ILI ufanikiwe unatakiwa kutumia uwezo na nguvu
ambazo tayari unazo. Inakubidi kuwa mshindani, kukubali kuwa unaweza na kufanya bidii zaidi.
Pia yakupasa uwe na utayari wa kutaka kuwa na mafanikio katika maisha yako. Pasipokuwa na utayari hutafanya chochote.
Vyoyote vile utakavyofikiri kuwa tajiri katika akili yako utafanikiwa.
Tuangalie mfano wa kweli uliomtokea mkulima mmoja maskini aliyekuwa anaishi katika Bara la Afrika, ambaye alikuwa na shamba kubwa la dhahabu bila yeye kujua. Mkulima huyo alitumia muda na miaka mingi akijitahidi kupanda mazao katika shamba lake ambalo lilikuwa gumu kulilima na lenye miamba.
Kutokana na ugumu aliokuwa anakabiliana nao, mkulima huyo alipumbazwa na utajiri wa haraka haraka ambao angeupata kutoka kwa mtu mmoja ambaye alikuwa anatafuta madini ya dhahabu katika maeneo mbalimbali kwa kufanya utafiti. Kwani naye mtu huyo alikuwa anataka kuwa tajiri.
Mkulima yule kwa kuwa alichoka kulima, aliamua kuuza shamba lake kwa mtu yule aliyekuwa anatafuta madini ya dhahabu. Alipata pesa akawa na maisha mazuri kwa muda, mwishoni alikata tamaa, aliishiwa fedha, alivunjika moyo na kupata hisia za kujirusha mtoni ambapo alizama na kufariki dunia.
Wakati huo, mtu yule aliyenunua shamba la mkulima wakati akifanya utafiti wake alikuta jiwe lisilo la kawaida katika mto uliopita katika shamba lake.
Alilipima na kukuta ni jiwe kubwa la dhahabu lenye thamani. Hivyo tangu wakati huo mtu huyo alikuwa ni mojawapo kati ya matajiri wakubwa duniani.
Yakupasa katika maisha yako ya kila siku kutokuchukua maamuzi ambayo baadaye yataleta hasara katika maisha yako au familia yako kwa ujumla.
Unapokuwa na kitu kabla hujachukua hatua yoyote ya kukiuza au kubadili uamuzi wako wa awali juu ya kitu hicho ni vizuri kuomba ushauri kwa watu unaowaamini na kuwategemea.
Si wote watakaokushauri vizuri, ni juu yako wewe kuweza kupima ni ushauri gani ambao unaweza ukakufaa kutokana na mwelekeo wa jambo lako.
Tukirudi katika mfano wetu tunaona kwamba, mkulima wa kwanza hakujua kuwa alikuwa anamiliki shamba kubwa lenye madini ya dhahabu.
Kama angeomba ushauri au angepoteza muda wake kufanya utafiti katika shamba lake, naye angekuwa ni mmoja kati ya matajiri waliopo.
Alilima, alichoka akaamua kuuza mali yake kwa ajili ya kutafuta bahati yake katika shughuli nyingine bila kugundua kuwa shamba alilokuwa nalo ndio utajiri wake.
Angejaribu kuchunguza kwa nini hilo shamba lake lina miamba mingi na anaweza kunufaikaje nalo, asingefikia hatua ya kujirusha mtoni na hatimaye kufariki dunia.
Mfano huu unamhusu kila mmoja wetu ambaye anafananishwa kuwa na shamba lenye madini ya dhahabu. Kwa maneno mengine kila mtu katika kazi yake anayoifanya iwe ni kilimo, biashara, uvuvi nk, kama atatulia na kuifanyia tathmini kazi yake na kuamua kupiga hatua zaidi lazima atafanikiwa.
Usiwe mwepesi wa kuachilia mambo kutokana na ugumu wake na kufikia hatua ya kukata tamaa, kuvunjika moyo na hata wengine kuchukua uamuzi wa kujiua. Kama kila mtu atatulia na kufanya utafiti katika shughuli yake anayoifanya atagundua kuwa ana utajiri mwingi, haijalishi kama ni utajiri wa malighafi, roho au vyote.
