Tunaishi katika dunia iliyojaa uhalifu. Uhalifu wa aina mbalimbali kuanzia wizi wa kutumia silaha, wizi wa maarifa yaani utapeli na hata wizi wa kutumia kemikali na teknolojia. Hali ya uhalifu inazidi kuongezeka kutokana na sababu kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na hali ngumu ya uchumi na kukua kwa utofauti wa kipato kati ya masikini na matajiri. Kama inavvyofahamika, idadi kubwa ya watanzania hawana ajira wala mbinu za kujitafutia kipato kihalali hivyo kujikuta wakishawishika kuingia katika uvunjaji wa sheria ikiwa ni pamoja na wizi na ujambazi. Moja kati ya mambo muhimu sana katika maisha lakini yaliyosahaulika ni elimu juu ya tahadhari ya uhalifu. Pamoja na jitihada za vyombo vya dola na usalama katika kuimalisha ulinzi, ni jukumu la kila mmoja wetu kufahamu mbinu mbalimbali za kuzuia, kujikinga au kupunguza uwezekano wa uhalifu ikiwa ni pamoja na kupigwa, kutekwa nyara, kuvamiwa, kuporwa au kuibiwa kwa namna mbalimbali. Hizi ni moja ya mbinu unazoweza kutumia katika kujidhatiti na majanga niliyoyataja hapo juu;
• Mara nyingi uhalifu hupangwa na watu wanaokufahamu vizuri, hivyo usiwe mwepesi wa kumuamini mtu na kumpatia siri zako za karibu mfano kazi yako, mzunguko wa pesa, ratiba zako nk.
• Jitahidi kufanya mazoezi ya viungo au ulinzi binafsi ikiwa ni pamoja na kukimbia ili uwe na uwezo wa kukimbia au kutoweka unapobanwa katika mazingira hatarishi ya uhalifu
• Mahali unapoishi hakikisha unafahamiana vizuri na majirani. Mara nyingi majirani wanaweza kukupatia taarifa muhimu kuhusu watu au kundi la watu linaloshukiwa kuzuru au kuzurura maeneo ya makazi yako hasa nyakati ambazo haupo nyumbani
• Hakikisha una taarifa za kutosha za watu ambao unamahusianio nao ya karibu ikiwa ni pamoja na wasaidizi wa nyumbani. Kabla ya kuajiri, hakikisha unatafiti historia zao, wapi wanaishi, familia zao na hata historia zao za uhalifu
• Iwapo unaweza kumudu gharama ni vizuri ukawa na ulinzi binafsi hasa maeneo ya nyumbani. Ulinzi binafsi unaweza ukawa wa mlinzi wa kuajiriwa au vifaa maalum vya kuzuia uhalifu
• Uwapo nyumbani hakikisha una namba za simu za majirani, silaha, filimbi na namba za simu za kituo cha polisi kilicho karibu
• Ukiweza usizime simu yako hasa nyakati za usiku. Inaweza ikakusaidia kupokea au kupata taarifa za uhalifu
• Hakikisha unafunga milango yote kabla ya kulala. Usiwaachie wasaidizi wa nyumbani kazi hiyo mara nyingi husahau kufunga milango
• Ukisafiri na gari nyakati za usiku fuatilia nyendo za magari ya nyuma. Ukishuku gari au pikipiki au watu wowote wanaofuatilia nyendo zako, usiwahi kukimbilia ndani bali jaribu kupoteza ramani ya mwelekeo wako uone iwapo watazidi kukufuatilia. Iwapo utazidi kushuku mienendo yao badili njia na ikiwezekana nenda moja kwa moja kituo cha polisi
• Magari yaliyo na vioo vyeusi sana sio mazuri kwa usalama kwani lolote linalotokea ndani haliweza kuonekana kwa nje. Iwapo utatekwa ndani ya gari yenye kiza, hakuna atakayegundua kuwa uko katika hali ya shida
• Hakikisha unawasiliana na watu wa nyumbani kabla ya kufika nyumbani ili utaratibu wa kufungua geti uweze kuandaliwa mapema hasa nyakati za usiku
• Ukitembea kwa miguu barabarani usitembee upande mmoja kwa muda mrefu ukiweza ama pande ili kubaini yeyote ambaye anafuatilia nyendo zako iwe ni mwizi, kibaka au jambazi • Ukijenga au kuishi katika nyumba, bainisha ni maeneo gani utatumia kukimbia au kujificha nyakati za hatari. Inaweza ikawa ni juu ya dari au chini kwenye handaki
• Usisimame kutoa lifti kirahisi hata kwa mtu unayemfahamu. Maranyingi wahalifu hutumia mbinu mbalimbali kuingia katika himaya yako
• Usiamini mtu kwa kuzungumza nao kwenye simu. Na iwapo mtu anakupigia simu mkutane mahali fulani, ukawa na wasiwasi naye, jaribu kubadilisha sehemu ya kukutana ili kutibua mipango yoyote anayoweza kuisuka
• Usiamini sana kuongea mambo yako ya siri kwa kutumia teknolojia. Wahalifu wanao uwezo wa kudaka mawasiliano yako yote kupitia simu za mikononi au kompyuta na kuitumia kukumaliza • Usishikane mikono na mtu usiyemfahamu barabarani. Wahalifu wana silaha maalum za kukupa madawa ya kukulevya na kukufanyia uhalifu
• Usionane hovyo na wote usiowafahamu. Tengeneza utaratibu wa kukutana na watu kwa miadi maalum. Ukiwa katika nafasi kubwa ya uongozi au biashara, wachunguze watu unaotaka kukutana nao kabla ya siku ya miadi ikiwezekana tuma watu wako wa ulinzi kwa uchunguzi pasipo wao kujua
• Usile chakula usichokifahamu vizuri, unaweza kuwekewa madawa na kufanyiwa uhalifu • Mahusiano ya kimapenzi yanaweza kutumika katika uhalifu. Ni vizuri kuwa makini na mienendo ya kimahusiano
• Usipende kuendesha gari wakati umefungua vioo hasa nyakati za usiku
• Usiendekeze ugomvi hasa barabarani, wahalifu hupenda kuanzisha ugomzi kujenga mazingira ya uhalifu
• Wafundishe watu unaoishi nao namna ya kuwahudumia wageni, sio kila mgeni anaruhusiwa kuingia ndani ya nyumba
• Utaratibu wa ulinzi shirikishi ni muhimu kwa ulinzi hasa sehemu za makazi
• Utulivu ni moja ya silaha kubwa wakati wa hatari
• Usikae na kiasi kikubwa cha pesa nyumbani au sehemu ya kazi
• Usimzoeshe mtu yeyote kujua kwamba unatabia ya kukaa na pesa nyumbani au kazini
• Usiache watu wakafahamu mzunguko wako wa kipesa ikiwa ni pamoja na lini unaenda benki, benki gani na namna yako ya kubeba pesa
• Sio vizuri kufanya malipo ya fedha taslim hasa sehemu za kazi
• Ukisimamishwa na watu au kundi la watu barabarani usiku, usiwe mwepesi kusimama hata kama wamevalia sare za polisi au mgambo
• Epuka kusafiri nyakati za usiku
• Usimdhurumu mtu au kujenga chuki na uadui na watu. Mara nyingine uhalifu hufanywa kulipiza kisasi
• Usipende kutoa taarizafa za mtu ikiwa ni pamoja na namba zake za simu pasipo yeye mwenyewe kuridhia. Huwezi kujua anayemtafuta ana mpango upi
• Usiwaamini sana hata walinzi wako wenyewe
• Ukiwa kiongozi, tengeneza mazingira ya kila mtu kuwa mlinzi wa mwenzake
• Ukifanyika uhalifu sehemu hasa wizi, hakikisha unazuia mawasilisano hasa simu za mikononi kuepuka kuvuja kwa taarifa za uchunguzi
• Ni vizuri kulala ukiwa unajitambua na si kulala fofofo kwa uchovu au ulevi ili kugundua hali yeyote isiyo ya kawaida inayotokea nyakati za usiku
• Usipende kufungua mlango au kugeuka kwa sababu tu mtu amekuita jina lako
• Jenga utamaduni wa kukutana na watu maeneo ya wazi na si sehemu zilizojificha • Usipende kuongea mambo mengi hasa na watu usiowafahamu vizuri
• Usichoke kusali kwa ajili ya ulinzi wa Mungu

Categories:

Leave a Reply