picha kwa hisani ya google
BILA shaka ukiulizwa leo kama unataka kuwa tajiri, jibu lako litakuwa ni NDIYO! Lakini je, tunaelewa maana ya utajiri na namna ya kuwa tajiri? Hili ni swali ambalo majibu yake yanawasumbua wengi. Mada hii itakusaidia kupata mwanga wa maana na namna ya kuutafuta utajiri.

Wengi wanaamini kuwa ili mtu awe tajiri lazima awe na bahati ya kipekee. Watu wengi hudhani kuwa hawawezi kuwa matajiri mpaka watumie mizizi ya Bagamoyo, Tanga au Sumbawanga. Wengine huamini kwamba ili uwe tajiri, ni lazima uoe au uolewe na tajiri. Zipo imani nyingi juu ya utajiri, wengine wanaamini lazima uwe na ‘zali’, ufanye biashara ya magendo, ukwepe kodi, uibe, utoe uhai wa mtu au utumie njia nyingine haramu ndiyo uupate utajiri.



SIRI YA UTAJIRI HII HAPA


Siri kubwa ya mtu kuufikia utajiri wa kweli na wa kudumu, ni kuanzisha biashara yenye faida ambayo utakuwa na uwezo wa kuimiliki na siyo biashara ikumiliki wewe. Ukifanikiwa kuanzisha biashara yako, jambo la muhimu kuliko yote ni kuhakikisha unaipangilia ili iweze kujiendesha au kuendeshwa na watu wengine bila wewe kuhusika nayo moja kwa moja lakini kila kitu kiwe chini ya usimamizi na udhibiti wako.


Ukiwa na biashara inayojiendesha yenyewe, utakuwa na uwezo wa kuanzisha biashara nyingine zaidi, yaani ya pili. Hii ya pili ikifikia uwezo wa kujiendesha kama ile ya awali, sasa utakuwa na uwezo wa kufungua biashara ya tatu n.k.


Biashara ni kama mchezo fulani unaosisimua na inatakiwa ufurahie mchezo huo. Hivyo ndivyo wafanyavyo wajasiriamali wakubwa duniani kama akina Salim Bhakhresa na Reginald Mengi kwa hapa Tanzania, Aliko Dangote wa Nigeria, Mukhesh

Dhirubai Ambani wa India, Carlos Slim wa Mexico au Richard Brandson wa Uingereza mwenye makampuni zaidi ya mia tatu.


Jambo la kutia moyo ni kwamba, unaweza kujifunza kufanya hivyo. Kumbuka kuwa hakuna aliyezaliwa anajua kufanya kitu chochote hapa duniani zaidi ya kulia, mara tu tulipozaliwa. Kila tunachokifanya, tumejifunza baada ya kuwa wenyeji hapa duniani. Vivyo vivyo, kila kitu hapa duniani, ukiwa na nia ya kweli, unaweza kujifunza mpaka ukafanikiwa na kuwa mtaalam.


Ni vizuri kufahamu pia kwamba, sio lazima uwe na biashara nyingi ili uwe tajiri. Wapo wajasiriamali wengi mabilionea ambao wanafanya biashara moja tu ambayo utakuta imepanuka na kuwa kubwa katika nchi iliyomo au imefanikiwa kupata masoko mpaka nchi za jirani au hata za mbali.


Lengo la makala haya si kukwambia uwe kama Bill Gates au Warren Buffett (matajiri namna mbili na tatu duniani kwa sasa) au uwe na hela kuliko watu wote barani Afrika au Tanzania, japo hayo yote yanawezekana. Lengo ni kukufundisha namna ya kubuni, kuanzisha, kuendesha na kuipangilia biashara yako mpaka ifike hatua ya kujiendesha yenyewe.


Shauku yangu kama mwandishi wa ujasiriamali ni kukusaidia wewe msomaji kwa kukupa maarifa yatakayokufanya uanze biashara hata bila fedha au kwa mtaji mdogo ili hatimaye uwe na uhuru wa kifedha na muda, uishi upendavyo na usiteseke uzeeni. Nitakufundisha mbinu, mikakati na maarifa ambayo yatakufanya uwe mmiliki hodari wa biashara na mwekezaji mkubwa.


USIKUBALI MTU AKUCHAGULIE KESHO YAKO


Wakati wa uhai wako, kipawa kikubwa kuliko vyote ulivyonavyo ni kipawa cha kufanya uchaguzi wa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo mtindo wa maisha unaotaka kuishi. Baadhi ya mambo mazuri ambayo unaweza kuyafanya unapokuwa na uhuru wa kifedha na muda ni kama vile;

•Kusafiri na kuishi kokote ulimwenguni wakati wowote upendapo.
•Kujisomesha na kujilipia karo katika chuo chochote popote ulimwenguni.
•Kutembelea maajabu mbalimbali ulimwenguni.
•Kusoma vitabu vya riwaya, vya maendeleo binafsi au vyovyote uvipendavyo kwa uhuru.
•Kutumia muda wako kwa ndugu au marafiki wa muhimu zaidi.
• Kwenda kutazama mechi za kimataifa za michezo mbalimbali popote pale ulimwenguni na burudani zingine za aina mbalimbali.
• Kujifunza kuimba na kutoa CD yako kwa kuwa una muda na kipato cha kufanya hivyo.
• Kuogelea au kujifunza kuogelea na kufurahia uumbaji wa Mungu.
• Kuwatembelea wazazi wako mara kwa mara kadiri upendavyo.

Haya na mengine mengi, huwezi kuyafanya kama huna uwezo wa kifedha na muda hivyo ni muhimu kila mmoja akajifunza namna ya kutafuta fedha ili ayafurahie maisha.

source friend of mine MZIZI MKAVU MEMBER OF JF

Categories:

Leave a Reply