MAFANIKIO YAPO KILA SEHEMU

Wapo wenye dhana kwamba ili ufanikiwe ni lazima ukafanye biashara au kazi nje ya nchi kama Dubai, marekani, Uingereza na sehemu nyingine za Bara la Ulaya. Dhana hiyo ni potofu kwani ukweli kwamba hakuna sehemu ambayo ina fursa nyingi za kukuwezesha kutajirika kwa urahisi kama barani Afrika hususan Tanzania. Hapa kuna kila kitu; watu, malighafi, na fursa za kila aina.


Pia kwa sababu watu wengi sana si wajasiriamali, jambo hilo linakupa fursa ya kuneemeka zaidi. Wajasiriamali wengi waliopo nchini hawaoti ndoto kubwa, kitu kinachomaanisha kuwa kama utaanza kupanga mipango mikubwa, unaweza kuwa mtu wa kushangiliwa na wengine kwa jinsi maisha yako yanavyoweza kuwa bora.


UTAFITI WA KITAALAMU UNASEMAJE?

Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Profesa Paul Collier kutoka kutoka Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani umeonesha kuwa katika makampuni 950 ya Kiafrika yaliyofanikiwa miaka ya hivi karibuni, yalirejesha na kukuza mitaji yake kwa asilimia 11 zaidi ya makampuni ya Amerika ya Kilatino (Latin America) na Asia na makampuni haya ya Kiafrika yamepata faida asilimia 70 zaidi ya makampuni ya Kichina yanayofanana nayo.

Kutokana na utafiti wa Collier, kuna matumaini kuwa wawekezaji wanaowekeza kwenye masoko ya nchi zinazoendelea wanaweza kuanza kuwekeza kwa kasi zaidi hapa Afrika, masoko ya hisa ya Afrika kuondoa lile la Afrika ya Kusini yanakuwa kwa kasi ya ajabu huku yakiongeza

mitaji yake maradufu kutoka dola bilioni 11 3.4 hadi dola bilioni 224.7 ndani ya kipindi cha miaka kumi kuanzia 1992 na 2002.

Ninayasema yote hayo msomaji kukuonyesha jinsi ulivyo na nafasi kubwa ya kufanikiwa hapa Afrika kupitia ujasiriamali.

UKITAKA KUWA MJASIRIAMALI, ANZIA HAPA


Baada ya kueleza hayo machache, bila shaka wengi wanataka kufanikiwa kupitia ujasiriamali lakini huenda watu hawajui maana yake na nini cha kufanya ili kufanikiwa kupitia ujasiriamali.

• Fanya utafiti wa bidhaa au huduma unayotaka kuanza kuitoa kwa kuzingatia maeneo uliyopo, upatikanaji wake na upatikanaji wa wateja. Jiulize, ni maeneo gani ambayo wewe binafsi unadhani unaweza kuwekeza/kuanzisha biashara na baadae kuwa bilionea?
•Jitayarishe vizuri kabla hujaanzisha biashara yeyote. Kamwe usikurupuke hata kama faida inaonekana ni nzuri. Matajiri wakubwa na wawekezaji mahiri huangalia kwanza usalama wa mtaji kabla ya kuangalia faida.
•Jiamini na usiwe na hofu ya kushindwa. Kama wewe ni muumini wa dini yoyote, mwamini Mungu kisha jiamini binafsi. Amini kwamba unachofikiria kukianzisha kitafanikiwa na yashinde mawazo ya kufilisika, kuibiwa au kupoteza fedha. Kwa mjasriamali kujiamini binafsi (self-confidence) ni moja kati ya siri kuu za mafanikio.
•Kamwe usikate tamaa katika maisha yako. Watu wengi, kwa sababu ya kutojua, hukata tamaa wakati wako jirani sana na mafanikio. Usiwe kama

wao, ili kushinda maishani itakupasa uwe king’ang’anizi wa kufuata ndoto zako, na uwe tayari kupambana kwa muda mrefu, wakati mwingine hata kama huoni dalili za kufanikiwa! Hii ndiyo namna mabingwa wote walivyoweza kuwa mabingwa.

Kushindwa ni jambo la kawaida sana maishani kiasi kwamba mtaalamu maarufu wa Uongozi duniani John C. Maxwell ameandika kitabu kizima

‘Failing Forward’ (kushindwa kwa kwenda mbele) akielezea namna ya kusonga mbele bila kukata tamaa hata kama unashindwa mara nyingi.

Bila shaka umesikia habari za Thomas Edson aliyewahi kushindwa mara elfu kumi katika juhudi zake za kutengeneza taa ya umeme. Hakukata tamaa na ndio maana leo tuna taa za umeme.

Itaendelea

Categories:

One Response so far.

  1. Anonymous says:

    Asante sana kwa kuandika makala inayotia moyo, ili kuondokana na umaskini na mawazo potofu kuwa mafanikio yako nchi za Magharibi

Leave a Reply