Wengi Wetu tunaishi katika mazingira ambayo yanaathiri sana amani yetu ya moyoni. Yamkini tunaonekana tunafuraha, tunacheka tunahusiana vema na wanaotuzunguka lakini ukweli ni kwamba ndani yetu hatuko sawa.  Wengi tunawaona wana maisha mazuri sana kwa jinsi ya nje,  wana majumba mazuri ya kuishi, wana magari mazuri ya kutembelea, watoto wazuri na kazi nzuri pia na tukiwaangalia tunadhani wanafuraha sana ndani yao lakini nimepata bahati ya kuzungumza na wengi wa aina hii na kugundua  kuwa hawakuwa na furaha ya maisha yao kama wengine walivyofikiri.  Viko vitu vingi vinavyoweza kuiathiri amani ya moyoni mwako, kwa mfano; hali mbaya ya mahusiano baina yako na umpendaye, matatizo ya tabia za watoto wako, matatizo ya kazini kwako, kushindwa kufikia malengo binafsi, historia yako binafsi, maumivu ya moyo, mambo ya ndugu na mengine mengi.

Dhumuni langu katika makala hii ni kujaribu kuzibua kanuni chache za kusaidia kuishulikia hali hii ili uweze kupona  katika tatizo  hili.
1.     Jitahidi kutokuingilia mambo ya wengine, labda tu uruhusiwe na mhusika
Wengi tumejikuta katika matatizo sababu tu ya kuingilia mambo yasiyokuwa yetu, tunafanya hivyo sababu mara nyingine  tunafikiri tunavyojua sisi ndio sawa, na  mtazamo wetu ndio ukosahihi zaidi, na yeyote asiyeafikiana na mtazamo wetu anastahili kupingwa.  Lazima tutambue kwamba Mungu amemuumba kila mmoja wetu tofauti.  Hakuna watu wawili watakao waza au kutenda sawa sawa.  Jali yaliyo yako kwanza na utailinda amani ya moyo wako (mind your own business).

2.     Jifunze kusamehe na kusahau
Hii ni nguzo na msaada mkubwa katika kutafuta amani ya moyoni.  Mara nyingi tunaweka hisia za maumivu moyoni dhidi ya mtu aliyetuumiza au kutuudhi, taratibu tunaumba na kulea chuki kali moyoni.  Matokeo yake wengine wanakosa usingizi, wanapata vidonda vya tumbo, wengine shinikizo la damu (BP) n.k.  Chuki au maumivu  haya ya moyo yalifanywa mara moja, lakini matokeo yake yanaeendelea kuharibu maisha na afya kwa muda mrefu kwa sababu tu ya wewe kuikumbuka chuki au uchungu.  Achana na tabia hii mbaya.  Maisha ni mafupi sana hustahili kuyaweka katika matatizo yote haya.  Samehe, sahau na tembea mbele.  Upendo wakati wote huchanua katika tendo la kutoa  na kusamehe (love flourishes  in giving and forgiving )

3.     Kamwe usijitutumue kutafuta umaarufu, kujulikana au kutambulika
Fahamu kuwa ulimwengu huu una wabinafsi wengi sana, mara chache  watakusifia pasipo kuwa na wivu.  Wanaweza kukusifia leo kwa sababu unanafasi au uwezo fulani, lakini subiri utakaposhuka chini.  Watasahau kabisa yote mema uliyofanya na kuanza kutafuta kila chafu na ovu ulilotenda, hata kama lilitendeka mafichoni.  Kwa nini unataka kujiua ukitafuta kutambulika na kukubalika.  Kwamwe kukubali kwao hakulingani na kero zao.  Kero zao zinazidi sana. Jitahidi kufanya majukumu yako kwa nidhamu ya hali ya juu na moyo wote, ukimwogopa na kumheshimu Mungu na sio mwanadamu.
4.     Usiwe na Wivu
Wote tunajua jinsi wivu unavyoweza kusumbua amani yetu ya moyoni.  Unajua kabisa kuwa unafanyakazi zaidi ya wenzako ofisini lakini wao wanapata kupandishwa cheo au faida zingine za kikazi  na sio wewe.

Wewe umeanza biashara miaka  tele iliyopita, lakini haujafanikiwa kama jirani yako ambaye ana mwaka tu katika biashara.  Iko mifano tele kama hii katika maisha ya kila siku.  Je ndio inakufanya uwe na wivu?  Hapana,  kumbuka kuwa kila maisha ya mtu hutegemezwa na mustakabali wake utakavyokuwa, ambao ndivyo unavyompeleka yeye hivyo alivyo.  Kama umepangiwa kufikia hatua fulani hakuna atakayeweza kusimamisha.  Kama hujapangiwa hivyo, hakuna atakayeweza kukusaidia kufikia pale pasipo pako. Hakuna utakachokipata kwa kulaumu wengine kwa bahati zako mbaya.  Wivu hautokupeleka kokote, zaidi utakuondolea amani moyoni mwako.
5.     Jifunze kubadilika kutokana na mazingira
Kama  unadhani utaweza kushindana na mazingira na kuyabadilisha, kuna  uwezekano mkubwa kuwa utafeli.  Badala yake jifunze kubadilika wewe kwanza ili kuendana na mazingira yanayokuzunguka, ambayo unadhani yako kinyume na matakwa yako.  Kwa kufanya hivi hata mazingira yaliyoonekana kuwa magumu taratibu yatabadilika na kuwa ya kuridhisha.
6.     Jitahidi kustahimili vile visivyoweza kubadilika (Endure what cannot be cured)
Hii ni njia bora yakugeuza bahati mbaya kuwa bahati nzuri.  Kila siku tunakutana na matatizo, balaa, magonjwa, hofu na hata ajali ambazo ni zaidi ya uwezo wetu.  Kama hatuwezi kufanya chochote dhidi ya mambo haya magumu wala hatuwezi kuyabadilisha basi ni vema tujifunze kustahimili, kukubali na kuchukuliana na hali tukiwa bado wenye tumaini.  Jiamini wakati wote unapoyapitia haya na utaona mbegu ya ujasiri na uvumilivu inaota ndani yako na taratibu nguvu ya kuendelea mbele itaibuka.
7.     Kamwe using’ate zaidi ya unavyoweza kutafuna
Mara zote kumbuka wazo hili,  maranyingi katika maisha haya yenye mahangaiko tele na kiu ya kufikia malengo makubwa wengi wetu tumejikuta tunachukua majukumu mengi kuliko uwezo wetu wa kuyatekeleza.  Maranyingine tunafanya hivi kwakuzifurahisha nafsi zetu tu.  Fahamu ukomo wa uwezo wako, kwanini uchukue mzigo ambao utakuzidishia matatizo?  Hutoweza kupata amani  moyoni kwa kuongeza mipaka ya majukumu  yako ambayo yanakuzidi.  Punguza majukumu na tumia muda mwingi utakaoupata katika kutafakari jinsi gani utaboresha yale machache unayoyafanya.  Tumia pia muda wako kwa kuongeza ubora wa mahusiano yako na wale wanaokuzunguka kuanzia familia, marafiki na kwa jinsi hii lazima utahisi  amani tele moyoni na nafsini mwako.
8.     Pata muda wa kutafakari mara kwa mara
Kutafakari hutuliza akili nafsi  na kupunguza au kupooza mawazo masumbufu.  Hii ni  aina ya juu zaidi ya kutafuta amani ya moyoni na nafsi.  Imechunguzwa kwamba kama utaweza kutumia angalau lisaa kutafakari kila siku basi utaweza kuendelea kuwa na amani nafsini na moyoni katika masaa mengine yote yaliyobaki katika siku hiyo.  Nafsi na  moyo wako havitaweza kusumbuliwa kwa urahisi tena kama ilivyokuwa awali.  Taratibu utaongeza muda wako wa kutafakari, na matokeo yatabadilika zaidi pia.  Najua unaweza kuwaza kuhusu muda unaopotea hapo, lakini kinyume chake hii itaongeza ufanisi na kuboresha matokeo ya kila utakacho kifanya, tena katika muda mfupi.
9.     Kamwe usiiache nafsi yako pweke
Kuna msemo wa kiingereza unaosema “An Idle mind is the devil’s wadshop”, ukimaanisha  kuwa nafsi iliyoachwa pweke pasipo chakufanya wala chakufikiri ndio karakana ya ibilisi ya kufanya mambo machafu. Wakati wote iweke nafsi na moyo wako katika kuwaza yaliyobora, yanayojenga na yakimaendeleo.  Amua kuyawaza yale unayoyathamini.  Je unathamini pesa zaidi ya amani ya nafsini mwako?  Vitu kama  kazi za kijamii, kujitolea, Ibada, unavithamini kwa kiasi gani?  Yamkini vinaweza visiwe na uthamani wa kifedha  lakini vinaweza kukupa utoshelevu wa moyoni kwa kiasi kikubwa. Hata kama umepumzika, iruhusu nafsi , moyo na akili yako kufanya vitu vya kiafya kama vile kusoma mambo mazuri, kubadilishana mawazo, nk.
10.                        Usipende kujiweka njia panda na usiruhusu majuto
Utapoteza muda mrefu, masaa, siku wiki na hata miaka kama kila siku unajiuliza “sijui nifanye nini kati ya haya? Usijiingize katika mijadala isiyo na mwisho ya nini kifanyike.  Najua ni vema kuwa na malengo, lakini hatuwezi kupanga kwa kikamilifu kwa asilimia 100, maana hatuwezi kutabiri yaliyombele yetu.  Thamini muda wako na tenda yale mambo ambayo yanaumuhimu na uwezo wa kufanyika.

Haijalishi kama utashindwa mara ya kwanza, bado utaweza kujifunza kutokana na kushindwa huko ili ufanikiwe siku nyingine.  Kukaa na kuanza kufikiria kule kushindwa kwako hakutokusaidia chochote.  Jifunze kutokana na makosa yako ila using’ang’ane  na makosa yako ya awali. Jifunze  kutokujuta ovyo, yamkini kilichotokea kilipangwa kitokee vile kilivyotokea kwa makusudi fulani, yanini kulilia maziwa yaliyokwisha kumwagika?

Kuna maandishi niliyasoma katika kitabu fulani yakielekeza namna ya maneno ya kukusaidia kupata amani ya moyo kila siku, wewe pia waweza kuyatumia maneno haya na yatakusaidia.

Mungu nisaidie kuweza kuleta mabadiliko
katika yale ambayo nina uwezo wa kuyabadilisha.
Ni saidie kuweza kuyakubali yale nisiyoweza kuyabadilisha,
na kuifahamu tofauti iliyopo baina ya haya mawili.

Categories:

Leave a Reply