Muda ulipita tulijadili kwa kina namna unavyoweza kupata mafanikio katika sekta mbalimbali kama ukiamua kuwa mjasiriamali. Tulifafanua kwa kina nini cha kufanya unapoamua kuwa mjasiriamali. Leo tunaendelea na mada yetu...

NINI CHA KUFANYA BIASHARA YAKO INAPOKWAMA?

Inapotokea umekwama kwa namna yoyote ile katika biashara yako, hutakiwi kukata tamaa bali jiulize maswali yafuatayo:
•Umewahi kushindwa mara ngapi katika maisha yako? Nini ulijifunza uliposhindwa, iwe ni kwenye biashara, ajira au mambo yoyote ya kimaisha?
•Je, unamfahamu mjasirimali/wajasiriamali gani ambao wamefanikiwa kuliko wewe na unaweza kujifunza kutoka kwao? Hata kama ni maarufu na wako juu sana, panga mpango wa kuonana nao na kuomba ushauri. Usiogope, wengi huwa hawana shida na wanapenda kuwasaidia watu kwa kutoa ushauri ili mradi tu ukiomba kwa heshima na usionyeshe kwamba unataka kuchezea muda wao.
• Unafikiri ni jambo gani limesababisha ukakwama katika biashara yako? Ulikosea wapi na nini cha kufanya ili yaliyotokea yasijirudie?
Ukijiuliza maswali haya, bila shaka utaanza kuona kuwa unayo nafasi ya kuinuka kutoka pale ulipokwama na kuendelea na biashara yako.

HATUA TATU MUHIMU
Siri za mafanikio ya biashara siku zote zimekuwa na zitaendelea kuwa rahisi na zimepangwa katika hatua tatu muhimu:
Hatua ya Kwanza: Mtafute mtu wa kumuuzia bidhaa au kutoa huduma.
Hatua ya Pili: Ukipata mteja, hakikisha unamhudumia vizuri ili arudi tena kwako kwa mara nyingine.
Hatua ya Tatu: Hakikisha bidhaa au huduma unayotoa ina ubora wa kumfanya mteja mmoja akawashawishi wenzake kuja kwako.
Watu wengi hawana fedha kwa sababu hawana kitu chochote wanachouza kwa watu wengine. Wengi wetu tunajua zaidi kununua kuliko kuuza hivyo tunatoa fedha nyingi kuliko tunazoingiza. Kama huna kipato cha kutosha, unapaswa kuanza kujiuliza swali hili: “Je, unataka kuuza nini? Utamuuzia nani?”
Usumbue ubongo wako mpaka ukupe majibu matano, halafu chukua muda kufikiria ni biashara gani unadhani unaweza kuwa unaielewa vizuri na unaweza kuifanya kwa bidii au unaweza kumpata mtu anayeielewa vizuri akusaidie. Ukipata majibu tayari utakuwa umeianza safari ya kuelekea kwenye mafanikio.

MAKUNDI MATANO YA MABILIONEA
Kuna milango mitano ya watu kuwa matajiri wakubwa ambayo mabilionea duniani wanatokea:

1. WATAALAMU WANAOLIPWA VIZURI
Kundi la kwanza ni wanataaluma wanaolipwa vizuri (well paid professionals) kama wanasheria wazuri, madaktari bingwa na wahandisi. Wengi waliofanikiwa katika kundi hili wanajua jinsi ya kuweka akiba na kuwekeza akiba zao kwenye maeneo yenye marejesho mazuri. Mabilionea wanaotokea kundi hili ni asilimi 10 tu ya mabilionea wote.

2. WAKURUGENZI WA MAKAMPUNI MAKUBWA
Kundi lingine la mabilionea ni wakurugenzi wanaolipwa vizuri na makampuni makubwa (well paid executives). Hawa ni asilimia 10 ya mabilionea wote pia. Mara nyingi hawa huwa wametoka na kampuni mbali na wamekua nayo wakipandishwa cheo baada ya cheo mpaka kufikia hatua ya juu. Mara nyingi, watu wachache katika kundi hili huwa na uwezo mkubwa wa kuzishikilia fedha zao na kutozifuja na hiyo huwafikisha kwenye ubilionea.

3. MAAFISA MAUZO
Kundi la tatu ni maafisa mauzo au mameneja wa idara za mauzo. Hawa huwa ni takriban asilimia 5 ya mabilionea wote na kinachowafanya wawe mabilionea ni kwa sababu ya nafasi ya kupata kamisheni kutokana na mauzo wanayoyafanya. Wengi wao huwa ni waajiriwa wa makampuni ambayo wamekuwa wakifanya nayo kazi kwa muda mrefu na kuzifahamu vizuri na baadaye kuja kuwa na milango mingi ya mafanikio.

4. WATU WENYE VIPAJI MAALUM
Kundi la nne ni watu wenye vipaji maalumu kama wanamichezo, wanamuziki, watunzi wa filamu na vitabu na kadhalika. Hawa ni wachache sana 1%, lakini huonekana wengi sana kwa sababu ya kelele zinazoendana na umaarufu wao.

5. WAJASIRIAMALI
Hili ndiyo kundi kubwa kuliko mengine yote, asilimia 74% ya mabilionea wote ni wajasiriamali. Hii inamaanisha kuwa nafasi ya mtu yeyote kuwa bilionea ni kubwa zaidi kupitia ujasiriamali kuliko kitu kingine chochote.

Itaendelea

Categories:

2 Responses so far.

  1. Ahsante kwa dondoo nzuri za Mafanikio Ya Kiuchumi. Naamini utaendelea na muendelezo wa hiyo post. Nami pia nakukaribisha utembelee Life Skills Blog ( www.kamotta.blogspot.com ) upate dondoo nyingi za maisha na maarifa.

  2. asante mkuuu na tuendeleee kushirikiana

Leave a Reply