijiweni, kina babu wanashinda kwenye kahawa na kucheza bao siku nzima au vijana wanacheza pool siku  nzima. Mtu yeyote aliyefikisha umri wa miaka 18 anapaswa kuwa na shughuli ya kufanya kama ni ya kuajiriwa au ya kujiajiri. Jee wewe ni kati ya  watu wengi ambao  wana mitaji lakini hawajui wafanye nini unaweza kutumia akili yako kubuni shughuli ya kufanya au kutumia kipaji chako kufanya biashara. Hatua ya pili ni kujenga tabia ya kuweka akiba. Katika dunia ya sasa kuna sehemu nyingi ambazo unaweza kuweka akiba yako mfano kwernye SACCOS, akaunti za akiba kwenye benki mbali mbali. Unapaswa kuweka kati ya asilimia 10 % hadi 15 % ya mapato yako kwa mwezi. Mwisho ni kuwekeza fedha zako katika vitegauchumi endelevu. Jee ni vitegauchumi gani ambavyo ni endelevu, kuwekeza katika majengo ya kupangisha. Kwa nini tunashauri uwekeze pesa zako katika vitegauchumi ni kwa sababu pesa ikikaa sana benki huwa inaongezeka kidogo kidogo kwani faida inayopatikana ni ndogo kuliko mfumuko wa bei hivyo baada ya muda pesa yako itashuka thamani, lakini ukiwekeza kwenye kitegauchumi endelevu thamani ya pesa yako inapanda. Kwa mfano ukiwekeza kwenye majengo ya kupangisha kila hali ya uchumi inavyozidi kuwa mbaya thamani ya majengo na kodi ya nyumba inapanda.Vitegauchumi huingiza pesa bila kukulazimu kuendelea kufanya kazi hivyo hata ukizeeka au kuugua au kufukuzwa kazi vitegauchumi vyako vinaweza kukulinda kwani vitaendelea kukupa kuipato bila kufanya kazi. Swali la kujiuliza ni jee chanzo chako kikuu cha mapato yako ni katika kazi unazozifanya kila siku au kutoka kwenye vitegauchumi? Kama unategemea kazi kuingiza sehemu kubwa ya kipato chako una hatari ya siku moja kurudi kwenye umasikini kama ukiugua muda mrefu, kufukuzwa kazi au kustaafu.Jitahidi kuwekeza pesa zako kwenye vitegauchumi vilivyo endelevu ili uwe na uhakika wa maisha.
Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi wa Kampuni ya CPM Business Consultants, Mjasiriamail,Mshauri wa biashara na mtunzi wa kitabu cha mbinu za biashara , Kupata ushauri wa biashara, Ili Kupata mafunzo ya ujasiriamali bila malipo kwa email bofya hapa kujiunga;  http://mshauriwabiashara.weebly.com

Categories:

Leave a Reply