Kabla hatujaanza kukimbia huku na kule kufikiria kutafuta shamba lenye majani mabichi, tuhakikishe kuwa mashamba tuliyonayo tunayatumia vizuri. Mara nyingi, tunapoendelea kuangalia mashamba mengine, watu wengine nao wanaangalia mashamba yetu.
Kumbuka maandalizi yanakufanya kumaanisha jambo lolote unalotaka kulifanya, kwa kuwa utakuwa umelifanyia tathmini.
Mtafiti mmoja aliwauliza watu 3,000 kila mmoja peke yake kuwa wanaishi ili iweje? Mtafiti huyo alipatwa na mshtuko alipogundua kuwa asilimia 94 ya watu wote walioulizwa hawakuwa na sababu za msingi. Hao walikuwa ni wanawake na wanaume ambao wamekuwa wakipata taabu na kuendelea kuvumilia wakati wanasubiri siku nyingine mpya ianze katika maisha yao.
Mtafiti huyo aligundua kuwa watu hao walikuwa wakisubiri jambo fulani liweze kutokea ili maisha yao yabadilike, walikuwa wakisubiri siku ya kesho, wakisubiri mwaka ujao, wakisubiri watoto wao wakue na waondoke nyumbani pia fulani afariki ndipo waanze kuchukua hatua ya kufanya jambo kubwa la kubadilisha maisha yao.
Hii haileti maana wakati unapozungumzia kumwondoa mtu katika hali aliyonayo na kuwa katika hali bora zaidi.
Kumbuka jana imepita, na kesho hujui kama utakuwepo. Mtu yeyote ambaye hana malengo anaishi maisha ya kubahatisha. Ni vizuri kufahamu sheria ambazo zinaweza kukuongoza katika maisha yako ya kila siku. Dunia ni yako kama utaijua siri ya mafanikio.
Wakati mwingine vitu tulivyonavyo kama nyumba, gari au vinginevyo vinaweza kuharibika kabisa lakini upo uwezekano wa kupata vingine kama utakuwa na malengo ya kuwa na mafanikio zaidi ya hapo ulipokuwa. Jambo la msingi usikate tamaa.
Mtu yeyote anaweza akapitia kipindi kigumu cha kuishiwa na kufilisika kabisa, lakini inawezekana kupata bahati nyingine ya kutajirika. Hali hiyo inaweza kutokea mara kwa mara lakini cha msingi fanya bidii bila kukata tama, ukijua kuwa unapambana na maisha.
Hata kama umepata janga la kuunguliwa na nyumba yako, upo uwezekano wa kuijenga tena.
Kwa hiyo tumepata bahati kwa kuwa na nguvu isiyozuilika ya kufanya jambo kila unaponuia kufanya hivyo.
Maisha ya utajiri yanamzunguka kila mmoja wetu, inatakiwa upokee maisha hayo kwa moyo wa ukunjufu.
Fikiri kwa muda. Kufikiri ni zawadi kubwa ambayo inakupa matarajio kwa mambo yako yajayo ambayo umeyapanga.
Gari unaloliendesha, nyumba unayoishi, kiti unachopumzikia, vyote hivyo ulivipata baada ya kufikiri.
Ni kwa nini watu wengi wanaendelea kushindwa katika maisha yao? Ni kwa sababu watu wengi hawajui kanuni mbalimbali za maisha wanayoyaishi. Kwa kushindwa kuelekeza fikra zao katika mambo wanayoyatarajia.
Umekuwa ukiruhusu mawazo yako kuwa kizuizi cha mafanikio yako? Kwa kuwa na mawazo hasi, mawazo ya umaskini, ukabila, wasiwasi au uwoga? Kama ndivyo, badilika. Chukua muda kila siku kufikiria, kuchuja na umakini katika mipango yako unayoipanga.
Utaona kuwa fikra zako zina nguvu pamoja na kukua. Kila unapoendelea kufikiria, ndipo mipango yako inapoimarika. Baadaye, utafanikiwa na kuwa mtu mwenye maendeleo.
tukutane kwenye mueendelezo wa mada hii unaweza kutuandikia au kuacha comment kwenye blog hii na uka share na wenzako
Categories:

Categories:

Leave a Reply