UMEKUWA ukiruhusu mawazo yako kuwa kizuizi cha mafanikio yako? Kwa kuwa
na mawazo hasi, mawazo ya umaskini, ukabila, wasiwasi au woga? Kama
ndivyo, badilika. Chukua muda kila siku kufikiria, kuchuja na umakini
katika mipango yako unayoipanga. Utaona kuwa fikra zako zina nguvu
pamoja na kukua. Kila unapoendelea kufikiria, ndipo mipango yako
inapoimarika. Baadaye, utafanikiwa na kuwa mtu mwenye maendeleo.
Kumbuka
mawazo ndiyo mwanzo wa mafanikio yako. Unapokuwa na ndoto ya mafanikio
kwanza yakupasa kuwa na wazo lako ambalo baadaye unatakiwa kulifanyia
kazi, ili utengeneze bahati yako. Kwa kufuata maelekezo hayo utakuza
upeo wako.
Ota ndoto kubwa. Wengi wanaweza kukupotosha kutokana na
utajiri wa malighafi ulionao na kukudanganya kwa njia nyingi, lakini
hakuna mtu anayeweza kukupotosha katika msimamo na kutumia fikra zako.
Wengi
wanaweza wasikutendee haki, kama wengi wafanyavyo, wanaweza kukupotosha
katika uhuru ulionao, lakini hawawezi kukuchukulia mawazo unayoyawaza.
Kutokana na fikra zako utakuwa unashinda siku zote. Unataka kuwa na
furaha? Unataka kuwa na amani? Unataka kuwa na cheo, nguvu au utajiri?
Fikiri kuwa navyo, utafanikiwa.
Fikra unazowaza ni muhimu kuliko
ujuzi ulionao. Ujuzi una mipaka, mawazo yanatawala muda wote, yanaleta
maendeleo. Kila mtu binafsi anakuwa na ndoto za mafanikio bila
kujitambua. Kwa mfano, wazazi wanapopanga ni jinsi gani watawaendeleza
watoto wao, wajasiriamali wanapopanga ni jinsi gani wataendeleza
biashara zao hiyo yote ni mifano ya kuwa na ndoto njema ya mafanikio.
Watu
wachache wamejifunza kutumia mawazo yao kwa faida lakini wengi wetu
mawazo tuliyonayo yanapata kutu kutokana na kutoyafanyia kazi. Hakuna
sababu ya kuona aibu katika dunia ya ubunifu.
Kuwa na mawazo ya
kufanya jambo fulani ni kitu kizuri katika dunia hii tunayoishi. Kila
mmoja wetu ana kiwanda chake cha kuwa na mawazo. Lakini ni wapi mawazo
hayo yanapotoka? Ni wapi waandishi, wana sayansi na wabunifu wanapopata
mawazo makubwa? Kwa nini baadhi ya watu wengine wanakuwa wabunifu zaidi
ya wengine? Ni kutokana na kutumia vizuri mawazo yao.
Kila mmoja
wetu, kwa wakati mmoja au mwingine, lazima kujifunza chanzo halisi cha
mawazo. Utajiri, unaweza kuupata, inategemeana na ulivyoyaweka mawazo
yako. Wazo dogo rahisi linaweza likabadilisha kabisa maisha yako
uliyonayo. Pia huwezi ukajua ukubwa wa mafanikio yako mpaka
utakapojifunza jinsi ya kuchanganya juhudi zako na mawazo yako. Kwa
vyovyote unapotaka mafanikio unajitathmini wewe mwenyewe.
Mwili
uliopumzika una nguvu, vile vile akili. Kama unataka kuwa mbunifu na
mpokeaji wa mawazo mapya, inakubidi kupata muda kwa mawazo hayo na
kuyafanyia kazi.
Jizoeze kila siku kuwa na muda wa mapumziko, chagua
chumba kizuri kilichotulia au kiti kizuri ambacho kitakusaidia kutuliza
akili kwa urahisi. Unavyoendelea kujifunza kupumzika, utapata mawazo
ambayo yatakufikisha katika malengo na matarajio yako.
Mtunzi
anafikiri juu ya uimbaji, mchoraji anafikiri juu ya rangi, mwandishi
anafikiri juu ya habari na maneno. Kama utachukua wazo moja na
kulitendea kazi litakupa matokeo mazuri. Yafanyie kazi mawazo
yanayokujia. Kuwa na utayari katika kunasa mawazo yako. Mawazo mengi
mazuri yanapotea kwa sababu hayawekwi kwa maandishi.
Tathmini mawazo
yako. Mara tu unapomaliza kuyachuja mawazo yako, unachagua yale
unayotaka kuyafanyia kazi. Utagundua kuwa nayo yanahitaji kuongezewa
ubora wake. Jifunze kutokufunga milango yako ya kuwa mbunifu.
Ni
jambo lisilowezekana kati yetu kuwa kinyume na ujuzi tulionao. Mfano mtu
hawezi kupita mbele ya gari liendalo kasi kwa kuwa anajua kuwa ataumia,
hawezi kuogelea baharini kama anajua kuwa atazama, hawezi kuwa mstari
wa mbele katika jambo la hatari kama anajua kuwa atadhurika.
Mafanikio
hayahitaji kuwa na kiasi kikubwa cha ujuzi juu ya jambo fulani, lakini
unatakiwa kung’ang’ania ili uweze kupata mafanikio hayo kwa ujuzi wowote
ulionao.
Mkulima mmoja aliyejulikana kwa jina la Walter na ambaye
siku za usoni angependa kuwa mchezaji bora wa mpira wa miguu, alimuuliza
rafiki yake kuwa amewezaje kupata sh milioni 10 katika kazi yake
anayoifanya kutokana na ujuzi alionao na kuweza kushinda kila dhana ya
kushindwa ambayo ilikuwa inaibuka katika utendaji wake?
Rafiki huyo
alimjibu kuwa wakati anaanza, alijua anataka kufanya nini na
anachotarajia kukipata. Alikuwa na njozi iliyomwezesha kujenga picha
katika mawazo yake kulingana na malengo aliyotaka kuyafikia katika
maisha yake. Hivyo hiyo ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika maisha
yake.
Walter alisema kuwa kuna wakati alisikia umati wa watu
ukishangilia katika mawazo yake. Kuna wakati alijenga picha ya sherehe
ya kupewa tuzo iliyojaa waandishi wa habari za michezo, wageni na
wanamitindo mbalimbali. Ndoto hiyo sasa ameanza kuifanyia kazi, hivyo
anaamini atafanikiwa kama rafiki yake huyo alivyofanikiwa.
Inaonyesha
watu wengi wamekuwa hawako tayari kutulia na kufanyia kazi ndoto zile
wanazokuwa nazo, kwa kuzipa nafasi ndogo katika utekelezaji wake.
Kuna
mamilioni ya watu ambao wanaamini wanaangamia kwa umaskini na kushindwa
kwa sababu baadhi ya malengo waliyonayo wamekuwa hawawezi kuyafanyia
kazi. Bila kujua watu wengi hujitengenezea mazingira mabaya kutokana na
mawazo hasi ambayo yanachukuliwa na mawazo na kutafsiriwa kwenda katika
vitendo.
Kama mwanamume au mwanamke ambaye amejenga katika mawazo
yake utajiri na mafanikio na akafikia mafanikio hayo, ni hivyo pia kwa
Wamarekani weusi ambao waliikabili meza ya kushindwa kwa maisha kwa
sababu mawazo yao yalikuwa yamejenga picha ya umaskini, bahati mbaya na
kushindwa. Lakini kwa sasa Wamarekani weusi hao wamepata mafanikio.
Kwa
sasa hivi utaweza kutambua kwamba mawazo ni vitu ambavyo vikifanyiwa
kazi vizuri na kutekelezwa vinaweza kuwekwa katika mfumo wa uhalisia.
Kama utakuwa na njozi za kupata zaidi na ukazijengea picha hiyo bila
kujali utakumbana na vikwazo gain, hiyo itakuwa ni vipaumbele katika
maisha yako.
Kama utaruhusu picha ya namna hii kuwa ya kudumu katika
ulimwengu wako wa mawazo; utafikiri mawazo ya mafanikio na kuzungukwa na
watu wenye mafanikio watakaotia moyo njozi zako.
Utatenga sehemu ya
kipato chako kwa ajili ya kujilipa wewe mwenyewe, moja ya hatua muhimu
katika kupata utajiri. Utajihusisha katika mpango ambao unaleta
mafanikio binafsi na kukufanya uchague lengo la maisha yako.
Pia
utatafuta ujuzi na utaalamu kwa wale wote ambao wamefanikiwa. Mwishoni
utafanikiwa licha ya kukumbana na vikwazo katika kutekeleza njozi zako.
Categories: