Written by stephen
LEO nitazungumzia suala la dhamana. Dhamana ina wigo mpana sana
ikihusisha aina zifuatazo: hisa, vipande, hatifungani na amana za
serikali.
Katika mada ya leo nitapenda kuaangazia aina mojawapo ya dhamana ambayo ni hisa na wakati ujao nitazungumzia dhamana nyingine.
Mbali na kuzungumzia suala la hisa leo, wajasiriamali wanashauriwa
kusoma baadhi ya vitabu ambavyo waandishi wameandika mada mbalimbali za
ujasiriamali ikiwamo uwekezaji katika hisa.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 84 ya Watanzania
wakiwamo wasomi na wengine ambao hawajabahatika kusoma hawajui au hawana
elimu kuhusu kuwekeza katika hisa.
Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba mada hii haijawekwa katika mitaala
mbalimbali ya elimu. Kama ipo basi wale wanaostahili kuifundisha ama
hawana uelewa mpana na uzoefu wa kuwawezesha wanafunzi wao kufahamu
umuhimu wake katika medani za kiuchumi.
Hisa inaelezeka kwa namna mbalimbali, kwa ujumla wake hisa ni mali,
rasilimali, kitegauchumi, hati miliki, biashara, dhamana ya mkopo, ni
akiba, ni fedha iliyohifadhiwa, na ni mtaji.
Katika mtazamo wa kibiashara, hisa ni uwekezaji wa mtaji au fedha ambayo
imewekezwa na mfanyakazi, mkulima, mfanyabiashara au mtu mwingine
ambaye ameamua kununua hisa kutoka katika kampuni fulani kwa lengo la
kupata faida kupitia gawio na ongezeko la bei ya hisa husika.
Uwekezaji katika hisa kama biashara nyingine unahitaji umakini na
upembuzi yakinifu. Kufanya upembuzi wa wapi uwekeze fedha zako na wapi
ununue hisa kwa msingi wa kupata faida.
Mjasiriamali au watu wengine wanaweza kufanya upembuzi yakinifu, lakini
kama watu makundi niliyoyataja hapo juu wana uelewa wa kutosha na mbinu
za kusoma taarifa mbalimbali za kampuni ambayo unakusudia kununua hisa.
Kwa mfano, unapaswa kufanya upepenuzi yakinifu wa taarifa za fedha na
hali halisi ya kampuni husika
katika soko la hisa.
Kwa upande mwingine, washauri wataalam wana ujuzi wa kufanya upembuzi
yakinifu katika masuala ya uwekezaji kwenye soko la mitaji ambao wa
wanapatikana kwenye masoko ya hisa katika jengo la Habour-view, mtaa wa
Samora, jijini Dar es Salaam.
Ununuzi wa hisa unaweza kufanywa katika soko la awali mathalani pale kampuni inapotangaza kuuza hisa zake.
Baada ya kampuni kutangaza kuuza hisa, watu wananunua kwa thamani
halisi, lakini baadaye zinauzwa katika soko la hisa ambako thamani ya
hisa inabadilika kuendana na hali ya soko.
Tukiangalia upande wa kampuni, mpaka Agosti, mwaka huu kulikuwa na zaidi
ya kampuni 16 zilizosajiliwa katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).
Kampuni 11 ni za kizalendo na kampuni sita ni za nje.
Kwa mujibu wa Emilian (2010), asilimia 0.39 tu ya Watanzania wamewekeza
kwenye soko la hisa. Kutokana na tatizo hilo, bado ni tatizo kubwa kwa
Watanzania na kwa jicho la pili ni fursa kubwa kwa wajasiriamali,
wafanyakazi na wanafunzi kuwekeza katika hisa.
Uwekezaji katika hisa unachangamoto zake ikiwzmo kushuka kwa bei ya
hisa, kukosa gawio, mfumuko wa bei, viwango vya riba, kukosa wanunuzi
kutokana na ukwasi na hitilafu mbalimbali.
Kwa hali ya kawaida uwekezaji katika hisa una faida nyingi kuliko
changamoto kwa mfano, kupata gawio baada ya kampuni kutengeneza faida,
ongezeko la thamani ya hisa, punguzo la kodi ya zuio kwenye gawio.
Katika masuala ya hisa, hakuna kodi kwenye ongezeko la thamani, urahisi
wa kuuza na kununua hisa, na ukiwekeza katika hisa unapata muda wa
kufanya shughuli nyingine. Kwa upande mwingine hisa ni dhamana ya kupata
mkopo, hisa ni urithi mzuri, ukijiwekea utaratibu wa kutenga asilimia
fulani ya pato lako kutoka kwenye mshahara ama biashara kwa ajili ya
kununua hisa ni uamuzi mzuri, na hisa pia ni utajiri.
Unapowekeza katika hisa jihadhari na makosa yafuatayo; kununua au kuuza
hisa zako bila utafiti, kutokujua tofauti ya thamani ya bei, kununua kwa
kuangalia jina na umaarufu wa kampuni, kutokua na malengo maalum,
kununua kwa kuwa bei ni rahisi, kukosa maarifa au kutozingatia elimu ya
fedha, hisa na uwekezaji, na kuwekeza fedha nyingi kwenye kampuni moja.
source: http://www.jamiiforums.com/business-and-economic-forum/375940-jifunze-faida-na-mbinu-za-kununua-hisa.html
Categories: