Mawasiliano bora  ni muhimu sana kwa mafanikio yetu katika nyanja mbalimbali.  Kama hatuna mawasiliano yaliyobora au hatuwezi kuwasiliana inavyotakiwa basi itakuwa ngumu kwa watu wengine kutusaidia katika kile tunachokihitaji.  Mawasiliano yasiyo bora au kushindwa kuwasiliana vema kunadumaza na mara nyingine kuua  kabisa mahusiano baina yetu na wengine.  Kwa  maana hii basi hauna budi kuzingatia sana maelezo na ushauri kutoka katika mada hii na kuyaweka maelezo haya katika matendo ili yakusaidie maishani.
Vitu vya kuzingatia.
  1. Yatazame au yachukulie mazungumzo yako na wale unaohusiana nao kama majadiliano ya kawaida tu na sio mashindano.
Hii itakusaidia kuwa na mahusiano na mawasiliano bora na wengine hususani pale utakapoyaona yale mnayozungumza mara kwa mara kama majadiliano na siyo mashindano. Majadiliano ni mazungumzo yenye kusudi la kufikia suluhisho au muafaka fulani.  Ni mazungumzo ambayo yanapotumika nia yake siyo kumuumiza, kumuumbua mtu bali kutoa nafasi kwa pande zote kufikia matokeo bora. 
Mazungumzo ya yenye ushindani ni yale yenye nia ya kuumiza, kuumbua, kuaibisha, na kudharaulisha, na ambayo nia yake ni kumuonyesha mshindi na aliyeshindwa mwishoni mwa mazungumzo hayo.
Wale wenye tabia ya kuzungumza kiushindani huyachukulia mazungumzo kama nafasi ya kuonyesha ubabe au kunyanyasa wengine. Hata kama  yule mnayezungumza naye ana nia ya mashindano, wewe fanya majadiliano ya kawaida ili taratibu uweze kumbadilisha mtazamo wake.
  1. Kuwa msikilizaji makini na hitaji kusikilizwa pia
Kati ya alama za uonyesha kuwa wewe ni mwenye mawasiliano bora ni pamoja na uwezo wa kuwa msikilizaji mzuri.  Wako watu ambao hupenda kuongea tu na sio kusikiliza.  Sambamba na hilo, unatakiwa kuomba na wewe pia usikilizwe vizuri. Muombe yule anayekusikiliza akuache umalize kuongea ndio na yeye aanze kuongea.  Kamwe hamtafikia muafaka wowote ikiwa wote wawili mnaongea kwa wakati  mmoja.
Yafuatayo yatakuwezesha kuwa msikilizaji mzuri
-          Msikilize yule anaeongea kwanza na kumuelewa
-          Fahamu fika kile kinachozungumzwa elewa nia na dhumuni la majadiliano
-          Uliza swali pale unapodhani hujaelewa ili uweze kuelewa vema nia ya mzungumzaji
-          Jaribu kuweka kwa kifupi au kwa muhtasari kile kilichozungumzwa, mweleze anayezungumza unavyojihisi juu ya  alichokuwa akikieleza, na hakikisha  ulimuelewa vema.
-          Eleza unavyofikiri wewe.  Mweleze aliyekuwa anazungumza kama umekubaliana nae au la, toa sababu za kukubaliana au kutokukubaliana.
  1. Kuwa mzungumzaji mwenye ujasiri.
ujasiri katika mazungumzo huchochea uhalisi na kuaminika katika kile unachokisema.
Zifuatazo ni tabia za mzungumzaji bora;
a)      Tumia sentensi zinazokuelekea wewe zaidi ya sentensi zinazo waelekea wengine. Jilenge wewe zaidi ya kuwalenga wenzako unapozungumza. unapotumia sentensi za “ninyi” au “wewe” mara nyingi unaweza kuonekana usiye na ujasiri, tofauti na pale unapotumia sentensi zenye “mimi”. Unaweza kuonekana pia kama usiye yaamini  maneno yako.
