MTU yeyote aliyevunjika moyo au kukata tamaa kutokana na mambo magumu
yaliyompata, iwe ni kuyumba kiuchumi, kufiwa na ampendaye, kukimbiw
a na
watoto, maradhi yasiyotibika au kuachwa na mume au mke, huwa anapata
maumivu makali yanayokata kama kisu ndani na hata kuathiri hisia, fikra
pamoja na maamuzi anayoweza kuyafanya.
Maisha yaliyojaa utoshelevu na mafanikio na uwezo wa kupata kila kitu
cha muhimu unachokihitaji, ikiwa ni pamoja na ndoto zako nyingi
kutimizwa, yaweza kubadilika kabisa na kuwa kinyume cha hapo kiasi cha
kufanya mtu ahisi hana sababu tena ya kuishi iwapo sababu au vigezo
vyote vilivyokuwa vikikupa utoshelevu na furaha vimetoweka!
Watu uliowazoea na kushirikiana nao wanaweza kukutenga au kukushusha
hadhi mara wagunduapo kuwa meli yako yakaribia kuzama, iwe ni kiuchumi,
kijamii au kiafya.
Inaaminika kuwa haijalishi ni sababu gani kubwa iliyomfanya mtu kukata
tamaa ya maisha, kuvunjika moyo, au kuwa na msongo wa mawazo.
Njia inayotumika ili kuponya na kurejesha katika uzima na ubora wa
maisha ni ile ile kwa kila mtu.
Mungu hafurahishwi na kushindwa kwetu, naye huumia pamoja nao wanaoumia
lakini yupo tayari kuponya vidonda vyote vilivyoshindikana kupona ili
kufanya upya tena.
Madaktari husema mfupa uliovunjika ukiunga unakuwa na nguvu zaidi pale
palipokuwa pamevunjika kuliko sehemu nyingine za huo mfupa.
Ndivyo ilivyo hata kwa mtu aliyekata tamaa na kuvunjika moyo anapokubali
kuchukua hatua za kupambana na hali yake hiyo, mwisho wa siku aweza
kuwa mwenye nguvu na bora kuliko alivyokuwa hapo awali.
Hebu tuangalie kanuni za kukabiliana na hali ya kukata tamaa. Kwanza
yatakiwa ukubaliane na zile hali ambazo huwezi kuzibadili tena. Kumbuka
yapo mambo katika maisha yako, hata ungejaribu kwa jitihada kubwa sana
kuyabadili usingaliweza.
Mfano: Huwezi kubadili hali ya hewa, huwezi kubadili majira au mzunguko
wa saa, huwezi kubadili yaliyokwisha kupita, Huwezi kubadili ukweli
kwamba umpendaye kakutoka na mambo mengine yafananayo na hayo.
Wakati mwingine waweza kulazimika kukubaliana na majibu ya kukatisha
tamaa ya daktari yanayoashiria mwisho wa maisha au ugonjwa usio na tiba
lakini bado ukiwa na amani moyoni na kumuachia Mungu aamue, waweza
kukubaliana na matokeo.
Ufunguo wa amani moyoni ni pale unapokubali kuwa huwezi kubadili
matatizo mengine bali waweza kuacha mikononi mwa Muumba ambaye ni mkuu
kupita wote.
Muombe Mungu akujalie neema kukubaliana na vile usivyoweza kuvibadili
pia akujalie nguvu kubadili vile unavyoweza na hekima ya kujua utofauti.
Yakupasa kusimama ili kukabiliana na changamoto yako mwenyewe. Kamwe
usikimbie matatizo! Hakuna mtu yeyote anayependa kuaibika, kuaibishwa au
udhaifu wake kuanikwa hadharani kwa kila mtu kuuona, zaidi sana
inapokuwa kwamba yeye ni mtu mwenye heshima au dhamana katika jamii yake
aliyopo.
Mfano: Wakati mwingine tunajitwika lawama tusizostahili ili tu
kuhalalisha au kubadili mwonekano halisi uwe tofauti.
