MTU yeyote aliyevunjika moyo au kukata tamaa kutokana na mambo magumu yaliyompata, iwe ni kuyumba kiuchumi, kufiwa na ampendaye, kukimbiwa na watoto, maradhi yasiyotibika au kuachwa na mume au mke, huwa anapata maumivu makali yanayokata kama kisu ndani na hata kuathiri hisia, fikra pamoja na maamuzi anayoweza kuyafanya. Maisha yaliyojaa utoshelevu na mafanikio na uwezo wa kupata kila kitu cha muhimu unachokihitaji, ikiwa ni pamoja na ndoto zako nyingi kutimizwa, yaweza kubadilika kabisa na kuwa kinyume cha hapo kiasi cha kufanya mtu ahisi hana sababu tena ya kuishi iwapo sababu au vigezo vyote vilivyokuwa vikikupa utoshelevu na furaha vimetoweka! Watu uliowazoea na kushirikiana nao wanaweza kukutenga au kukushusha hadhi mara wagunduapo kuwa meli yako yakaribia kuzama, iwe ni kiuchumi, kijamii au kiafya. Inaaminika kuwa haijalishi ni sababu gani kubwa iliyomfanya mtu kukata tamaa ya maisha, kuvunjika moyo, au kuwa na msongo wa mawazo. Njia inayotumika ili kuponya na kurejesha katika uzima na ubora wa maisha ni ile ile kwa kila mtu. Mungu hafurahishwi na kushindwa kwetu, naye huumia pamoja nao wanaoumia lakini yupo tayari kuponya vidonda vyote vilivyoshindikana kupona ili kufanya upya tena. Madaktari husema mfupa uliovunjika ukiunga unakuwa na nguvu zaidi pale palipokuwa pamevunjika kuliko sehemu nyingine za huo mfupa. Ndivyo ilivyo hata kwa mtu aliyekata tamaa na kuvunjika moyo anapokubali kuchukua hatua za kupambana na hali yake hiyo, mwisho wa siku aweza kuwa mwenye nguvu na bora kuliko alivyokuwa hapo awali. Hebu tuangalie kanuni za kukabiliana na hali ya kukata tamaa. Kwanza yatakiwa ukubaliane na zile hali ambazo huwezi kuzibadili tena. Kumbuka yapo mambo katika maisha yako, hata ungejaribu kwa jitihada kubwa sana kuyabadili usingaliweza. Mfano: Huwezi kubadili hali ya hewa, huwezi kubadili majira au mzunguko wa saa, huwezi kubadili yaliyokwisha kupita, Huwezi kubadili ukweli kwamba umpendaye kakutoka na mambo mengine yafananayo na hayo. Wakati mwingine waweza kulazimika kukubaliana na majibu ya kukatisha tamaa ya daktari yanayoashiria mwisho wa maisha au ugonjwa usio na tiba lakini bado ukiwa na amani moyoni na kumuachia Mungu aamue, waweza kukubaliana na matokeo. Ufunguo wa amani moyoni ni pale unapokubali kuwa huwezi kubadili matatizo mengine bali waweza kuacha mikononi mwa Muumba ambaye ni mkuu kupita wote. Muombe Mungu akujalie neema kukubaliana na vile usivyoweza kuvibadili pia akujalie nguvu kubadili vile unavyoweza na hekima ya kujua utofauti. Yakupasa kusimama ili kukabiliana na changamoto yako mwenyewe. Kamwe usikimbie matatizo! Hakuna mtu yeyote anayependa kuaibika, kuaibishwa au udhaifu wake kuanikwa hadharani kwa kila mtu kuuona, zaidi sana inapokuwa kwamba yeye ni mtu mwenye heshima au dhamana katika jamii yake aliyopo. Mfano: Wakati mwingine tunajitwika lawama tusizostahili ili tu kuhalalisha au kubadili mwonekano halisi uwe tofauti. Tupo tayari kuingia gharama iwayo yoyote kuzuia au hata kuahirisha matukio ya uchungu maishani, lakini mara nyingi hizi huwa ni mbio za sakafuni ambazo huishia ukingoni. Kamwe usikimbie changamoto zinazokukabili kimaisha. Simama kidete kubaliana na ukweli halisi ya kwamba mambo mengine huwezi kuyabadili bali kuyakubali. Mtu huheshimika kwa jinsi awezavyo kukabiliana na changamoto zake mwenyewe za maisha. Fahamu kuwa huwezi kubadili mitazamo ya watu wengine juu yako. Waweza kubadili mtazamo wako mwenyewe na matendo yako, na hapo ndipo watu wanaokuzunguka watakapobadili mitazamo yao juu yako kutokana na badiliko lako. Mfano: Iwapo unataka jamii ikuchukulie kama mtu anaye jiheshimu, mkarimu au mwenye kujithamini ni lazima na wewe mwenyewe uishi kama unavyotaka watu hao wakuchukulie. Huwezi kutegemea kuheshimiwa na watu iwapo wewe mwenyewe haujiheshimu au hauthamini utu wako. Watu wengi hupenda kuheshimiwa au kusifiwa hata kwa mambo ambayo hawastahili au hawajayafanya; kwa kisingizio cha cheo au dhamana katika jamii husika. Lakini mwisho wa siku ukweli unapokuja kudhihirika, unakuwa umeshusha kabisa hadhi na dhamana yake katika jamii. Hivyo uponyaji wa kihisia unaanza pale unapochukua hatua kubwa ya kwanza ya kukubaliana na hali halisi juu ya vile vitu ambavyo huwezi kubadilisha. Kukubali inamaanisha kuacha kuzuia yasiyozuilika. Mfano, huwezi kumlazimisha mtu kufanya asiyotaka kufanya. Huwezi kubadili kifo au ugonjwa nk. Kukubali huondoa maumivu mengi yaliyojificha na kuchukua uchungu na maumivu moyoni. Ikubalike tu kwamba unapoacha kujitaabisha kwa mawazo, hali ya kuchanganyikiwa hutoka na hapo ndipo mwisho wa mateso na mwanzo wa amani. Kuna amani ipitayo ufahamu wa kibinadamu ambayo Mungu hutoa kwa wale wote wanaokubali kumwachia nafasi. Usijisumbue kwa jambo lililo nje ya uwezo wako kwani utashindwa kufurahia maisha kwasababu ya kufikiri sana mambo usiyoweza kuyabadili. Mfano, mambo madogo kama mvua itanyesha au jua litawaka, si juu yako kujitaabisha nayo. Simama imara, kusanya nguvu zako na kabiliana na changamoto zako. Acha kujitesa kwa mawazo na ukubaliane na hali halisi unayoipitia. Hakuna mafanikio pasipo maumivu. Mbali na maumivu unayokutana nayo hutokea mabadiliko ambayo husababishwa na kuachwa na mke, familia au watoto. Watu huweza kubadilika kutokana na jinsi ulivyo, kwa kuwa hautakuwa kama ulivyokuwa siku iliyopita. Na kwa uwezo wa Mungu unaweza kubadilika na kuwa mtu mzuri zaidi kwa siku zijazo. Usijaribu kubadili tabia ya mtu mwingine. Kwa msaada wa Mungu, atakusaidia kuibadili tabia yako. Unaweza ukaibadili tabia yako, unaweza ukabadili ustaarabu wako, unaweza ukabadili tabia mbaya ikawa nzuri, unaweza ukaibadili kazi yako, unaweza ukabadili ndoa yako ingali mapema na waweza ukabadili moyo uliovunjika. Kila siku watu hubadilika, kwa msaada wa Mungu katikati ya watu wazuri hufanywa imara kuliko hali ya kukatishwa tamaa uliyokuwa nayo.

Categories:

Leave a Reply