Ili kuwa mtu wa mafanikio ni vema kutumia mbinu ya kufikiri kwa ubunifu kile unachotaka kukifanya.
Ni
vizuri kuwa na imani, unaweza kufanya jambo lako na likafanikiwa,
kwani unapoamini litafanikiwa, akili yako itazidi kutafuta njia ya
kulifanikisha zaidi.
Kuamini kuwa unaweza kufanya jambo kubwa,
kunafungua njia ya mafanikio. Kamwe usiseme ama kufikiri kuwa huwezi
kufanya jambo fulani katika maisha yako, badala yake, jaribu kufanya
kile unachofikiri kuwa huwezi.
Usiruhusu mambo ya mila na desturi ama utamaduni uliouzoea kutawala akili yako.
Kuwa mtu wa kupokea mambo na mawazo mapya kila wakati, kisha uyafanyie kazi.
Kila wakati jaribu njia mpya katika kufanikisha mambo yako, pamoja na kuwa mfuatiliaji wa shughuli zako unazozifanya.
Iulize
nafsi yako, inakupasa kufanya nini ili kuweza kufanya vizuri zaidi?
Wakati unajiuliza swali hilo, unakuwa tayari umeshapata jibu, cha
msingi ni kulifanyia kazi jibu hilo ulilolipata bila kuchelewa.
Pia
jiulize ni kwa vipi unaweza kufanya vizuri zaidi? Pia ni vema ukawa
na mazoea ya kusikiliza na kuuliza kwa wengine, kuhusu mambo unayotaka
kuyafanya kwani utapata mawazo mengi usiyoyajua kutoka kwa wengine.
Yapanue
mawazo yako, kwa kujichanganya na watu mbalimbali wakiwamo wenye
ujuzi wanaoweza kukupa mawazo na njia mpya za kufanya mambo.
Moja
ya kanuni ya mtu anayependa au mwenye mafanikio ni kuwa na muonekano
mzuri mbele ya jamii, kuanzia anavyozungumza hadi mavazi yake.
Unaweza
usikubaliane nami, lakini ukweli ni kuwa, kama wewe ni mfanyabiashara
wa nguo, jinsi unavyokuwa mtanashati mbele za watu, ndivyo
watakavyopenda kuja katika duka lako na kununua bidhaa zako hizo.
Lakini,
kama utakuwa haujijali kwa upande wa mavazi, halafu ukawa
mfanyabiashara wa bidhaa hiyo, utapata wateja wale wasiokujua na
wanaokujua wachache.
Utanashati unavutia biashara yako, si tu kwa
biashara ya nguo, bali hata katika shughuli zako nyingine
unazozifanya, uwe ni mwanasheria, mwalimu ama mpishi wa chakula, vile
unavyoonekana ndivyo unavyozidi kuimarisha biashara yako.
Kumbuka watu wanakutathmini kutokana na muonekana ulio nao.
Hebu tuangalie mfano huu kuwa, mtu anafanya biashara ya nyanya, anazipanga mafungu mafungu na kuziuza.
Mwingine
anafanya biashara hiyo hiyo, na kuziweka nyanya zile katika mfuko
wenye kuonyesha bidhaa iliyopo ndani yake na kufunga vizuri.
Biashara
hizo zikiwa katika eneo moja, watu wengi watanunua zile zilizofungwa
vizuri kwenye mfuko wakiamini kuwa ni salama zaidi.
Mfano huo ni sawa na muonekana ama utanashati wako kwa watu katika shughuli yoyote ile unayoifanya.
Uvaaji mzuri na wa heshima kwenye jamii, unakufanya uheshimike na kuaminika kuwa unaweza kufanya mambo makubwa unayoyapanga.
Ni vizuri kuboresha mawazo yako kila siku, kama watu maarufu wanavyokuwa.
Kuboresha mawazo, kufikiri na utendaji wako kutakuletea mafanikio katika mipango yako yote.
Hivyo ni vema, kula vizuri ili uweze kufikiri vizuri katika mambo unayoyafanya.
Endapo hautakula mlo kamili, akili yako haitakuwa na uwezo wa kufikiri vizuri, utabakia kuwa mtu wa kushindwa.
Kama
mtu anakula vizuri, anajilinda na magonjwa mbalimbali, mwili wake
unakuwa na afya pamoja na akili yake kuwaza mambo makubwa.
Akili yako huwezi kuilisha chakula unachokula, bali chakula chake ni mazingira yanayokuzunguka.
Mtu
yeyote anayetembea katika nchi ama mikoa mbalimbali, huwa na
mazingira ya tofauti, kila anapokwenda hujifunza kitu
kitakachomsaidia.
Mazingira ya eneo ulilopo yanaifanya akili yako
ifikiri zaidi ufanye kitu gani cha mafanikio katika eneo hilo ulilopo
kitachokupatia maendeleo.
Ukubwa wa jinsi unavyowaza, malengo yako, mazingira yako au vile unavyoonekana, ni kutokana na mazingira uliyopo.
Unapokuwa na watu wenye mawazo ya kuchelewa kufanikisha mambo, nawe utakuwa mtu wa kuchelewa kufikia malengo uliyojiwekea.
Kwa maana nyingine, kushirikiana na watu wenye mawazo makubwa kunakufanya uwaze mambo makubwa ya maendeleo.
Pia kukaa karibu na watu wenye malengo ama maono ya mafanikio, kunakufanya nawe uwe katika hali hiyo.
Katika jamii tunayoishi, kumekuwa na watu wenye tabia zilizogawanyika katika makundi matatu.
Kundi la kwanza, ni la watu wale ambao wameona kuwa hawawezi kufanya jambo likafanikiwa kabisa.
Wamekuwa na ujuzi na kukubali ujuzi huo katika eneo moja, yaani wameridhika na hali hiyo.
Kama,
Mungu amekupa ujuzi wako mzuri na ukabahatika kupata kazi sehemu
nzuri, pamoja na kufanya kazi ile, utumie ujuzi wako katika maeneo
mengine.
Unaweza kufungua ofisi yako na kuanzisha kitu chako mwenyewe huku ukiendelea na kazi yako.
Kamwe
usijikatishe tamaa kwa kuona kuwa huwezi kufanya hivyo, kudhani kuwa,
wewe umeumbwa kwa ajili ya kufanya kazi za wengine tu.
Kuna watu
wenye malengo makubwa na waliopanga kuyatimiza lakini kutokana na
ushindani uliopo hufika mahali na kushindwa kuendelea na mikakati
waliyojiwekea.
Tunaweza kusema, wamekata tamaa na kuacha kuyafanyia kazi malengo yao, mwishoni hupoteza mwelekeo kabisa.
Kundi
hili, wamejijengea tabia ya hofu, hofu ya kushindwa kutimiza malengo
yao, hofu ya ulinzi, hofu katika jamii inayomzunguka na kupoteza kila
wanalicho nacho.
Kundi la watu hawa, kamwe hawatafanikiwa kwani
wameshajiweka kwenye kundi la kushindwa ingawa lina watu wenye akili,
vipaji walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Kundi la tatu ni la watu wale ambao hawako tayari kukatishwa tamaa, hawa ni asilimia ndogo sana katika jamii.
Kundi
hili pamoja na kukatishwa tamaa, katika mipango yao, wamekuwa
wakijitahidi kufanya jitihada mbalimbali ili wajikwamue katika hali hiyo
waliyonayo na kuwa katika hatua nyingine.
Mara zote hupumua
mafanikio katika maisha yao. Kundi hili pia lina furaha kwa kuwa
limeshakamilisha baadhi ya malengo waliyojiwekea.
Wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali, lakini wamezishinda, wamekuwa wakiangalia siku mpya ikianza na jambo jipya.
Ni
ukweli usiopingika kuwa, kila mmoja wetu anapenda kuwa katika kundi
la tatu, ambalo kila mwaka wanapata mafanikio, wanaofanya mambo
mbalimbali na matokeo yake yanaonekana..
Makala
hii imeandaliwa kwa msaada wa kitabu cha 'The Magic of Thinking Big,’
kilichotungwa na David Schwartz pamoja na mitandao mbalimbali.
No comments:
Post a Comment