Maadili ya kazi:

Tofauti kubwa kati ya maadili ya biashara, ujasiriamali, kazi za kuajiriwa au vitu vingine vyovyote kama vile matumizi ya barabara, familia n.k. ni katika maadili.  
 Asilimia kubwa ya watu walioko katika kazi zao za kitaaluma (professionals) au zisizo za kitaaluma (unprofessionals) hawafuati maadili ya kazi (Work Ethics),  matokeo yake siku zote watanzania tumekuwa tukilia maendeleo hatuyaoni, au maendeleo yanachelewa wakati chanzo cha kwanza cha tatizo nisisi.
Labda nikuulize, Je hujawahi kuona?
 • Mfanyakazi anatumia muda mrefu kusoma gazeti ofisini?
 • Story na soga zikitawala ofisini?
 • Wafanyakazi wakienda kula kwa zaidi ya lisaa (yaani wanatoka eneo la kazi kabla ya muda wa kwenda kula na kurudi baada ya muda wa kawaida wa kutoka kula).
 • Mfanyakazi akiwapa kipaumbele  wale anaowajua au waliomuwezesha kuwa au kufikia namna   fulani?
 • Wafanyakazi wakichelewa kufika kazini na kuwahi kutoka eneo la kazi kabla ya muda wa kawaida.
 • Wafanyakazi wakianza wikiendi mapema na kuchelewa kuimaliza wikiendi hiyo (athari za yaliyoendelea wikiendi yanaathiri hata utendaji wa muda wa kazi mwanzo wa wiki.
 • Muuza duka akikaa nje ya duka akipiga soga au kusoma gazeti  na mteja anapokuja muuza duka huyu anamuuliza mteja kitu anachotaka akiwa nje ya duka pasipo hata kuingia ndani ya duka palipo eneo lake la kazi (maranyingine nawaza labda anatamani hata kitu hicho kisiwepo dukani ili asisumbuliwe kukatisha anachofanya na kuingia ndani ya duka).

Tunamaanisha nini katika suala zima la maadili ya kazi?
-          Jinsi nzima ya kiutendaji
-          Mahusiano yetu na wafanyakazi, wafanyabiashara wenzetu, wajasiriamali wenzetu, na mahusiano yetu na wateja au wapokea huduma
-          Mjumuisho wa sheria na misingi ya kiutendaji inayokubalika katika eneo la kazi.

Baadhi ya Maadili hayo.
-          Kuweka mazingira ya kazi safi na salama kwa ajili yako wewe mwenyewe na wafanyakazi wengine.
-          Kuwaheshimu na kuwachukulia vema wafanyakazi wenzako na wewe binafsi pia.
-          Kutoa maslahi sawa na ya haki kwa mtoa huduma yeyote. (epuka dhuluma au ubahili)
-          Kushuhulikia mambo yote yanayohusu biashara yako au kazi yako kwa ukweli, uaminifu na katika muda sahihi.

*Waefeso 6:9 “Hivyo hivyo enyi waajiri wachukulieni waajiriwa/wafanyakazi (subordinates) kwa haki, msiwaudhi mkijua kuwa wote tuna mwajiri mkuu mbinguni, Yeye aisye upendeleo.”

Baadhi ya maadili yanayomlenga mfanyakazi / mwajiriwa.
 • Fika katika eneo la kazi kwa muda muafaka na pia toka kwa muda muafaka.
 • Fanya kila kinachoihusu ajira yako / kampuni yako katika kila sekunde uwayo katika eneno la kazi (usihamishie  mambo ya nyumbani au ya mtaani kazini).
 • Tunza mali / vitu vya ofisi /kampuni kwa uangalifu mkubwa na upendo, viangalie kama vile ni mali yako na unawajibu navyo. Hembu jaribu kuangalia mtazamo wa watu katika vitu vya umma, na ndiyo maana vingi havidumu (Hii ndiyo sababu ya magari ya umma kuwa juu ya mawe)
 • Heshimu kampuni au ofisi yako kwa uaminifu na kweli. Mtu awaye yoyote asikuhofie au kukushuku chochote katika nafasi yako, mfano kuwepo kwa mazingira ya rushwa.
Wakolosai 3:22-24 “Enyi waajiriwa, wafanyakazi waheshimu waajiri wenu katika kila kitu mfanyanacho. Muwaridhishe katika yote, sio tu wakiwa wanawatazama… mkijua kuwa mna mtumikia mwajiri mkuu Yesu Kristo.”
 • Maadili ni suala la uchaguzi binafsi na kwa hiyo, jinsi maadili ya sehemu ya kazi yanavyochukuliwa au kufuatwa inategemea sana maadili binafsi aliyonayo wewe mfanyakazi au mfanyakabiashara. Ni ngumu kufuata maadili ya kazi wakati hata wewe mwenyewe huna maadili yako binafsi, pia ni ngumu kufuata utaratibu uliowekewa au mliowekeana wakati hata ule wa maisha yako binafsi umekushinda.
 • Mtazamo mkubwa wa ulimwengu wa leo kuhusiana na maadili ya kazi ni kwamba, kosa kubwa unaloweza kufanya katika utendaji wa yote yasiyo haki katika eneo la kazi ni kukamatwa. Unachotakiwa kujitahidi kazini ni kukwepa kugundulika kuwa unapindisha baadhi ya maadili.
 • Juhudi kubwa makazini sasa imewekwa katika kuzisaka na kuzigundua mbinu za mwajiri au mashirika ya uchunguzi kama TAKUKURU, wakaguzi wa mahesabu (auditors), na kutafuta ufumbuzi wa kuwakwepa.Mtazamo wa kibiblia:

1 Wakorintho 4:2 “Sasa basi yawapasa wote walioaminiwa katika chochote kuuonyesha uaminifu.”
Lazima kuonyesha uaminifu ili tuweze kutumainiwa na kuaminiwa zaidi.
Kumbuka, “Aliye mwaminifu katika madogo huaminika zaidi pia katika makubwa.....”
1 Wathesalonike 5:24 (KJV) “Iweni waaminifu kama yeye aliyewaita.”
·   Ebu jitazame kama aliye ajiriwa na Mungu, Je utafanya unayoyafanya katika eneo lako la kazi leo?
·   Nidhamu ya kazi ni matokeo ya uaminifu, na uwakili mwema katika mamlaka iliyoko na uaminifu kwa Mungu mwenyewe.
-   “Utamheshimu Mungu kwani yeye ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri.”

Categories:

Leave a Reply