Tunapozungumzia uwezo wa kujitegemea na kujisimamia mwenyewe tunalenga ule uwezo wa kufanya mambo yako wewe mwenyewe. Namaanisha pia uwezo wa kufanya kwanza kile kinachokuhusu na unachokiweza na ndipo baadae waweza kuomba msaada iwapo inalazimu badala ya kuanza kuomba usaidiwe kabla ya kujaribu wenyewe. Uwezo wa kujitegemea ni muhimu sana katika maendeleo ya mtu binafsi na wengi wamejikuta wanashindwa kupiga hatua maishani, wala kufanya maamuzi yeyote ya muhimu na yatakayoweza kubadilisha maisha yao kwa sababu tu hawawezi kujitegemea kimawazo, kifikra na kimsimamo. Wengi wamekuwa wakiburuzwa tu na watu wengine au na wakubwa wao wa kazi au hata ndugu zao au wazazi wao pasipo wao kuonyesha misimamo au ujasiri walionao. Yamkini unatamani moyoni mwako kufanya au kupata kitu fulani unachokitamani lakini unabaki kuumia sana moyoni maana ukweli ni kwamba wewe binafsi huwezi kukifanya au kukisema hicho unachokitamani bali unabaki kufanya au kusema vile ambavyo wengine wamekuamulia.
Mfululizo
wa mada hii utakuwezesha kujijengea uwezo wa kuwa thabiti katika
kufanya kile ambacho ulikuwa huwezi kufanya hususan katika kujisimamia
na kujitegemea mwenyewe. Labda nitoe mifano michache;
Wako
wanandoa ambao mmoja wao hawezi kamwe kujisimamia na kujitegemea
kifikra au hata kimaamuzi, mchakato wa kufanya maamuzi yeyote hata yale
rahisi unakuwa mgumu sana. Tabu kubwa hutokea pale Mungu anapomchukua
mmoja wao.
Wako
watu waliooana lakini mmoja wao bado nguvu ya maamuzi yake iko kwa
wazazi wake au mzazi mmoja wa upande wake, labda mume hawezi kuamua kitu
chochote hadi amsikilize mama yake mzazi, ili ni tatizo kubwa. Au kila
mume anachofanya anaambiwa na na kuelekezwa baba yake mzazi. Kwa upande
mwingine wako wanawake pia ambao maamuzi ya familia zao hayawezi
kufanyika mpaka yaafikiwe au kusahihishwa na mama mzazi wa mwanamke,
hapo iko shida kubwa pia. Tofauti au kinyume na kujitegemea ni kuwa
tegemezi. Utegemezi ni hali ambayo haifurahishi moyo hatasiku moja na
huzuia au kudumaza maendeleo ya mtu.
Tuangalie faida za kujitegemea na kujisimamia mwenyewe.
Ø Utaweza kuvijua vitu au mambo vizuri au bayana zaidi pale utakapo yatafuta wewe mwenyewe na sio kwa kusaidiwa.
Ø Ujasiri
wako hukua pale unapojitegemea kimawazo. Ukiwa unauliza kila kitu kwa
wenzako, ujasiri wako huathiriwa kwa kiwango kikubwa.
Ø Kwa kujitegemea tunaokoa muda. Unapowategemea wengine sana, unapoteza muda kila wakati kuwatafuta na kuwasubiria ili wakusaidie.
Ø Utaweza
kufanya mambo kwa uangalifu mkubwa ukijua kuwa wewe peke yako ndiyo
mwajibikaji wa matokeo. Kwa hiyo utaweza kufanya vitu vilivyo vya ubora
zaidi.
Tuone pia hasara za kutokujitegemea au kuwa tegemezi kifikra na kiutendaji:
Ø Kutojitegemea
mwenyewe sio tu kunakunyima faida zilizotajwa hapo awali bali
kunakufanya uishi maisha yasiyo na nguvu (powerless life) na maisha ya
kushindwa. Maisha haya baadhi ya wanasaikolojia wameyaita. Ni maisha ya
uathirika, Maisha ya kujihatarisha, Maisha ya kuidhinishiwa na Maisha ya
kujilaumu.
Uhalisi
wa mawazo ya wanasaikolojia hawa umesimama kwenye ukweli kwamba yeyote
mwenye tabia tegemezi huwa na fikra au mawazo yafuatayo.
· Huwa
na tabia ya kuwaza kama vile anatarajia kuhatarishwa na kitu fulani na
kwa hiyo hubaki kulaumu ile hali ya kufikirika ya ile hatari (hulaumu
wasichokiona kama vile kimeshatokea).
