UJASIRIAMALI---UFUGAJI BORA WA KUKU WA KIENYEJI

Idadi ya wanyama wanaofugwa kwa chakula imezidi ile ya binadamu zaidi ya mara mbili kote ulimwenguni. Kuna maelfu ya wanyama kote duniani ilihali ni wachache tu wanaoweza kufugwa. Kati ya hawa wanyama, ni aina nne (Ng'ombe, kondoo, mbuzi na kuku) wanaochukua asilimia 95% ya wanyama wote wanaofugwa. Wanyama hawa hupatikana katika nchi za hari kwenye nyanda za chini. Lakini kati ya mifugo hawa, kuku ni maarufu katika nchi za hari na hata kote ulimwenguni.Lengo la makala haya ni kutoa maelezo ili kusaidia wafugaji wa kiwango kidogo katika nchi
zinazostawi, katika kupunguza umaskini. Sehemu ya kwanza (I) itatoa maelezo kuhusu ufugaji na
hasa ufugaji wa kuku, Sehemu ya pili (II) itaangazia maswala yafuatayo katika kuinua hali ya uchumi
kwa kufuga kuku:
1. Kuendeleza ufugaji wa kuku za kienyeji kwa kutumia njia zisizohitaji gharama nyingi.
2. Kutafuta mbinu na njia muafaka za kuzalisha viwango vya kuku bora kwa njia ya kiasili.
3. Matumizi ya njia za kiasili au zile zisizo gharimu pesa nyingi kutibu na kuzuia magonjwa ya
kuku.
SEHEMU YA I: MAELEZO KUHUSU UFUGAJI WA KUKU KATIKA NCHI
ZINAZOENDELEA
NAFASI YA MIFUGO
Licha ya kukosa mashamba makubwa ya kuendeleza ufugaji wa ng'ombe, jamii nyingi katika nchi za
hari (tropics) hupata nafasi ya kufuga kuku kwa kiwango kidogo. Idadi ya wanyama wanaofugwa
huongezeka sambamba na ile ya watu. Idadi ya watu inapoongezeka ndipo ile ya mifugo huzidi.
Idadi kubwa ya watu huhitaji chakula kingi na matumizi huongezeka, hivyo basi watu hufanya bidii
kuzalisha chakula na mapato kutoka kwa shamba.
Ufugaji wa ng'ombe na wanyama wanaohitaji lishe kwa wingi huhitaji kiasi kikubwa cha shamba ili
kupanda mimea na lishe la mifugo. Ukilinganisha na ufugaji wa kuku, utahitaji mabaki ya vyakula
na sehemu ndogo ya shamba. Ufugaji wa kuku umeweza kunawiri hata pasipo fedha.
Katika nchi za hari ufugaji wa kienyeji hautahitaji kazi nyingi, kazi hii hufanywa na akina mama na
watoto. Kwa kawaida katika nchi hizi kazi nyingi za nyumbani hutekelezwa na mama. Vyakula vya
kuku vyaweza kutoka kwa: 1) Mabaki ya chakula, 2) Mabaki ya mimea, 3) Mabaki kutoka jikoni
na 4) Vyakula vya kujitafutia (kwa mfano kwekwe, mbegu, wadudu, nyongonyongo, n.k). Mfumo
wa kufuga kuku kwa njia ya kienyeji hutumia viungo vinavyopatikana kwa urahisi na kuimarisha hali
ya kiuchumi na chakula bora kwa jamii.
Ni muhimu sana kufuga mifugo hata ikiwa ni kwa kiwango kidogo kwa sababu ya 1) Chakula bora
na kuongeza mapato ya jamii kwa viwango vya kuridhisha; 2) Mifugo ni hakiba au banki, faida yake
huzaana tu kama riba ya benki; 3) Mifugo yaweza kuuzwa ili kugharamia karo ya wanafunzi,
malipo ya hospitali, gharama nyingine za nyumbani na hata shambani; 4) Kwa matumizi ya kijamii
(kwa mfano kulipia mahari, shughuli za kidini, n.k); 5) Mifugo husaidia katika kukabili wadudu,
kwekwe na kuimarisha rutuba kutokana na mbolea ya kinyesi. Ni bayana kwamba mifugo ni
muhimu sana kwa mkulima yeyote yule.
UMUHIMU WA UFUGAJI WA NJIA YA KIENYEJI
Ufugaji wa kuku katika nchi zinazostawi waweza kugawanywa mara mbili: 1) Ufugaji wa
kitamaduni au kienyeji pasipo kuwepo gharama, na 2) Ufugaji wa kisasa unaohitaji fedha nyingi.
Ufugaji wa viwango vikubwa kwa kuzingatia mfumo wa kisasa ni maarufu katika kuzalisha kuku wa
nyama na wale wa mayai. Mfumo huu hujumuisha asilimia ndogo sana ya aina ya ufugaji.
Itafahamika kwamba mfumo wa kisasa haujaadhiri ule wa kienyeji. Idadi kubwa ya watu katika nchi
za hari hutegemea mfumo wa kienyeji kwa nyama na mayai.
Mfumo wa kisasa huhitaji pesa nyingi za kununua vyakula vya kuku. Aidha mfumo wa kisasa huhitaji kazi nyingi ili kutekeleza. Mfumo wa kisasa
umefaulu katika nchi zilizostawi kutokana na hali nzuri ya kiuchumi katika kuzalisha (kuku wa hali
ya juu, kuangua vifaranga kwa stima, vyakula vilivyo na madini mengi, vifaa na zana za mashine,
utaalamu wa hali ya juu n.k). Haitafaa sana kuanzisha mfumo kama huu katika vijiji vya mataifa
yanayostawi.
"Mageuzi" katika ufugaji (kuambatanisha mfumo wa kisasa pamoja na ule wa kienyeji) yamefanyiwa
majaribio katika mataifa yanayostawi tangu miaka ya 1950. Matokeo ya kuku wapatao 200 hadi 300
kwa shamba moja hayajawai kufaulu. Hasara imepatikana na waweza kuona nyumba zilizokuwa na
kuku bila chochote, pesa nyingi zimepotea na kuku hawapo.
Mfumo wa kienyeji ni bora (Katika hali ya kiuchumi) iwapo idadi ya kuku haitazidi kuku 50. Ni
rahisi kuweza kuwatunza kuku, kwani hakuna gharama nyingi. Iwapo vyakula au zana za kisasa
zitanunuliwa, basi haitakuwa kwa viwango vikubwa. Mazao ya nyama na mayai yataleta faida.
Sehemu nyingi katika mataifa yanayostawi hakuna stima, katika nchi za hari, ufugaji kwa kiwango
kidogo umeweza kufaulu na kuimarisha uchumi.
FAIDA ZA UFUGAJI WA KUKU KWA NJIA YA KIENYEJI
Faida za uzalishaji kuku ili kuimarisha uchumi kwa njia hii zimepuuzwa na viongozi na wafadhili.
Kuku huleta faida kwa jamii kama tulivyoona katika sehemu ya I. Zaidi ya hayo, ufugaji wa kuku waweza kuimarishwa pasipo gharama nyingi ukilinganisha na mifugo wengine.
· Hutupatia fedha kwa kuuza nyama na mayai
· Mayai ni chakula kilicho na madini muhimu na kisicho ghali katika soko lolote. (madini kama methionine na cystine), madini haya ni muhimu sana kwa afya ya watu hasa watoto wachanga. Pia hutupatia protini.
· Kinyesi cha kuku ni mbolea safi
· Kiwanda asilia cha kutotoa vifaranga
· Gharama za kuanzisha na kuendeleza ni nyepesi
· Kitoweo chepesi na rahisi kwa wageni, kitoweo hakihitaji hifadhi hutumika mlo mmoja au miwili na kumalizika
· Jogoo hutumika kama saa inapowika
· Manyoya ya kuku hutumika kutengenezwa mapambo mbalimbali, mito na magodoro
· Kuku wanahisimu wadudu waharibifu
Kuku ndiye mnyama wa kipekee anayeweza kuishi mahali popote hapa ulimwenguni bila kuadhiriwa
na viwango vya hali ya hewa. Ufugaji wa kuku ndio shughuli inayofanyika kwa wingi duniani kuliko ufugaji wa aina yeyote. Kuku hunawiri vyema katika nchi za hari kutokana na uwiano uliopatikana wakati wa mwanzo binadamu alipofuga Asian jungle fowl aina ya kuku-mwitu. Mayai pia yaweza kuhifadhiwa kwa urahisi na huchukua nafasi ndogo kuliko aina ya bidhaa zozote za mifugo. Mayai yaweza kuwekwa mahali kwa muda mrefu bila kuhitaji barafu. Hautahitaji kuhifadhi kuku kwa njia yoyote, kwani nyama yake hupatikana pale unapohitaji kwa kuchinja.
Upungufu wa kuku wa kigeni ukilinganisha na wale wa kienyeji ni kama ufuatao:
• Kuku wa kigeni hawawezi kukalia na kuangua mayai, hivyo basi wahitajika kununua vifaranga (gharama);
• Vifaranga wa kigeni huhitaji utunzaji maalum na vyakula maalum (gharama);
• Kuku waliozalishwa kwa njia ya kisasa huhitaji chakula kingi ili kutaga mayai (gharama);
• Kuku wa kisasa huhitaji zaidi kuchanjwa dhidi ya magonjwa (gharama)ukilinganisha na wa kienyeji (japo nao huhitaji chanjo);
• Kuku wa kutaga mayai huhitaji mwangaza wa stima (saa 14 kwa siku) ili kutaga mayai (gharama)
Kwa kuongezea, rangi ya nyama na mayai ya kuku wa kienyeji huvutia kuliko ile ya kuku wa kisasa.
Hivyo basi jaribu kuendeleza na kuhimiza ufugaji wa kuku za kienyeji.
Iwapo mkulima ana jogoo mmoja na kuku kumi na mbili, basi kila mwezi waweza kupata kuku
akikalia mayai 10-12 kwa mwezi (mayai yote kwa wakati mwingi hayataanguliwa) kuna hakikisho la
kupata vifaranga vinne kila mwezi. Kuku mzima atachukua miezi minne kuchunga vifaranga
walioanguliwa. Kwa hivyo, kati ya kuku wote kumi na mbili kila mara kutakuwa na kuku wanne
wakitunza vifaranga, huku wale wengine wanane wakitaga mayai.
Kuku waliofugwa kwa njia ya kitamaduni hupata vyakula vyao kwa kutafuta mbegu, wadudu
nyongonyongo, n.k; Lakini kuku hawa hukosa vyakula vya kutosha vilivyo na nguvu ili waweze
kutaga mayai. Vyakula vya kutoa nguvu daima huwa ni haba.
Waweza kuwalisha kuku kwa nafaka ili wapate chakula cha nguvu (mfano kilo moja ya nafaka
iliyopondwa kila siku kwa kuku 10), nafaka hii yapaswa kuwa kavu. Vifaranga wapewe kiasi kidogo
cha nafaka au mchele wiki za kwanza. Kuku wanaolishwa nafaka baada ya kujitafutia chakula nje
huongeza idadi ya mayai (kutoka asilimia 20-25% hadi 40-50%). Kuna umuhimu wa kuhifadhi
nafaka kama lishe badala ya kuuza kwani utapata mayai mengi ambayo baadaye utaweza kuuza.
Hautahitaji kununua vyakula vya protini kwani kuku hujitafutia lishe la protini.
Ikiwa hauna nafaka, waweza kutumia vyakula vya mzizi au ndizi. Vyakula vya aina hii hata hivyo,
huwatatiza kuku wanapovitonogoa, kiwango cha mayai sio kikubwa kama cha wale wanaolishwa
nafaka.
Kwa kuwalisha kuku kwa nafaka utapata hakikisho la mayai manne kwa siku kutoka kwa wale kuku
wanane. Iwapo hakuna nafaka, kati ya kuku wanane wanaotaga utapata mayai mawili tu kwa siku.
Ni bora kutumia nafaka hii kama lishe kuliko kuuza na hatimaye kununua vyakula vya dukani.
Kuku kumi na mbili na jogoo mmoja wanaolishwa kwa kilo moja ya nafaka kila siku waweza
kuelezwa hivi:
• Waweza kuuza kuku wanne kila mwezi na kujaza pengo hilo na wale vifaranga (vifaranga
wanne huanguliwa kila mwezi) na
• Dazani kumi za mayai kila mwezi (mayai manne kila siku).
Kwa mwaka mmoja waweza kukadiri ile faida utakayopata na vile hali ya kiuchumi yaweza
kuinuliwa katika mataifa yanayostawi.
Hata hivyo faida hii haitaafikiwa iwapo magonjwa
hayatazuiwa au kukabiliwa kama ifuatavyo.
TEKELEZA UTARATIBU WA KUZUIA MAGONJWA
Magonjwa ndio husababisha hasara katika mfumo wa ufugaji wa kuku. Kuku waliochanjwa dhidi ya
magonjwa hudumisha afya bora. Jaribu kila mara kuzuia magonjwa, kwani kuzuia ni bora kuliko
kuponya. Kinga yaweza kutolewa mara kwa mara (kila baada ya miezi mitatu) dhidi ya magonjwa
yafuatayo:
Ugonjwa wa Newcastle
Ugonjwa huu ndio huadhiri kuku na kusababisha hasara katika nchi za hari. Virusi vya ugonjwa huu
huenea kwa kasi na rahisi kiasi cha kusababisha vifo kwa asilimia 100%. Dalili za kwanza ni shida
ya kupumua na kung'amua hewa, sauti kama ya kikohozi na kutokwa mate. Kinyesi chaweza kuwa
na rangi ya kijani kibichi. Hadi sasa hakuna dawa.
Waweza kuzuia ugonjwa huu kwa kutoa chanjo. Dawa za chanjo hupatikana kote ulimwenguni hata
katika nchi za hari kwenye vipimo vya vitone mia moja. Madawa haya yaweza kuhifadhiwa kwa
muda. Waweza kuweka kwa wiki moja mbali na jua au joto kali (Chanjo hii ni ya kipekee, kwani
aina nyingine ya chanjo huwekwa kwa friji). Waweza kutoa chanjo kwa kutia vitone kwenye
mdomo. Kuku wote (wakubwa kwa wadogo) wapaswa kupewa chanjo baada ya kila miezi mitatu.
Minyoo
Minyoo kama chango (roundworms) na tegu (tapeworms) huadhiri kuku wa kienyeji. Kuku hukosa hamu ya chakula, mayai hupungua na magonjwa mengine hushambulia. Ni bora basi kutoa minyoo.
Mchanganyiko wa madawa ya aina tatu ndio hutumiwa kuangamiza minyoo, madawa haya ni
piperazine, phenothiazine na butynorate. Madawa haya hupatikana kama vidonge (tumia kidonge 1
kwa kuku mzima na 1/2 kwa vifaranga). Iwapo hautapata dawa hii, waweza kutumia Panacur au
dawa nyingine ya kuangamiza minyoo. Wapatie kuku dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu.
Wadudu
Wadudu kama chawa au utitiri husumbua kuku katika ufugaji wa kienyeji. Chawa au utitiri
husababisha harara ya ngozi, kuku walio adhiriwa hupata shida na kukosa usingizi. Hali hii
hupunguza kiwango cha mayai na uzito wa kuku.
Tumia asilimia 5% ya unga wa malathion kwa kupulizia kuku (puliza kwa chupa uliyo toboa
mashimo) pulizia kila kuku ili kuzuia chawa na utitiri (kilo moja ya unga huu yaweza kutibu kuku
150). Pulizia dawa hii baada ya kila miezi mitatu, waweza kupuliza kwa wakati mmoja wa kutoa
chanjo na dawa zilizotajwa hapo juu. Puliza unga huu pia kwenye viota vya kuangulia mayai.
Waweza kutayarisha 5% ya malathion kwa kuchanganya 25% ya unga wa malathion (kiwango cha
kilimo) na sehemu nne za jivu kutoka jikoni.
Magonjwa ya mapafu
Magonjwa ya mapafu huadhiri njia inayopitisha hewa na kuambatanisha mate na sauti kama ya
kikohozi. Ugonjwa huu huenea polepole. Uambukizanaji pia hutokea kwa polepole na vifo sio kwa
wingi. Hata hivyo, kutaga mayai na uzito hupungua. Shida hii yaweza kusambaa hata kutoka mahali vifaranga huanguliwa hadi pale walipouzwa.
Tylosin19 ndio dawa inayoweza kutibu magonjwa ya mapafu. Kiasi cha 35mg ya tylosin hutosha
kuku mmoja (kiwango hiki hufaa kuku na hata vifaranga) dawa hii husimamisha madhara kutokana
na magonjwa ya mapafu. Tibu kuku kila baada ya miezi mitatu, waweza kutekeleza kwa wakati
mmoja wa kutoa kinga na kuangamiza minyoo. Tylosin hupatikana kwa pakiti ndogo ya 4gm.
Waweza kutayarisha dawa hii kwa kutumia maji na 35gm ya tylosin (gramu nne kwa vikombe viwili
vya maji), kiasi hiki chaweza kutolewa kwa vitone kwa kila kuku.
.............................. ....//.............................. .
KWA UFUPI (SUMMARY)
Kabila za Kuku
Si rahisi kupata kabila halisi (pure breed) au kizazi halisi (pure line) za kuku wa kienyeji kutokana na mwingiliano wa vizazi kati ya aina mbalimbali za kuku hao. Lakini hata hivyo baadhi ya kuku wa kienyeji wanaweza kutambuliwa kutokana na maumbile yao kwa mfano
1. Kuchi




  • Warefuna wenye kusimama mgongo ukiwa wima
  • Wana manyoya machache mwilini na vilemba vyao ni vidogo
  • Majogoo huwa na wastani wa kilo 2.5 na mitetea kilo 1.8
  • Mayai gram 45

2. Ching'wekwe (Umbo dogo)

  • Hupatikana zaidi Morogoro na umasaini
  • Majogoo kilo 1.6
  • Mitetea kilo 1.2
  • Yai gram 37
  • kuku hawa wanafaa sana kwa biashara ya mayai kwa kuwa hutaga mayai mengi sana.

3. Umbo la Kati

  • Majogoo kilo 1.9
  • Mitetea kilo 1.1
  • Mayai gramu 43
  • Hukua upesi na hupata kinga upesi baada ya kuwachanja dhidi ya ugonjwa wa Mdondo (New Castle)

4. Singamagazi

  • Hupatikana zaidi Tabora
  • Majogoo wana rangi ya moto na mitetea rangi ya nyuki
  • Majogoo kilo 2.9
  • Mitetea kilo 2
  • Mayai gramu 56

5. Mbeya

  • Wanapatikana Ileje Mbeya na asili yao ni Malawi
  • Mjogoo kilo 3
  • Mitetea kilo 2
  • Mayai gramu 49
  • Uwezo wao wa kuatamia mayai na kuangua ni mdogo sana ukilinganisha na kuku wengine

6. Pemba

  • Maumbo ya wastani na miili myembamba
  • majogoo kilo 1.5
  • mitetea kilo 1
  • mayai gramu 42

7. Unguja

  • Hawatofautiani sana na wa Pemba
  • Vilemba vyake ni mchanganyiko- vidogo an vikubwa
  • Majogoo kilo 1.6
  • Mitetea kilo 1.2
  • Mayai gramu 42

SIFA WA KUKU WA KIENYEJI

  1. Wastahimilivu wa Magonjwa
  2. Wana uwezo wa kujitafutia chakula
  3. Huatamia, kutotoa na kulea vifaranga
  4. Wanastahimili mazingira magumu(ukame, baridi n.k)
  5. Nyama yake ina ladha nzuri

KATIKA KUWAENDELEZA KUKU WA KIENYEJI NI VYEMA

  1. Wajengewe nyumba bora
  2. Wapewe kinga dhidi ya ugonjwa wa Mdondo (New Castle), Ndui (Fowl Pox) pamoja na kinga ya minyoo.
  3. Malezi bora ya vifaranga
  4. Kuwapatia chakula cha ziada pamoja na maji ya kunywa ya kutosha.

NYUMBA BORA
Eneo inapojengwa nyumba au banda la kuku liwe

  • Linafikika kwa urahisi
  • Limeinuka juu pasituame maji
  • Pasiwe na pepo zinazovuma

Vifaa kama miti, nyasi, makuti, fito, udongo mabanzi ya miti, cement, mabati n.k
Sifa za Nyumba Bora ya Kuku

  • Paa imara lisilovuja
  • Kuta zisiwe na nyufa
  • Sakafu isiwe na nyufa
  • Madirisha ya kutosha kupitisha hewa
  • Iwe na mlango wa kuingia kufanya usafi
  • Iwe na ukubwa (nafasi) unaolingana na idadi ya kuku. Wastani wa kuku 10-15 kwa mita moja mraba

Mambo muhimu ndani ya nyumba

  • Chaga za kulalia kuku
  • Sakafu iwekwe maranda (wood shavings), makapi ya mpunga, n.k
  • Viota vya kutagia mayai sentimita 35x35x35 na idadi ya viota iwe nusu ya idadi ya kuku waliofikia hatua ya kutaga na viwekwe sehemu iliyojificha (faragha)

UATAMIAJI WA MAYAI
Kuna njia 2

  • Njia ya kubuni (incubators)
  • Asili

Kumuandaa kuku anayeatamia

  • Weka maranda au majani makavu ndani ya kiota
  • Anapokaribia kuatamia toa mayai ndani ya kiota pamoja na maranda, hakikisha mikono haina manukato
  • Nyunyiza dawa ya kuua wadudu (viroboto, utitiri n.k) ndani ya kiota, pia mnyunyizie dawa kuku anayetarajia kulalia mayai
  • Rudisha mayai kwenye kiota ili kuku aanze kuatamia
  • Kwa kawaida kuku hulalia mayai yake kwa muda wa siku 21 ndipo huanguliwa

ULEAJI WA VIFARANGA
Kuna njia mbili

  • Njia ya kubuni
  • Njia ya asili

Njia ya ASILI
Kuku mwenyewe hutembea na vifaranga akivisaidia kutafuta chakula. Ni vizuri kumtenga kuku mwenye vifaranga katika chumba chake pekee ili vifaranga wasishambuliwe na kuku wengine hali kadhalika kuwalinda na wanyama na ndege wanaoshambulia vifaranga.
Njia ya KUBUNI
Vifaranga huwekwa kwa pamoja kwenye chumba maalum na kupatiwa joto maalum, chakula pamoja na maji. Tumia taa ya kandili (chemli), umeme au jiko la mkaa na hiyo taa iweke kwenye mzingo(mduara) walipo vifaranga. Pia kuna kifaa kinaitwa Kinondoni Brooder ni kizuri kwa kutunzia vifaranga. Kwa kutumia kifaa hiki kuku wanaweza kunyang'anywa vifaranga vyao mara tu baada ya kutotoa na kuviweka kwenye hii brooder na hao kuku wakaachwa bila vifaranga vyao, baada ya majuma matatu au manne, kuku hao huanza tena utagaji na kuendelea na uatamiaji hadi kutotoa tena. Kwa mtindo huu kuku anaweza kutotoa mara 5-6 badala ya kama ilivyo sasa mara 2-3 kwa mwaka. Vifaranga vikae ndani ya brooder majuma 3-4 na baadaye fungua milango ya brooder kuruhusu vifaranga vitoke na kuzungukazunguka chumbani bila kuvitoa nje kw kipindi cha mwezi mmoja au zaidi kutegemeana na mazingira.
KULISHA KUKU WA KIENYEJI
Kuku mkubwa huhitaji gramu 120 za chakula kwa siku, ni vizuri kuku wanaofugwa huria (free range) kupatiwa chakula cha ziada gramu 30 kila siku nyakati za jioni.
Kuku walishwe

  • Mizizi-mihogo, viazi vitamu, mbatata, magimbi, n.k
  • Nafaka-mahindi, Mpunga, Mtama, Ulezi na Pumba za nafaka zote
  • Mboga-Mikundekunde, nyanya, milonge, majani ya mapapai
  • Matunda-Mapapai, maembe, n.k
  • Mbegu za Mafuta-Karanga, ufuta, mashudu ya pamba, alizeti, n.k
  • Unga wa dagaa
  • Maji

KUCHANGANYA CHAKULA CHA KUKU

  • Pumba.............kilo20
  • Mashudu ya Pamba n.k...kilo 3
  • Dagaa iliyosagwa.........kilo 1
  • Unga wa majani uliokaushwa kivulini na kusagwa........kilo 2
  • Unga wa Mifupa ..........kilo 0.25
  • Chokaa ya mifugo ........kilo 0.25
  • Chumvi........................ gramu 30
  • Vichanganyio/Premix...gramu 25

KUPANDISHA

  • Uwiano wa mitetea na jogoo ni mitetea 10-12 kwa jogoo mmoja
  • Sifa za mtetea ni mkubwa kiumbo, mtagaji mayai mengi, muatamiaji mzuri na mlezi wa vifaranga
  • Sifa za jogoo ni awe mkubwa kiumbo, miguru imara na yenye nguvu, mrefu, upanga/kilemba kikubwa, awe na uwezo wa kuitia chakula mitetea na awe na tabia ya kupenda vifaranga
  • Jogoo huanza kupanda akiwa na umri wa miezi 7-10 na kuendelea hadi miaka mitatu na asipande watoto wake
  • Mitetea huanza kutaga wakiwa na miezi 6-8

