Posted by Unknown on
-
WATU
wengi huhangaika sana kujua kama wanaifurahisha jamii au wanaiudhi.
Wengine wamefikia hatua ya kujiuliza, wamewakosea nini watu
wanaowazunguka mpaka wakajikuta wamechukiwa? Kisaikolojia fikra za
namna hii, ni sawa na kutafuta gari kwenye mwanga kwa njia ya kupapasa!
“Nashanga mama mdogo ananichukia bure, tena hakuna kosa nililomfanyia
lakini hanipendi tu.” Je, wewe nawe umekuwa miongoni mwa watu wanaodhani
unachukiwa bure?
Achana na hulka hiyo, hebu tambua ubaya wako
kwa kuangalia vidokezo vifuatavyo, ambavyo naamini ukivisoma kwa umakini
utagundua ni wapi unakosea hadi kufikia hatua ya kuchukiwa katika
jamii.
Je, inapotokea umesababisha wenzako wajisikie vibaya huwa
unajisikiaje moyoni mwako? Mfano ulikuwa katika mazungumzo ya kawaida na
rafiki yako, lakini kwa sababu za kibinadamu akapokea mazungumzo yako
vibaya na kufadhaika. Wewe unapotambua kuwa umemuondolea mwenzako furaha
huwa unajisikiaje moyoni? Kama huumizwi na tukio hilo tambua kuwa wewe
ni mtu mbaya.
Jiulize, katika maisha yako ni mara ngapi umewafanya
wengine wafurahi kwa kuwatatulia matatizo yao, kuwasaidia katika shida
na kuwavusha katika hali ngumu za kimaisha? Au umekuwa mtu wa kusubiri
usaidiwe wewe hata kwa vitu unavyoweza kuwasaidia wenzako?
Tangu umeanza kazi umeshawahi kutoa sehemu ya mshahara/pato lako
kuwasaidia wazazi na ndugu zako au umekuwa mtu wa kutoa visingizio vya
hali ngumu ya maisha licha ya kuwa unafanya anasa mjini? Ikiwa hujawahi
kuwasaidia watu kupata furaha, fahamu kuwa unaishi na ubaya kwenye
jamii, jiandae kuchukiwa.
Je, unaposikia wenzako wana shida huwa
unazichukuliaje?, je ni sehemu ya tatizo lako au hujiweka pembeni na
kuwaachia binadamu wenzako wamalize matatizo yao? Ukiwa hivyo hicho ni
kipimo kikubwa cha ubaya wako kwenye jamii unayoishi.
Umekuwa
ukitumiaje uwezo wako wa mali au hata nguvu za mwili mbele ya wenzako?
Je, ni kwa kuonea na kuwakandamiza watu uliowazidi? Ikiwa una tabia
hiyo anza kujihesabu kuanzia leo kwamba wewe ni mtu mbaya mbele ya
jamii.
Angalia mazungumzo yako, je yamekuwa ni ya kuwatia moyo watu,
kuwafariji na kuwaelimisha au umekuwa mtu wa kutoa matamshi ya
kudhalilisha, kuudhi na kuwavunjia heshima wenzako? Kama ulimi wako
unatoa maneno yenye ‘sumu’ usitegemee kupendwa.
Je, umekuwa mtu
wa haki, mwenye kuwatanguliza wenzako? Unaweza kutoa unachokitegemea
ili kumsaidia binadamu mwenzio? Ukiwa huwezi kufanya hivyo na umekuwa
mtu wa kukumbatia mali zako ujue wewe ni mbaya.
Toka ndani ya moyo
wako unafurahia jamii kuwa na umoja au umekuwa mtu unayechochea
migawanyiko baina ya watu wanaopendana? Endapo una tabia kama hiyo
fahamu kuwa matendo yako ni mabaya.
Ni mara ngapi umezuia hasira
zako kwa lengo la kuepusha migogoro? Unaweza kuvumilia kuonewa au
umekuwa mtu wa kulipa kisasi kwa kudhamiria kufanya mambo mabaya kwa
makusudi licha ya moyo wako kukuonya mara nyingi usifanye hivyo? Kama
una tabia hiyo tambua kuwa huo ndiyo ubaya wako kwenye jamii, chukua
hatua za kujisahihisha wewe kwanza kabla ya kuwanyooshea wenzako kidole!
Categories:
Vzuri inapendeza