· Hufikiri
kwamba kusaidiwa ni haki yao na sio kama zawadi tu, fikra hizi
huwadhoofisha na taratibu huleta matatizo makubwa hususani mmoja
anapokuwa kwenye mahusiano kama vile uchumba au hata ndoa.
· Hufikiri
kwamba maisha yake yako hatarini na wengine ndio wanaoweza kumsaidia
aondokane na hatari hizo mawazo haya humfanya mtu huyu kujiona mtazamaji
tu wakati wengine ndio watendaji.
Watu
au mtu mwenye mawazo kama haya anafananishwa na yule ambaye kwa kuhofia
ajali za barabarani humkabidhi mtu mwingine gari ili amwendeshe, hata
kama ujuzi wa huyo aliyepewapewa kundesha gari ni mdogo.
Watu
wajinsi hii au wenyetabia hii huwalaumu na kuwashutumu wengine badala
ya kuchukua majukumu ya kuyaendesha maisha yao wenyewe. Tabia ya kulaumu
wengine kama wao ndio chanzo cha matatizo yanayotokea kwetu inaathari
kubwa sana kimafanikio. Mfano; Kwa kuwalaumu wengine kwa yale
yanayotokea kwetu inapunguza hamu ya kujibidisha na kushuhulikia mizizi
ya matatizo yetu.
Kuwalaumu
wengine kila siku hutushawishi tuamini kuwa sisi ndio wenye matatizo,
kwa kuwalaumu wengine kila mara utajiona wewe ndio muathirika na kwamba
wao ndio washindi na wanyanyasaji wako. Kwa hali hii taratibu utaanza
kujiona uliyemnyonge, dhaifu na wakushindwa na wengine. Ukweli ni kwamba
wewe sio mnyonge na wakushindwa, bali tatizo ni utegemezi ulionao kwa
wengine.
Nini
kifanyike ili kukuza uwezo wetu wa kujitegemea na kujisimamia wenyewe.
Zifuatazo ni njia rahisi na zenye ufanisi katika kukuwezesha kukuza
uwezo wako wa kujitegemea na kusimama kwa miguu yako.
1. Miliki hisia zao. (Own your feelings)
Hii
inamaanisha kwamba inakubidi ukubali na kuamini kuwa wewe ndiye
unayeweza kufanya ujihisi vizuri au vibaya hususani pale ambapo mtu
fulani amefanya kitu kwako. Mfano; mtu anapofanya kitu au kusema kitu
ambacho kinakusumbua hutakiwi kutumia sentensi kama “unanifanya nijihisi
vibaya” au “usinifanye nikasirike” bali unatakiwa kusema “Najihisi
nimekasirika au “unanitia hasira”.
Pia
usiseme “Ulichokisema kimeniudhi sana” badala yake waweza kusema
“nimekasirishwa sana na ulichokisema” sentensi hizi “umenifanya
nijihisi” na “ninajihisi” zaweza kuonekana zinafanana lakini
zinautofauti mkubwa. Katika sentensi ya kwanza unawapa wengine au mtu
mwingine uwezo wa kukuudhi, lakini sentensi ya pili inaonyesha umiliki
wako wa kule kujihisi vile unavyojihisi. Iko tofauti ya kusema
“umenifanya nijisikie raha” na kusema “ninajisikia raha sana”.
Kwa
kutumia sentensi ya kwanza, unajiweka chini ya milki na utawala wa yule
anayekusababishia furaha au hasira wakati kwa kutumia sentensi ya pili
unamiliki uwezo wa kujipa raha hiyo wewe mwenyewe.
2. Zikubali hisia zako (Accept your feelings)
Ni
vema kukubali ukweli kwamba sisi wenyewe ndio tunaojisababishia kuhisi
vizuri au vibaya kwa yale ambayo tunajiambia wenyewe, na kwa hiyo basi
hatuna budi kukubali kubeba majukumu ya hisia zetu wenyewe. Pia kuwa
huru kujiambia au kujinongonezea kitu upendacho mwenyewe ingawa
unahitaji kukubali matokeo ya vile utakayojihisi.
Mfano;
Umempoteza mtu unayemjali sana na kumtegemea maishani. Waweza kujiambia
kuwa “maisha hayana budi kuendelea, nitajipa moyo”
Lakini
pia waweza kujiambia; “Basi tena, sintakuwa na mbele wala nyuma, maisha
yameshaharibika’ sentensi hizi zote mbili zitakuwa na matokeo tofauti
ndani yako, ni jukumu lako kuzikubali hisia zako na kuyakubali matokeo
yake pia.
3. Fanya kile unachotakiwa kufanya (Do your assignment)
Wakati
wowote unapokuwa na kazi au jukumu la kufanya mfano. Kazi uliyopewa na
mwalimu, bosi wako, mwalimu wako wa dini, mzazi wako nk. ifanye akazi
hiyo ukijua unaelewa kila kitu kinavyotakiwa kufanyika. Hata kama kwa
bahati mbaya unakuja kuonekana umekosea kidogo mwishoni, lakini
umeifanya kwa juhudi na maarifa yako mwenyewe. Baadaye waweza sasa
kuhitaji maelekezo kutoka kwa wengine nahii itakuwezesha kuwa na uhakika
na kile ulichokifanya zaidi ya kutegemea majibu au mwongozo wa wengine
kuanzia mwanzoni kabisa.
4. Tafuta kupata taarifa kutoka kwenye vyanzo halisi (Go to the Source)
Wakati
wowote tafuta kufahamu mambo au kupata taarifa yoyote kutoka chanzo
halali na chakuaminika, zaidi tu ya kuambiwa na watu ambao hata wao wako
kwenye kujifunza kama wewe. Kwa nini utegemee na kusimamia taarifa
uliyopewa na aliyesoma gazeti, kwani wewe huwezi kulitafuta ulisome
mwenyewe? Kuna watu ambao katika kila wasemacho wakiulizwa wamesikia
wapi, husema fulani alisema, hamna hata kimoja walichofanya jitihada za
kukitafuta wenyewe, au kushuhudia wenyewe.
Kuna
waandishi wa habari ambao huandika habari walizoambiwa na waandishi
wenzao waliomsikiliza mhusika akizungumza. Habari za waandishi hawa
wawili zitatofautiana, kwa sababu ya ukweli kuwa mmoja amendika
alichokisikia kwenye kutoka kwenye chanzo na mwingine ameandika
alichokisikia kutoka kwa aliyesikia.
Wataalamu
wa mawasiliano wanathibitisha kwamba, kwa kadiri taarifa au habari
inapopita kwa watu wengi kutokea kwenye chanzo husika ndivyo inavyozidi
kupotoshwa ule uhalisia wake na mwisho wasiku, wale waliopata habari
hiyo baadae sana hupata taarifa yatofauti kabisa, na hata wanapoisema
hukosa ujasiri maana hawana uhakika nayo. Kwa tabia ya kupenda kwenda
kwenye vyanzo halisi tunaepuka kupotoshwa na wengine na tunajijengea
ujasiri katika yale tunayoyafanya au kuyaongea.
5. Epuka kutafuta uhakika toka kwa wengine kila mara
Kila
wakati jaribu kufanya kwanza kile unachokiamini. Epuka kuuliza uliza
juu ya vitu ambavyo tayari unauhakika navyo, kisa tu unataka walau mtu
mwingine akuhakikishie au kukuthibitishia kuwa unachokiamini ni kweli.
Mfano;
kama wewe ni mgeni wa mkoa unaouendea wa Dodoma na mabango unayoyaona
yanakuonyesha jina la eneo au mji wa Dodoma, hakuna haja ya kuuliza mtu
mwingine “eti ndio tumeshafika Dodoma’. Wakati kila bango na ishara
inakuonyesha kuwa tayari uko Dodoma. Tofauti na swali la kwanza, waweza
kubadili na kutumia sentensi na kusema “Angalia Dodoma inavyopendeza”
kama umekosea chochote, mtu huyu wapili ataweza kukusahihisha.
6. Epuka maelezo yenye viulizo vya maswali (Avoid Questions tags)
Ingawa
maelezo yenye viulizo vya maswali ni muhimu katika mawasiliano, lakini
ikiwa nia ni kujenga uwezo wa kujitegemea na kujisimamia maswali haya
sio mazuri, hususani pale ambapo nia ni kumfanya mwingine
kutuhakikishia au kututhibitishia kile talichokiongea. Njia rahisi ni
kujiuliza wewe mwenyewe kuwa ungejisikiaje ikiwa huyu mwezako
uliyemuliza asingekubaliana na kile ulichokisema?
Mfano;
Epuka kusema “Nimependeza! si ndiyo? Badala yake sema “nimepandeza”.
Sentensi ya kwanza yenye swali na “si ndiyo?” humpa uwezo na mamlaka
aliyeulizwa kukupa uhakika wa kupendeza kwako au kukukatisha tama kuwa
kujapendeza, bali sentensi ya pili isiyo na swali la
“si ndiyo?”kukupa umiliki wewe mwenyewe, pasipo kumtegemea yeyote kuthibitisha juu ya kupendeza kwako.
7. Epuka mijadala yenye mabishano (Avoid heated discussion)
Badala
ya kujiingiza katika mijadala yenye misuguano ili tu kuwashawishi
wengine waone unachoongea ni cha ukweli jaribu kukaa kimya na kwa
utaratibu na ufupi ukiseme unachokisema ukikiaminikuwa ni cha kweli.
Mijadala
yenye mabishano na mivutano huonyesha kuwa hatuna uhakika na kile
tunachokiongea na kwa hiyo tunakuwa na hofu pale ambapo wengine
hawatuungi mkono.
Kibaya
kingine kinachoweza kukutokea unapojiingiza kwenye mijadala yenye
misunguano ni kwamba unabaki kuwa kichekesho kwa wale wanaokusikiliza na
kukuangalia, mara unajigundua kuwa kila unapoanza kuongea wengine
wanacheka, utajiumiza kichwa bure, na kumuumiza kichwa yule mnayebishana
naye. Tatizo baadae utajisikia kuhukumiwa na kujilaumu, wakati mjadala
wowote wenye kujenga kamwe hauna majuto.
8. Heshimu mawazo ya wengine (Respect others issues)
Kumbuka
kwamba watu hutoa mawazo yao wakiamini kuwa vile wanavyovisema ni vya
kweli. Yamkini wanayaamini mawazo yao maana wana uzoefu wa muda katika
vile wavavyovisema na ndiyo maana wanathubutu kusema hivyo
wanavyovisema, watu hawa wanahakika kuwa wayasemayo ni kweli sawa sawa
na vile wewe unavyoamini kwamba unayoyasema ni kweli.
Ili
kubadili mtazamo huu wa mtu yahitaji uwezo wa ushawishi na kujadiliana
kwa upendo. Mtu mwenye busara daima huanza kwa kuheshimu mawazo ya
wenzake na siyo kuyapinga na taratibu baada ya kuyaheshimu, huanza
kuonyesha ubora wa yale aliyonayo na mapungufu yaliyopo kwa yale wengine
waliyonayo. Kamwe usianze kwa kuponda, kulaumu au kukejeli, kwasababu
kwa kufanya hivyo yawezekana ukafunga milango hata kwa mawazo yako
kutopokelewa tena.
9. Jenga tabia ya kutembea hatua ya zaidi (Learn the habit of going a step further)
Hii
ni tabia ya kuweza kufanya zaidi ya ulichoambiwa au ulichoagizwa pasipo
kutegemea au kutarajia malipo au upendeleo tofauti. Kama utakuwa na
tabia hii kamwe hutahitaji mtu wa kukusimamia ili umalize kazi yako.
Watu wenye tabia hii pekee ndio wenye uwezo wakuwa mabosi juu ya kazi
zao wenyewe. “bosi wako anakuwa ni wewe mwenyewe”. Ziko aina mbili mbaya
sana za watu kinyume na hii niliyoitaja hapa juu. Wako wale wasioweza
kufanya lile wanalotarajiwa kulifanya. Na pia wako wale ambao hufanya tu
lile walilotarajiwa kulifanya. Kamwe wewe usiwe kati ya hawa.
10. Kuwa mgunduzi (Be innovative)
Huu
ni uwezo wa kutumia njia mbalimbali, mawazo mbali mbali na jitihada
mbalimbali ili kushuhulikia changamtoto za kila siku maishani.
Ili kuwa mgunduzi yahitaji mtu mwenye mitazamo au tabia za aina mbili.
(a) Kwanza
yakupasa uitazame elimu tunayoipata mashuleni kama nyenzo ya kutusaidia
kuyashuhulikia matatizo ya maisha. Hii ina maana, utatumia yale
uliyoyapata au kufundishwa shuleni au chuoni kuyakusianisha na utatuzi
wa changamoto za maishani na kamwe hautamhitaji tena mwalimu akueleze
jinsi ya kufanya kila kitu.
(b) Aina
nyingine ya tabia ni ile ya kuweza kuziamini njia na mbinu
unazozigundua wewe mwenyewe. Unapogundua au kuwaza kitu na ukaona
kinauwezo wa kutatua changamoto fulani kimaisha basi endelea kukitumia
au kuzitumia mbinu hizo mradi tu mbinu hizo ziwe zenye maadili. Kama
wewe ni mtu usiyeweza kujitegemea na kujisimamia mwenyewe kamwe
hutoziamini mbinu ulizozigundua hata kama mbinu hizo zinaonekana
kufanya kazi, kwa kuwa wewe mwenyewe hujiamini. Kwa kuwa mgunduzi
kutakuongezea uwezo wa kujitegemea na kujisimamia.
Categories: