UJASIRIAMALI MBINU ZA KUPATA UTAJIRI WA KUDUMU-
UNAWEZA KUACHA KAZI NA KUJIAJIRI

HUENDA wengi wakashtushwa na mada hii lakini ni ukweli usiopingika kuwa kuiajiri ni bora kuliko kuajiriwa. Kama wewe umeajiriwa, unaweza kuacha kazi na kujiajiri mwenyewe. Ni rahisi na kamwe hutajutia uamuzi wako.

Wengine hufananisha suala la kuacha kazi na tukio la kuruka kwenye dirisha la ndege ukiwa na parachuti ukitegemea kama litafunguka ili utue salama. Kama utajiandaa vyema, utakuwa sawasawa na mtu ambaye ameelekezwa vizuri namna ya kutumia parachute na amejiandaa barabara kiakili na kihisia.

Utafiti unaonyesha kuwa katika kila biashara zinazoanzishwa, asilimia 95 huanguka ndani ya miaka mitano na 5% huendelea. Lakini baada ya hapo asilimia 95% ya biashara ya asilimia hii huanguka ndani ya miaka 5 ifuatayo. Kwa nini kiwango cha biashara kuanguka ni kikubwa hivi? Kwa nini watu wengi huwa wanafilisika? Zifuatazo ni baadhi ya sababu:

1. Mjasiriamali kukosa uzoefu wa biashara
2. Mjasiriamali kukosa ujuzi na maarifa ya masoko
3. Kukosa nidhamu ya pesa
4. Kukosa mtaji
5. Mauzo kuwa chini
6. Kushindwa kuendana na baadhi ya wafanyakazi wake
7. Kuchukua mkopo mwingi bila matumizi sahihi
8. Kukosa stadi za mafanikio katika ujasiriamali
9. Kukosa msukumo binafsi wa kufanya mambo sahihi
10. Kujaribu kufanya biashara nyingi sana au mambo mengi ambayo yote yanahitaji muda na umakini (lack of focus)
11. Kukosa ndoto na shauku ya kufanikiwa
12. Magonjwa na afya mbovu
13. Tabia ya kuahirisha mambo mra kwa mara
14. Kukata tamaa kwa urahisi mambo yanapoonekana magumu
15. Mtazamo hasi (negative mental attitude)
16. Hali ya kutaka kitu bila kitu.
17. Marafiki au washirika wasio sahihi katika biashara yako (mkeo au mumeo aweza kuwa kikwazo)
18. Hofu na kutokuthubu
19. Kushindwa kufikiri kwa makini na kupenda kukisia mara kwa mara.

NATAKA KUACHA KAZI, NIFANYE BIASHARA GANI?

Mara nyingi hilo ndio swali ambalo huwa ninaulizwa sana. Watu hunipigia simu wakisema kuwa wamenisikia

kwenye vipindi vyangu vya ujasiriamali (huwa naendesha vipindi vya redio vya ujasiriamali) na hivyo huomba ushauri wa waanze vipi na wafanye biashara gani
Hilo ndiyo swali la muhimu sana kwa mtu anayetaka kuwa mjasiriamali na linaweza kumsaidia mtu kupata majibu sahihi ya kitu atakachokifanya na kumletea mafanikio maishani.

Watu wengi wakiulizwa ni biashara gani inaweza kukupatia fedha kwa urahisi, hujibu kwa kuangalia watu waliofanikiwa kupitia biashara mbalimbali na kuzitaja biashara hizo kama ndiyo zina faida kubwa. Ukweli ni

kwamba biashara yeyote inaweza kufanikiwa ikiwa itapata wateja wengi wakutosha. Hivyo suala la msingi, sio biashara gani ya muhimu, bali ni vigezo gani vya msingi.
KABLA HUJAACHA KAZI ZINGATIA YAFUATAYO:

• Chunguza siri za biashara zinazofanikiwa na mifumo iliyopo nyuma yake. Jaribu kuziangalia biashara za Wahindi na Waarabu zinazofanywa. Watu wengi huwa na wazo la bidhaa ya kuuza au hata kutengeneza kama vile mshumaa, rangi, shampoo nk lakini mara nyingi huwa hawana ujuzi wa kutengeneza mfumo mzuri wa uletaji wa faida.

• Pata mlezi au mshauri (Mentor) atakayekusaidia katika safari ya ujasiriamali. Neno mentor linamaanisha mtu ambaye amefanikiwa kwenye jambo fulani na ana uwezo wa kuwasaidia/kuwaelekeza watu wengine wafanikiwe kama yeye.

• Fanya kazi kwenye biashara ya mtu aliyefanikiwa na ambaye unataka kuja kuwa kama yeye. Wakati mwingine, njia ya mkato ya kujifunza biashara ni kukubali kutumika chini ya mtu mwingine ili ujionee moja kwa moja uendeshaji wa biashara kabla hujaamua kuingia moja kwa moja.

• Jenga tabia ya kuwauliza maswali ya msingi wajasiriamali waliofanikiwa. Kila unapopata nafasi ya kuwa na mtu tajiri, jipe moyo mara kwa mara halafu uliza swali hili: “Je siri ya mafanikio yako ni nini?”Utashangaa jinsi ambavyo watu wengi si wachoyo wa siri zao za mafanikio ili mradi tu uulize katika mazingira mazuri yenye heshima na hekima.

5. Jijengee uwezo wa kuuza. Uwezo wa kuwashawishi watu waweze kununua bidhaa yako au kutumia huduma yako ndiyo uweze kusimama katika ujasiriamali.

Categories:

Leave a Reply