      Sentensi zenye ujasiri na zenye kukulenga wewe binafsi ni kama vile
 “nimefurahi kukuona”
 “Ningependa kuzungumza na wewe”   
“Sijafurahishwa na maneno yako”
b)      Katika  mazungumzo yako tumia zaidi sentensi na siyo maswali. Hii itakuwezesha pia kuonyesha kuwa unaujasiri katika kile  unachokisema na unajiamini  wewe mwenyewe pia.
Mfano wa mazungumzo yakutumia swali: “Hivi ninyi mnamwonaje yule rafiki yetu?”
Badala yake  ungetekiwa kusema “mimi sifurahishwi na matendo ya huyu rafiki yetu”
Au maranyingine baba wa nyumba anapouliza “Hivi mnadhani nani baba humu ndani?” hii huonyesha kutojiamini kwake
“Hivi unafikiri mimi njinga?”
“Hivi jamani  sisi hatupewi huduma?”
Namna nyingine bora zaidi ya kuuliza swali
-          Je waweza kunisaidia tafadhali?
-          Je utakubali kuoana na mimi?
       Namna bora ya kuzungumza katika sentensi
-          nitafurahi sana ikiwa utakubali kuoana namimi.
-          Nitafurahi sana kupata msaada kutoka kwako
c)      Tumia zaidi sentensi zenye “kukiri” na sio sentensi zenye lawama. Sentensi zenye ukiri au kukiri ni zile ambazo anayezungumza anasema kile ambacho angetaka aone kikifanyika au kile ambacho angependa akione kikitendeka.
Kinyume chake ni sentensi zenye lawama; hizi ni zile ambazo mzungumzaji ana sema kile asichotaka, au kile asichokipenda kitokee au kifanyike.
Mfano wa sentensi zenye lawama:
·         Sipendi kabisa vile unavyonichukulia
·         Sipendi kabisa unavyoniingilia katika maongezi
Mfano wa sentesi zenye kukiri; “Ningefurahi kama ungesubiri nimalize kwanza kuongea  halafu na wewe utaongea”
Sentensi zenye lawama huonyesha ukosefu wa ujasiri kwa mzungumzaji,  mbaya zaidi, sentensi hizi hazisaidii chochote katika kubadili tabia ya yule anayeambiwa maana hazionyeshi bayana ni nini kinachotakiwa kufanyika.
Sentensi zenye lawama pia huonyesha wazi tabia yako sugu ya kulaumu, pia huonyesha vitu usivyovipenda tu, na kuvisahau vile vizuri unavyovipenda.  Ni ngumu sana kumsaidia mtu ambaye analaumu usiku na mchana kuwa hapendi hiki, hapendi kile, hataki hiki na wala hataki kile na bado hawezi kusema anapenda au kutaka nini badala yake.  Kwa hali hii watu hawa wanabaki kuwa walaumu mara dufu.
  1. Lugha ya  mwili wako iwe nzuri (Positive Body language)
Lugha ya mwili ni vile tunavyoweza kutumia miili yetu kuonyesha nia zetu.  Mwili ni kiungo muhimu sana cha mawasiliano.  Tafiti zinasema kwamba, hata wakati mtu anazungumza kupitia mdomo, asilimia 60 (sitini) ya ujumbe wake kupitia au kueleweka sio kwa kupitia maneno ya kinywani mwake bali ni kwa kupitia lugha ya mwili wake.  Jambo hili ndilo hutiliwa  mkazo na ule usemi usemao “matendo husungumza zaidi kuliko maneno”
Lugha ya mwili huusisha vitu kama vile; muonekano wa sura (facial impression), mikunjo ya uso, macho yalivyowekwa, kinywa kilivyo tumiwa, pua inavyofanywa wakati wa kuongea, mikono na pozi ya mwili ilivyo wakati wa kuzungumza.
Ni vema kujikumbusha kila wakati kuhusu umuhimu wa lugha ya mwili ili itusaidie kujijua sisi wenyewe na ule ujumbe tunaoutuma.
Hapa nataka kujaribu kueleza baadhi ya maeneo ya lugha ya mwili ambayo yatakusaidia kuweza kubadilika au kujirekebisha katika mchakato mzima wa mawasiliano kupitia mwili wako.
a)      Kutembea kwa hatua za kudunda au kunesa
Kutembea huku kuwasilisha hisia za ujasiri. Tabia hii huweza kuwa ya asili au ya kujifanyisha hususani apale unapodhani kuwa unachofanya ni cha muhimu zaidi na unapoamini kuwa wewe ni bora zaidi. Kutembea kwako kwaweza kuonyesha  kila kinachoendelea akilini mwako.
b)     Kupanda au kushuka, uzito au wepesi wa sauti unapoongea (Tone of voice)
Pale unapojua hauna ugomvi au uadui na yeyote basi sauti yako itakuwa nzuri, na yakiasi cha kusikika na yeyote.  Vituo vyako na misemo yako itakuwa ya kawaida na yenye uwiano. Pale unapohisi hofu, au kuwepo kwa wabaya wako, mara nyingi sauti yako huwa chini na isiyo na ujasiri.
Unashauriwa kwa hali yoyote ujitahidi kuzungumza kwa sauti ya kati, isiyo chini sana wala juu sana.
c)      Mavazi sahihi
Unapohisi una nafasi fulani katika jamii au sehemu fulani utajikuta unajali sana   suala la kuvaa kwako. Mavazi huweza kuzungumza nia ya moyo na huweza kuonyesha picha mbaya au nzuri kwa wanao kutazama. Mavazi ya aina fulani huweza kukupa tafsiri mbaya kwa watu tofauti na vile ulivyo kihalisia, au kwa upande mwingine mavazi mengine yamefanya wengine kuonekana kama vile ni wa maana sana na wakutegemewa wakati uhalisi haukuwa hivyo
d)     Pozi zuri la mwili
Kuketi au kutembea katika mwili ulionyooka huonyesha ujasiri.  Hii inamaana kifua kinakuwa mbele na tumbo ndani kidogo.  Hata askari waliojasiri huwa hulazimika kuwa katika pozi hili.  Pozi zuri ni ishara ya ukakamavu na afya njema pia.
e)      Muonekano wa macho
Muonekano wetu machoni huweza huonyesha hofu, aibu au ujasiri, hususani tunapokutwa katika maeneo au matukio ambayo hatukutarajia. Muonekano wa macho huthibitisha ukweli au uongo wa kile tunachozungumza.  Muonekano wa macho yetu huweza pia kuthibitisha kumaanisha au kutokumaanisha, uhakika au kutokuwa na uhakika katika kile tunachokizungumza. Wako wengine wasioweza kamwe kuwatazama machoni wale wanaowahofia au kuwaogopa. 
f)       Ukaribu au mgusano
Tabia ya kujitenga na wengine huweza kumaanisha kujikweza au kukosa ujasiri.  Jaribu kuwa karibu na wengine zaidi kadri utamaduni wa jamii uliyopo unavyokuruhusu.  Kama kukumbatia kunaruhusiwa katika jamii yako fanya hivo, kama kushika mkono ndio kunakoruhusiwa basi hakikisha unafanya hivyo, mara kwa mara. Mgusano wa mwili unamaana kubwa sana katika kuongeza ukaribu baina ya watu.
g)      Ishara za mwili (gestures)
Tumia ishara unapoongea. Mfano tumia mikono, tumia kichwa na macho kusisitiza unachoongea.  Kuongea tu kwa madomo pasipo kiungo chochote cha mwili, hufanya mazungumzo yako huwa butu sana.  Ishara za mwili tunazitumia kusisitiza au kuthibitisha tunachokiongea.  Ishara hizi za mwili zitumike taratibu, zisizidishwe sana maana na zaweza kuwabughudhi wengine.
Chris Mauki
Social, Relationship and Counseling Psychologist
E-mail: chrismauki57@gmail.com

Categories:

Leave a Reply