Mawasiliano
bora ni muhimu sana kwa mafanikio yetu katika nyanja
mbalimbali. Kama
hatuna mawasiliano yaliyobora au hatuwezi kuwasiliana inavyotakiwa basi itakuwa
ngumu kwa watu wengine kutusaidia katika kile tunachokihitaji. Mawasiliano yasiyo bora au kushindwa
kuwasiliana vema kunadumaza na mara nyingine kuua kabisa mahusiano baina yetu na wengine. Kwa
maana hii basi hauna budi kuzingatia sana maelezo na ushauri kutoka katika mada
hii na kuyaweka maelezo haya katika matendo ili yakusaidie maishani.
Vitu vya kuzingatia.
- Yatazame au yachukulie mazungumzo yako na wale unaohusiana nao kama majadiliano ya kawaida tu na sio mashindano.
Hii
itakusaidia kuwa na mahusiano na mawasiliano bora na wengine hususani pale
utakapoyaona yale mnayozungumza mara kwa mara kama
majadiliano na siyo mashindano. Majadiliano ni mazungumzo yenye kusudi la
kufikia suluhisho au muafaka fulani. Ni
mazungumzo ambayo yanapotumika nia yake siyo kumuumiza, kumuumbua mtu bali kutoa
nafasi kwa pande zote kufikia matokeo bora.
Mazungumzo
ya yenye ushindani ni yale yenye nia ya kuumiza, kuumbua, kuaibisha, na kudharaulisha,
na ambayo nia yake ni kumuonyesha mshindi na aliyeshindwa mwishoni mwa
mazungumzo hayo.
Wale
wenye tabia ya kuzungumza kiushindani huyachukulia mazungumzo kama
nafasi ya kuonyesha ubabe au kunyanyasa wengine. Hata kama yule mnayezungumza naye ana nia ya mashindano,
wewe fanya majadiliano ya kawaida ili taratibu uweze kumbadilisha mtazamo wake.
- Kuwa msikilizaji makini na hitaji kusikilizwa pia
Kati
ya alama za uonyesha kuwa wewe ni mwenye mawasiliano bora ni pamoja na uwezo wa
kuwa msikilizaji mzuri. Wako watu ambao
hupenda kuongea tu na sio kusikiliza.
Sambamba na hilo,
unatakiwa kuomba na wewe pia usikilizwe vizuri. Muombe yule anayekusikiliza
akuache umalize kuongea ndio na yeye aanze kuongea. Kamwe hamtafikia muafaka wowote ikiwa wote
wawili mnaongea kwa wakati mmoja.
Yafuatayo yatakuwezesha kuwa msikilizaji
mzuri
-
Msikilize yule anaeongea kwanza na kumuelewa
-
Fahamu fika kile kinachozungumzwa elewa nia na dhumuni
la majadiliano
-
Uliza swali pale unapodhani hujaelewa ili uweze kuelewa
vema nia ya mzungumzaji
-
Jaribu kuweka kwa kifupi au kwa muhtasari kile
kilichozungumzwa, mweleze anayezungumza unavyojihisi juu ya alichokuwa akikieleza, na hakikisha ulimuelewa vema.
-
Eleza unavyofikiri wewe. Mweleze aliyekuwa anazungumza kama umekubaliana nae au la, toa sababu za kukubaliana au
kutokukubaliana.
- Kuwa mzungumzaji mwenye ujasiri.
ujasiri
katika mazungumzo huchochea uhalisi na kuaminika katika kile unachokisema.
Zifuatazo ni tabia za mzungumzaji bora;
a)
Tumia sentensi zinazokuelekea wewe zaidi ya sentensi zinazo
waelekea wengine. Jilenge wewe zaidi ya kuwalenga wenzako unapozungumza.
unapotumia sentensi za “ninyi” au “wewe” mara nyingi unaweza kuonekana usiye
na ujasiri, tofauti na pale unapotumia sentensi zenye “mimi”. Unaweza kuonekana pia kama
usiye yaamini maneno yako.
Sentensi zenye ujasiri na zenye kukulenga wewe
binafsi ni kama vile
“nimefurahi kukuona”
“Ningependa kuzungumza na wewe”
“Sijafurahishwa na maneno yako”
b)
Katika
mazungumzo yako tumia zaidi sentensi na siyo maswali. Hii itakuwezesha
pia kuonyesha kuwa unaujasiri katika kile
unachokisema na unajiamini wewe
mwenyewe pia.
Mfano wa mazungumzo yakutumia swali: “Hivi ninyi mnamwonaje yule rafiki
yetu?”
Badala yake ungetekiwa kusema
“mimi sifurahishwi na matendo ya huyu rafiki yetu”
Au maranyingine baba wa nyumba anapouliza “Hivi mnadhani nani baba humu
ndani?” hii huonyesha kutojiamini kwake
“Hivi unafikiri mimi njinga?”
“Hivi jamani sisi hatupewi
huduma?”
Namna nyingine bora zaidi ya
kuuliza swali
-
Je waweza kunisaidia tafadhali?
-
Je utakubali kuoana na mimi?
Namna
bora ya kuzungumza katika sentensi
-
nitafurahi sana
ikiwa utakubali kuoana namimi.
-
Nitafurahi sana
kupata msaada kutoka kwako
c)
Tumia zaidi sentensi zenye “kukiri” na sio sentensi
zenye lawama. Sentensi zenye ukiri au kukiri ni zile ambazo anayezungumza
anasema kile ambacho angetaka aone kikifanyika au kile ambacho angependa akione
kikitendeka.
Kinyume chake ni sentensi zenye lawama; hizi ni zile ambazo mzungumzaji
ana sema kile asichotaka, au kile asichokipenda kitokee au kifanyike.
Mfano wa sentensi
zenye lawama:
·
Sipendi kabisa vile unavyonichukulia
·
Sipendi kabisa unavyoniingilia katika maongezi
Mfano wa sentesi zenye kukiri; “Ningefurahi kama ungesubiri nimalize
kwanza kuongea halafu na wewe utaongea”
Sentensi zenye lawama huonyesha ukosefu wa ujasiri kwa mzungumzaji, mbaya zaidi, sentensi hizi hazisaidii
chochote katika kubadili tabia ya yule anayeambiwa maana hazionyeshi bayana ni
nini kinachotakiwa kufanyika.
Sentensi zenye lawama pia huonyesha wazi tabia yako sugu ya kulaumu, pia huonyesha
vitu usivyovipenda tu, na kuvisahau vile vizuri unavyovipenda. Ni ngumu sana kumsaidia mtu ambaye analaumu usiku na
mchana kuwa hapendi hiki, hapendi kile, hataki hiki na wala hataki kile na bado
hawezi kusema anapenda au kutaka nini badala yake. Kwa hali hii watu hawa wanabaki kuwa walaumu
mara dufu.
- Lugha ya mwili wako iwe nzuri (Positive Body language)
Lugha
ya mwili ni vile tunavyoweza kutumia miili yetu kuonyesha nia zetu.
Mwili ni kiungo muhimu sana cha mawasiliano. Tafiti zinasema kwamba,
hata wakati mtu
anazungumza kupitia mdomo, asilimia 60 (sitini) ya ujumbe wake kupitia
au
kueleweka sio kwa kupitia maneno ya kinywani mwake bali ni kwa kupitia
lugha ya
mwili wake. Jambo hili ndilo hutiliwa mkazo na ule usemi usemao
“matendo husungumza
zaidi kuliko maneno”
Lugha
ya mwili huusisha vitu kama vile; muonekano wa
sura (facial impression), mikunjo ya uso, macho yalivyowekwa, kinywa kilivyo
tumiwa, pua inavyofanywa wakati wa kuongea, mikono na pozi ya mwili ilivyo
wakati wa kuzungumza.
Ni
vema kujikumbusha kila wakati kuhusu umuhimu wa lugha ya mwili ili itusaidie
kujijua sisi wenyewe na ule ujumbe tunaoutuma.
Hapa
nataka kujaribu kueleza baadhi ya maeneo ya lugha ya mwili ambayo yatakusaidia
kuweza kubadilika au kujirekebisha katika mchakato mzima wa mawasiliano kupitia
mwili wako.
a) Kutembea kwa hatua za kudunda au kunesa
Kutembea huku kuwasilisha hisia za ujasiri. Tabia hii huweza kuwa ya asili
au ya kujifanyisha hususani apale unapodhani kuwa unachofanya ni cha muhimu
zaidi na unapoamini kuwa wewe ni bora zaidi. Kutembea kwako kwaweza
kuonyesha kila kinachoendelea akilini
mwako.
b) Kupanda au kushuka, uzito au wepesi wa
sauti unapoongea (Tone of voice)
Pale unapojua hauna ugomvi au uadui na yeyote basi sauti yako itakuwa
nzuri, na yakiasi cha kusikika na yeyote.
Vituo vyako na misemo yako itakuwa ya kawaida na yenye uwiano. Pale
unapohisi hofu, au kuwepo kwa wabaya wako, mara nyingi sauti yako huwa chini na
isiyo na ujasiri.
Unashauriwa kwa hali yoyote ujitahidi kuzungumza kwa sauti ya kati, isiyo
chini sana wala juu sana.
c) Mavazi sahihi
Unapohisi una nafasi fulani katika jamii au sehemu fulani utajikuta
unajali sana suala
la kuvaa kwako. Mavazi huweza kuzungumza nia ya moyo na huweza kuonyesha picha
mbaya au nzuri kwa wanao kutazama. Mavazi ya aina fulani huweza kukupa tafsiri
mbaya kwa watu tofauti na vile ulivyo kihalisia, au kwa upande mwingine mavazi
mengine yamefanya wengine kuonekana kama vile ni wa maana sana na wakutegemewa wakati uhalisi haukuwa
hivyo
d) Pozi zuri la mwili
Kuketi au kutembea katika mwili ulionyooka huonyesha ujasiri. Hii inamaana kifua kinakuwa mbele na tumbo
ndani kidogo. Hata askari waliojasiri huwa
hulazimika kuwa katika pozi hili. Pozi
zuri ni ishara ya ukakamavu na afya njema pia.
e) Muonekano wa macho
Muonekano wetu machoni huweza huonyesha hofu, aibu au ujasiri, hususani
tunapokutwa katika maeneo au matukio ambayo hatukutarajia. Muonekano wa macho
huthibitisha ukweli au uongo wa kile tunachozungumza. Muonekano wa macho yetu huweza pia
kuthibitisha kumaanisha au kutokumaanisha, uhakika au kutokuwa na uhakika
katika kile tunachokizungumza. Wako wengine wasioweza kamwe kuwatazama machoni
wale wanaowahofia au kuwaogopa.
f) Ukaribu au mgusano
Tabia ya kujitenga na wengine huweza kumaanisha kujikweza au kukosa
ujasiri. Jaribu kuwa karibu na wengine
zaidi kadri utamaduni wa jamii uliyopo unavyokuruhusu. Kama kukumbatia kunaruhusiwa katika jamii
yako fanya hivo, kama kushika mkono ndio
kunakoruhusiwa basi hakikisha unafanya hivyo, mara kwa mara. Mgusano wa mwili
unamaana kubwa sana
katika kuongeza ukaribu baina ya watu.
g) Ishara za mwili (gestures)
Tumia ishara unapoongea. Mfano tumia mikono, tumia kichwa na macho
kusisitiza unachoongea. Kuongea tu kwa
madomo pasipo kiungo chochote cha mwili, hufanya mazungumzo yako huwa
butu sana. Ishara za mwili tunazitumia kusisitiza au kuthibitisha
tunachokiongea. Ishara hizi za mwili
zitumike taratibu, zisizidishwe sana
maana na zaweza kuwabughudhi wengine.
Chris Mauki
Social, Relationship and Counseling Psychologist
E-mail: chrismauki57@gmail.com
Categories: