Na: Meshack Maganga-Iringa.

Moja ya mambo yanayoweza kujenga mfumo rasmi wa uendeshaji wa biashara ni kusajili biashara zinazoendeshwa katika mfumo wa kampuni. Kwa wajasiriamali wengi, neno kampuni linaposikika huwa linatafsiriwa tofauti na mantiki yake.

Wengi hudhani kampuni hazianzishwi na wajasiriamali wa kawaida, wengine hufika hatua ya kudhani kuwa makampuni ni ‘madude’ makubwa yenye mamia ya wafanyakazi, rundo la majengo na hata mabilioni ya fedha. Kibaya zaidi wapo wanaodhani kuwa kuanzisha kampuni inahitajika mjasiriamali awe na elimu kubwa.

Kinyume na mitazamo ya wajasiriamali wengi nchini Tanzania, kampuni ni mfumo rasmi na wa kisheria wa kuendesha biashara ambapo, uwepo wa biashara unatofautishwa na mmiliki wa biashara. Katika mfumo wa makampuni, kampuni iliyosajiliwa inasimama kama mtu anaejitegemea kisheria. Kuna makampuni madogo na makubwa. Unaruhusiwa kisheria kusajili kampuni kwa kiwango chochote cha mtaji hata kuanzia shilingi laki moja na tena huhitaji kuwa na elimu ya chuo kikuu au uwe umesomea ujasiriamali kwenye vyuo vikuu unavyovifaham au kuvisikia ili kumudu uendeshaji wa kampuni yako.

Kwa mfano, mjasiriamali anapotaka kuongeza mtaji katika biashara yake, ikiwa biashara yake imesajiliwa kama kampuni, basi anaekwenda kukopa ni kampuni yenyewe na sio yule mjasiriamali. Hii ina maana kuwa, wakati wa kudai mkopo huo anaedaiwa ni kampuni na sio mmiliki wa kampuni. Kwa namna nyingine ni kuwa, ikitokea kampuni imeshindwa kulipa mkopo, basi benki itataifisha mali za kampuni pekee, bila kuingilia mali binafsi za mmiliki wa kampuni husika.

Mjasiriamali anapokuwa amesajili rasmi (kampuni) biashara zake, analazimika kuwa na mfumo rasmi wa kiutawala pamoja na utunzaji wa kumbukumbu za kimahesabu. Kunapokuwepo na kampuni hailazimiki mmiliki wa kampuni awepo ili biashara ziende. Hii ni faida tofauti na ilivyo kwa wafanyabiashara binafsi (sole proprietor) ambapo wao ni biashara na biashara ni wao. Wao wakifa na biashara zinawafuta nyuma yao makaburini. Lakini mmiliki wa kampuni akifa, kampuni inaendelea kuishi kwa kuwa yenyewe ni mtu kamili kisheria (legal person).

Biashara bila kuwa na mfumo rasmi wa uendeshaji ninaweza kuufananisha na ile hulka ya ndege aina ya mbuni ya kujificha mchangani. Mbuni kwa kawaida huwa ana asili ya kuficha kichwa chake mchangani pindi aonapo hatari ama anapotaka kuwa salama katika eneo lolote lile.

Biashara ambazo hazijitenganishi na wamiliki usalama wake ni mdogo, ukuaji wake ni wa kusuasua na urefu wa uhai wake daima huwa mashakani.  Mjasiriamali anapofikia uamuzi wa kuanzisha kampuni kuna hatua chache tu za kufuata. Kwanza anatakiwa kuandaa nyaraka za kampuni, ambazo zinaeleza muundo na mfumo wa kampuni inayokusudiwa. Nayaraka hizi zinajulikana kama, ‘Article of Association’ inaelezea muundo wa ndani wa kampuni wakati nyaraka nyingine ni ‘Memorundum of Association’ hii ikiwa inaeleza uwezo na mipaka itakayokuwa nayo kampuni inayokwenda kuundwa.

Mbali na nayaraka hizo, zipo fomu nyingine zinazotakiwa kujazwa ili kukamilisha masharti ya kusajiliwa kwa kampuni. Kwa kuwa suala la uandaaji wa nyaraka hizi lipo kitaalamu zaidi (taaluma ya biashara na sheria), mjasiriamali anaweza kuwasiliana na wataalamu wa masula ya biashara na kisheria ambao wataifanya kazi hii kwa haraka na kwa gharama ndogo.

Gharama ya kuwasilisha fomu na nyaraka hizo, kwa wakala wa usajili wa leseni na biashara (BRELA) haizidi shilingi elfu sabini. Kwa mfano, kwa kampuni ambayo inakusudia kuanza na mtaji wa shilingi milioni mbili, jumla ya gharama za kuwasilisha fomu, nyaraka pamoja na ada haizidi shilingi laki mbili na nusu (ukiacha gharama ya kuandaa nyaraka za kampuni kwa sababu hiyo itategemea na wataalamu walioziandaa).

Kingine cha kufahamu kuhusu uzuri wa kuanzisha na kumiliki biashara katika mfumo wa makampuni ni katika maeneo ya upatikanaji wa mikopo pamoja na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Kikawaida mabenki na taasisi za fedha zinaamini sana makampuni, ikifuatiwa na ushirika (partnership) na wa mwisho kabisa kuaminiwa ni wafanyabiashara binafsi (bila kujali ni mtaji mkubwa kiasi gani unamiliki).

Kwa upande wa uchumi wetu, usajili wa biashara katika mifumo rasmi inasaidia uwepo wa kumbukumbu rasmi kuhusu mienendo ya mibadilishano ya fedha na kiasi cha mitaji inayozunguka. Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 95 ya uchumi wa Tanzania, sio rasmi. Hii ni kusema kuwa hata takwimu za umasikini wa nchi hii, ‘zinapikwa’ kwa sababu si njia zote za uzalishaji mali zimejumuishwa kutokana na kutokuwa rasmi (informal economic sector).

Vile vile usajili wa majina na biashara unatoa haki miliki ya jina lako kutotumiwa na wengine. Kwa mfano, ukisajili kampuni kwa jina la Kyuta Enterprises & Company Limited, inakuwa ni kinyume na sheria kwa mtu ama biashara nyingine kulitumia jina hilo pasipo ruhusa ya wewe mmiliki. Hii inalinda wizi dhidi ya nembo (brands), matumizi mabaya ya kibiashara (business piracy) pamoja na haki-miliki ya kimatangazo

Japokuwa zipo changamoto na faida nyingi katika kuendesha biashara katika mifumo rasmi, itoshe tu kwa leo niseme kuwa ili ufurahie ufanyabiashara wako ni vema ukamiliki biashara katika mfumo rasmi. Kwa kadiri tupatavyo nafasi nitakuwa nikichambua mambo haya muhimu katika nyanja ya ujasiriamali, fedha na biashara.

Ushindi ni kwa kila mtanzania.Tukutane jumatano ijayo. Maoni na ushauri barua pepe yangu ni  hii

meshackmaganga@gmail.com  

Categories:

Leave a Reply