Washindi watatu wa mwezi uliopita wa shindano
la”Tweet” linalodhaminiwa na Mwenyekiti
Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, jana
walikabidhiwa zawadi zao.
Walioshinda ni Abnery Mwogela, Mwalimu kutoka
mkoani Iringa, Shilla Samson na Gerald Nyaissa,
mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma.
Wazo la wajasiliamali ambalo lilishindaniwa
mwezi uliopita lilikuwa linauliza “Mzazi afanye
nini kumwandaa mtoto kufanikiwa kiuchumi ”
huku mchakato wa kupata washindi hao
ukisimiwa na Kiongozi wa Taasisi ya Chuo cha
Uongozi na Ujasiliamali (IMED), Dk. Donath
Olomi.
Mshindi wa kwanza alijinyakulia Sh. milioni moja,
mshindi wa pili Sh. 500,000 na mshindi wa tatu
Sh. 300,000.
Wogela alijibu swali hilo kwamba mzazi
amuandae mwanae kuishi kwa kujiamini,
kudhubutu, kuanza kufanya anachodhani ni
vyema akifanye kwa wakati huo cha kiuchumi.
Mshindi wa pili alijibu kuwa Mzazi amwandae
mtoto katika mambo makuu manne, elimu,
kupenda kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na
kupenda kumcha Mungu.
Mshindi wa tatu alijibu kuwa kila siku mzazi
mnong`oneze mwanao; “Mungu amewapa matajiri
saa 24 kwa siku sawa na anayokupa wewe,
yatumie saa hizo kwa faida”.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi,
Dk. Mengi, alisema suala la mzazi kumlea mtoto
namna ya kujitegemea kiuchumi ni jambo la
msingi.
Alisema kama methali inavyosema kuwa mtoto
umleavyo ndivyo akuavyo, vivyo hivyo ndivyo
inavyokuwa kwamba malezi ya mzazi yanaweza
kumsaidia mtoto akabarikiwa katika maisha yake
na yakampa msukumo wa kujiendeleza au
yakamkatisha tamaa.
Dk. Mengi aliongeza kuwa suala jinginge ambalo
mzazi anatakiwa kutambua katika kumlea mtoto
ni pamoja na kumfundisha kumtanguliza Mungu
mbele katika shughuli zote anazofanya kwa kuwa
pia itamsaidia kuwa mwema.
Aidha, aliwataka vijana kufungua macho
kuangalia fursa mbalimbali ili waweze kuzitumia
na kuondokana na tatizo la kukosa ajira
linalowakabili vijana wengi.
Alisema zipo fursa nyingi ambazo endapo vijana
watazitumia pasipo kuchagua kiwango cha elimu
walichonacho, wataondokana na tatizo la ajira.
“Sisemi kwamba tatizo la ajira halipo, wala
sisemi watu wasilalamikie tatizo la ajira, lakini pia
tunatakiwa kufungua macho kuangalia fursa za
ajira zilizopo, fursa za ajira zipo nyingi ila
kinachotakiwa ni vijana kufungua macho na
kuangalia, ninaamini kwamba vijana wa
kitanzania wakijiamini wakatumia fursa zilizopo
wataondokana na tatizo hilo,” alisema.
Mwisho wa mzunguko wa shindano hilo
lililozinduliwa Mei 13, mwaka jana ni mwezi huu,
na katika miezi mitatau ijayo watakaa na
kuchambua mawazo yaliyoshindanishwa kwa
kipindi chote ili kuyafanyia kazi kwa vitendo
pasipo kuishia katika kushinda pekee.
CHANZO: NIPASHE

Categories:

Leave a Reply