Leo nimemkumbuka sana mdogo wangu wa hiari KOERO MKUNDI..sijui yupo wapi. nimemiss sana uandishi wako ambao ninauhusudu sana na ndio maana nimeona niweka moja ya makala azilizoandika na iliyonigusa sana. Kumsoma zaidi mdada huyu ingia hapaNusura niwe mtoto wa mitaani
Juzi ijumaa nikiwa ofisini kwangu alipita binti mmoja akiwa na begi lake dogo kama yale yanayotumiwa na wanaume kubebea Lap Top.
Alinisalimia kwa uchangamfu na kujitambulisha kwangu kuwa anitwa Yasinta. Alionekana kuwa mchangamfu utadhani tunafahamiana siku nyingi, hata hivyo na mimi nilimchangamkia pia. Kumbe Yasinta ni mfanyabiashara wa kuuza viungo mbalimbali kama vile vya Pilau, viungo vya Chai, kwa kweli sikujua kama chai nayo ina viungo, pia alikuwa na viungo vya kupikia nyama , samaki au hata kuku na hasa kuku wa kienyeji na alitumia muda huo kunifundisha namna ya kutumia. Kwangu mimi hayo yalikuwa ni mapinduzi makubwa katika mapishi ya vyakula vya kiswahili
Yasinta Alionekana kuwa ni mdogo kiumri yaani ukimuangalia kwa haraka haraka anaonekana kuwa na umri wa kama miaka 18, hata hivyo sikukosea sana kwani nilipoomuliza umri wake aliniambi kuwa ana umri wa miaka 19 na mwishoni mwa mwaka huu ndio atatimiza umri wa miaka 20. Mara akaja jirani yangu mmoja ambaye ofisi zetu zinafuatana, alipomuona Yasinta alimshangilia sana na kuwaita wenzake na kuwajulisha ujio wa Yasinta, nilibaki nimeduwaa.
Baadae niliambiwa kuwa Yasinta alikuwa ni maarufu sana pale kwani alikuwa akiwauzia viungo vya mbalimbali na hivyo kufurahia mlo wao wa siku. Waliniambia kuwa walimfahamu Yasinta takribani miaka mitano iliyopita tangu alipoanza kuwapitishia ile biashara, wakati huo akiwa ni binti mdogo sana kwa umbo na umri.
Ni mwaka jana mwishoni alipowaaga kuwa anatarajia kufunga ndoa, na walimchangia fedha na zawadi nyingine. Tangu wakati huo Yasinta hakuonekana mpaka wakadhani labda ameamua kuachana na biashara hiyo, au mumewe amemkataza kuendele nayo.
Nilinunua viungo mbali mbali na niliamua kutumia fursa hiyo kufanya mazungumzo nae.
Yasinta alianza biashara hiyo mnamo mwaka 2005 Mara baada ya kumaliza darasa la saba mkoani Mbeya.
Je alifikaje mjini?
Yasinta alikuja mjini mwaka 2004 akiwa ndio amemaliza darasa la saba, baada ya kuwa hakufaulu na mama yake kutokuwa na uwezo wa kumuendeleza kielimu alichukuliwa na mama mmoja aliyekuwa akiishi maeneo ya Ilala hapa jijini Dar es salaam mwenyeji wa huko huko Mbeya ili kuja kufanya kazi za ndani.
Baba yake alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu wakati alipokuwa darasa la nne na kuanzia hapo majukumu ya kutunza familia aliyabeba mama yake pekee. Akiwa ni wa kwanza kuzaliwa na binti pekee kwa wazazi wake huku akifuatiwa na na wadogo zake wawili wa kiume, hakuwa na jinsi ilibidi aje mjini kufanya kazi za ndani ili aweze kumsaidia mama yake kuwatunza wadogo zake.
Alidumu na yule mama kwa mwaka mmoja. Lakini kutokana na mateso ilibidi atoroke na kujikuta akishia mtaani. Siku moja katika mizunguko yake ya kutafuta kazi alikutana na mabinti wa umri wake ambao walikuwa wakijiuza maeneo ya Buguruni na walimtaka ajiunge nao ili kujitafutia kipato, na walimuhakikishia kuwa shughuli ile ya kujiuza ina kipato kushinda hata ya kuajiriwa, hata hivyo Yasinta alikataa kata kata kujiunga nao, akamua kujichanganya na wale mama ntilie pale Buguruni CCM kwa kuwasaidia ili kujipatia kipato, hata hivyo mama mmoja allijitolea kumpa hifadhi.
Siku moja akiwa katika shughuli zake kama kawaida, alipita mama mmoja na kuagiza chakula, wakati akimuhudumia na kwa kuwa alikuwa ndie mteja pekee kwa wakati huo alianza kuzungumza nae. Katika mazungumzo yao yule mama alimjulisha juu ya biashara ya Viungo, mbalimbali vya mapishi ambayo ndio aliyokuwa akiifanya. Yasinta alivutiwa sana na ile biashara na kwa kuamini kuwa ule ulikuwa ndio wakati wa kuondokana na kazi za kutumwa, alimuomba yule mama amfundishe namna ya kufanya ile biashara.
Kwa bahati nzuri yule mama alimkubalia na na kuahidi kumpitia kesho ili wafuatane nae ili akamuoneshe mahali anaponunulia na kumuonesha namna ya kutayarisha.
Na kweli yule mama alimpitia kesho yake. Yasinta alimuaga yule mama aliyempokea pale Buguruni na kuondoka na yule mama kuelekea Kariakoo kufanya manunuzi.
Yule mama alijitolea kumpa hifadhi ya muda nyumbani kwake maeneo ya Vingunguti na kumfundisha namna ya kutengeneza viungo mbali mbali, Kutokakna na bidii aliyonayo ilimchukua Kiasi cha mwezi mmoja Yasinta kufudhu mafunzo hayo.
Yule mama alimkopesha Yasinta mtaji wa shilingi elfu kumi wa kuanzia.
Yasinta anakiri kuwa awali alikuwa na wakati mgumu sana kutokana na biashara kuwa ngumu lakini yule mama alimpa moyo wa subira.
Haikuchukuwa muda mrefu hali ilibadilika na biashara kumnyookea na kuweza kulipa mkopo aliokopeshwa na yule mama yake mlezi ambaye alimfanya kama mama yake mzazi kutokana na kumlea. Ilimchukuwa mwaka mmoja Yasinta kuhama na kupangisha chumba chake maeneo ya Buguruni na kuanza kujitegemea huku akiendelea na biashara yake hiyo ya viungo. Kuanzia hapo akawa anatuma hela kwa mama yake huko mbeya ili ziweze kumsaidia.
Mwaka mmoja baadae Yasinta alifanikiwa kununua kiwanja chenye ukubwa wa nusu eka maeneo ya Kinyerezi na ili iwe rahisi kwake kujenga. Ikabidi ahamie Segerea ili awe karibu na kiwanja chake. Taratibu alianza kujenga nyumba yake ya vyumba viwili. Ilimchukua mwaka mmoja na nusu kukamilisha nyumba yake ya vyumba viwili na kufanikiwa kuweka umeme na kuhamia nyumbani kwake. Lengo lake la kwanza likafanikiwa.
Yasinta alijiwekea malengo makuu matatu, wakati alipoanza biashara ya viungo.
Aliyataja malengo hayo kuwa ni kujenga nyumba yake mwenyewe, kukarabati nyumba ya mama yake kule Mbeya na kuwasomesha wadogo zake mpaka chuo kikuu.
Baada ya mdogo wake anayemfuatia kumaliza darasa la saba mwaka juzi akamleta na kumuandikisha katika shule ya sekondari ya binafsi iliyoko maeneo ya Ubungo na gharama za masomo analipa yeye kutokana na biashara yake ya viungo anayofanya.
Je Yasinta amemudu vipi kufikia hapo alipofikia na nini matarajio yake? Nilimuuliza.
Yasinta alikiri kuwa subira na uvumilivu ndio umemfikisha pale alipo sasa, kwani kuna wakati biashara ilikuwa haitoki kabisa mpaka anashindwa kulipa kodi ya nyumba, lakini kwa kuwa alikuwa amejiwekea malengo alihisi kuwa alikuwa na deni kubwa mbele yake na hiyo ilimpa hamasa ya kutokata tamaa na aliamini kuwa atafanikiwa.
Anasema aliponunua kiwanja alianza kuishi kwenye nyumayake kabla hata hajaijenga, kwani alikuwa akijiona kabisa kuwa amejenga na alikuwa akiiona nyumba yake ikiwa imekamilika kabisa, hakudhani kama atashindwa, aliamini tu kuwa ataweza.
Vipi kuhusu wanaume?
Nilimuuliza kwa kuwa yeye ni binti ambaye bado ni mbichi, kabla hajaolewa aliwezaje kukabiliana na vishawishi vya wanaume hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa akiishi peke yake na shughuli zake ni za kuzunguka maofisini?
Yasinta alikiri kuwa alikuwa akipata sana mitihani ya kutakwa na wanaume, wengine wakiwa ni wababa wazima wakuweza hata kumzaa mara tano lakini alikuwa amejiwekea nadhiri ya kutofanya mapenzi kabla ya ndoa, pia alikuwa amepanga kuwa hataolewa mpaka awe amejenga nyumba yake mwanyewe, kitu ambacho amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Je alimpataje Mwezi wake?
Yasinta alicheka kidogo, huku akiongea kwa aibu kidogo, alisema, “ Huyu mume niliyekuwa nae nilijuana nae miaka miwili iliyopita wakati akisoma sekondari wakti huo, tulikuwa tukikutana mara kwa mara kituoni tukisubiri usafiri wa daladala wa kwenda mjini. Kutokana na usafiri wa daladala Segerea kuwa ni mgumu tulikuwa tukigombea mabasi pamoja, siku moja akanilipia nauli, nilikataa kwa kuwa niliona kuwa yeye ni mwanafunzi, kwa hiyo haikuwa ni vyema anilipie nauli, lakini alisisitiza kunilipia na akakataa kupokea hela yake aliyomlipa kondakta wa daladala, na huo ukawa ndio mwanzo wa kufahamiana kwetu.
Baada ya kumaliza masomo alijunga na chuo kimoja mjini na kusomea mambo ya information Technology, na sasa ameajiriwa na kampuni moja binafsi akiwa ni mtaalamu wa kompyuta”.
Je mumeo anayo mikakati gani ya kukuendeleza kielimu, au ndio umeridhika na kiwango cha elimu ya darasa la saba ulicho nacho? Nilimuuliza.
Yasinta alisema kuwa ameanza kusoma masomo ya sekondari ya jioni katika shule moja ya binafsi iliyoko Tabata na ndio ameanza kidato cha kwanza ambapo itamchukua miaka miwili kumaliza kidato cha nne.
Ukweli ni kwamba nilifurahishwa sana na mazungmzo yangu na Yasinta, kwani ni miongoni mwa mabinti wachache hapa nchini wenye mtazamo chanya kuhusiana na maisha, na ameonesha kuwa, ukiamua unaweza, kwani hakuna kisichowezekana chini ya jua, kinachotakiwa ni kujiwekea malengo na kuwa na nia na dhamira ya kufikia malengo uliojiwekea. Kingine ni nidhamu katika kila jambo unalolifanya, kwani bila nidhamu hakuna kufanikiwa.
Hivi ni wasichana wangapi ambao wameshindwa kuendelea na masomo, na badala ya kujitafutia maendeleo kwa njia ya halali wamejikuta wakijiuza ili waweze kujikumu?
Ni wangapi wamekufa kwa ukumwi au wanaugua ukimwi sasa hivi baada ya kujiingiza katika vitendo vichafu vya kujiuza mwili?
Yasinta katuonesha njia kuwa tukiamua tunaweza.
Namtakia kila la heri katika ndoa yake, idumu na iwe na amani na upendo

source: http://www.ruhuwiko.blogspot.com/2013/03/kutana-na-yasinta-mjasiriamali.html

Categories:

One Response so far.

  1. gloria says:

    yasinta yasinta yasinta! yaan kma anaigza hv kumbe ni ukwel! jaman! G naomba no ya uyo dada ili npate viungo. mungu ni mwema atafnkiwa zaid.

Leave a Reply