MAGONJWA YA KUKU
1. Mdondo/New castle
Virus vinavyosababisha ugonjwa huu huenezwa kwa hewa
Dalili

  • Kuhalisha choo cha kijani na njano
  • Kukohoa na kupumua kwa shida
  • Kupinda shingo kwa nyuma
  • Kuficha kichwa katikati ya miguu
  • Kukosa hamu ya kula na kunywa
  • Idadi kubwa ya vifo hadi 90%

Kinga

  • Chanjo (New Castle vaccine) kwa mpango wa siku 3, wiki 3, miezi 3
  • Epuka kuingiza kuku wageni
  • Choma au fukie mizoga ya kuku waliokufa kwa ugonjwa
  • Zingatia usafi wa mazingira

NDUIYA KUKU/ FOWL POX
Virus huambukizwa kupitia jeraha au mbu
Dalili

  • Vidonda vyenye utando wa kahawia/purple kwenye sehemu zinazoonekana
  • Kukosa hamu ya kula
  • Vifo vingi

Kinga

  • Chanja vifaranga wanapofikia mwezi 1-2 kwa kutumia chanjo ya Fowl pox vaccine
  • Epuka kuingiza kuku wageni
  • Zingatia usafi wa mazingira

HOMA YA MATUMBO/FOWL TYPHOID

  • Kuharisha kinyesi cha kijani na nyeupe
  • Kuku hukosa hamu ya kula
  • Kuku hukonda
  • Vifo hutokea kidogo kidogo kwa muda mrefu
  • Kinyeshi hushikamana na manyoya

Tiba
Dawa aina ya antibiotic, sulfa na vitamini
Kinga

  • Usafi
  • Fukia mizoga
  • Usiingize kuku wageni
  • Chinja kuku wote mara ugonjwa huu ukiingia na safisha banda, pia pumzika kufuga kwa miezi 6

MAFUA YA KUKU/INFECTIOUS CORYZA
Hutokana na bakitelia na hushambulia hasa kuku wakubwa
Dalili

  • Kuvimba uso
  • Kamasizilizochanganyikana na usaha unaonuka
  • Macho huvimba na kutoa machozi na pengine upofu
  • Hukosa hamu ya kula
  • Mbawa huchafuka na kutoa harufu mbaya

Tiba
Dawa za Antibiotic, sulfa na vitamini
KUHALISHA DAMU/COCCIDIOSIS
Husababishwa na vijidudu vya Protozoa
Dalili

  • Kuharisha damu
  • Manyoya husimama
  • Hulala na kukosa hamu ya kula

MINYOO
Dalili

  • Kunya minyoo
  • Hukosa hamu ya kula
  • Hukonda au kudumaa
  • Wakati mwingine hukohoa

Tiba
Dawa ya minyoo/Pipeazine citrate kila baada ya miezi mitatu
WADUDU
Viroboto, chawa, utitiri
Dalili

  • Kujikuna na kujikung'uta
  • Manyoya kuwa hafifu
  • Rangi ya upanga kuwa hafifu
  • Ngozi kuwa nene, ngumu na yenye magamba yanayodondoka kama unga

Kuzuia

  • Ziba mipasuko sakafuni na kwenye kuta za banda
  • Fagia banda mara mbili kwa wiki
  • Nyunyiza majivu au chokaa mara moja kwa wiki mara baada ya kufagia
  • Choma masalia ya mayai yaliyoanguliwa
  • Nyunyiza dawa kwenye viota
  • Weka maranda, majani makavu, makapi ya mpunga ya kutosha sakafuni ndani ya banda la kuku
  • Fuata kanuni za chanjo
  • Tenga kuku wagonjwa wakae mbali na kuku wazima

UPUNGUFU WA VIINI LISHE KWENYE CHAKULA
Dalili

  • Kuku hupungua damu, uzito na kudumaa
  • Mifupa huwa laini na kutokuwa imara
  • Hutaga mayai yenye gamba laini na madogo
  • Huwa na manyoya dhaifu,

Categories:

Leave a Reply