Tupo tayari kuingia gharama iwayo yoyote kuzuia au hata kuahirisha
matukio ya uchungu maishani, lakini mara nyingi hizi huwa ni mbio za
sakafuni ambazo huishia ukingoni.
Kamwe usikimbie changamoto zinazokukabili kimaisha. Simama kidete
kubaliana na ukweli halisi ya kwamba mambo mengine huwezi kuyabadili
bali kuyakubali.
Mtu huheshimika kwa jinsi awezavyo kukabiliana na changamoto zake
mwenyewe za maisha.
Fahamu kuwa huwezi kubadili mitazamo ya watu wengine juu yako. Waweza
kubadili mtazamo wako mwenyewe na matendo yako, na hapo ndipo watu
wanaokuzunguka watakapobadili mitazamo yao juu yako kutokana na badiliko
lako.
Mfano: Iwapo unataka jamii ikuchukulie kama mtu anaye jiheshimu, mkarimu
au mwenye kujithamini ni lazima na wewe mwenyewe uishi kama unavyotaka
watu hao wakuchukulie.
Huwezi kutegemea kuheshimiwa na watu iwapo wewe mwenyewe haujiheshimu au
hauthamini utu wako.
Watu wengi hupenda kuheshimiwa au kusifiwa hata kwa mambo ambayo
hawastahili au hawajayafanya; kwa kisingizio cha cheo au dhamana katika
jamii husika.
Lakini mwisho wa siku ukweli unapokuja kudhihirika, unakuwa umeshusha
kabisa hadhi na dhamana yake katika jamii.
Hivyo uponyaji wa kihisia unaanza pale unapochukua hatua kubwa ya kwanza
ya kukubaliana na hali halisi juu ya vile vitu ambavyo huwezi
kubadilisha.
Kukubali inamaanisha kuacha kuzuia yasiyozuilika. Mfano, huwezi
kumlazimisha mtu kufanya asiyotaka kufanya. Huwezi kubadili kifo au
ugonjwa nk.
Kukubali huondoa maumivu mengi yaliyojificha na kuchukua uchungu na
maumivu moyoni.
Ikubalike tu kwamba unapoacha kujitaabisha kwa mawazo, hali ya
kuchanganyikiwa hutoka na hapo ndipo mwisho wa mateso na mwanzo wa
amani.
Kuna amani ipitayo ufahamu wa kibinadamu ambayo Mungu hutoa kwa wale
wote wanaokubali kumwachia nafasi.
Usijisumbue kwa jambo lililo nje ya uwezo wako kwani utashindwa
kufurahia maisha kwasababu ya kufikiri sana mambo usiyoweza kuyabadili.
Mfano, mambo madogo kama mvua itanyesha au jua litawaka, si juu yako
kujitaabisha nayo.
Simama imara, kusanya nguvu zako na kabiliana na changamoto zako. Acha
kujitesa kwa mawazo na ukubaliane na hali halisi unayoipitia.
Hakuna mafanikio pasipo maumivu. Mbali na maumivu unayokutana nayo
hutokea mabadiliko ambayo husababishwa na kuachwa na mke, familia au
watoto.
Watu huweza kubadilika kutokana na jinsi ulivyo, kwa kuwa hautakuwa kama
ulivyokuwa siku iliyopita.
Na kwa uwezo wa Mungu unaweza kubadilika na kuwa mtu mzuri zaidi kwa
siku zijazo.
Usijaribu kubadili tabia ya mtu mwingine. Kwa msaada wa Mungu,
atakusaidia kuibadili tabia yako.
Unaweza ukaibadili tabia yako, unaweza ukabadili ustaarabu wako, unaweza
ukabadili tabia mbaya ikawa nzuri, unaweza ukaibadili kazi yako,
unaweza ukabadili ndoa yako ingali mapema na waweza ukabadili moyo
uliovunjika.
Kila siku watu hubadilika, kwa msaada wa Mungu katikati ya watu wazuri
hufanywa imara kuliko hali ya kukatishwa tamaa uliyokuwa nayo.
No comments:
Post a Comment