USHAURI umetolewa kwa Tanzania na Watanzania kuamka na kuchangamkia fursa za uwekezaji na biashara ambazo zimejitokeza nchini Sudani ya Kusini.

Ushauri huo ulitolewa Siku ya Jumatano na Meja Jenerali Wynjones Kisamba ambaye ni Naibu Kamanda wa vikosi vya kulinda amani katika jimbo la Darfur maarufu kama UNAMID, wakati alipokutana na kubadilishana mawazo na Maofisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York. Meja Jenerali Kisamba yuko hapa Umoja wa Mataifa, kwa ziara ya kikazi na mafunzo ya maOfisa wa ngazi za juu katika misheni za Umoja wa Mataifa, mafunzo ambayo yameandaliwa na Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa (DPKO). “ Tanzania tuna kila sababu ya kuwekeza nchini Sudani ya Kusini, zipo fursa nyingi mno kuanzia upelekaji wa chakula hadi ujenzi. Nilikuwa nyumbani hivi karibuni, nimekutana na viongozi mbalimbali na kuwaelezea juu ya fursa hizi”, alisema. Alisema ana wasiwasi kwani Watanzania wanachelewa kwani majirani wa Tanzania wamekwisha zichangamkia fursa hizo na wako mbali na kwamba ni kama wameishaingia mpaka jikoni. Aidha katika mazungumzo yake na maofisa wa ubalozi, Naibu Kamanda wa vikozi vya UNAMID alibainisha kwamba kama kweli Serikali, kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi zikiamua kuingia kibiashara Sudani ya Kusini hakuna tutakachopoteza. “Sudani ya Kusini ndio kwanza wanaanza kuijenga nchi yao, wanachangamoto nyingi, sisi tunaweza kuwasaidia kwa maana ya kuwekeza na kwa kufanya biashara. Kwa mfano wale wanakula sana chapati, hawana ngano, tunaweza kuwauzia ngano, wanahitaji mafuta ya kupikia tunayo alizeti, wanahitaji vifaa vya ujenzi, tuna viwanda vya saruji na nondo pia, kwa kweli fursa zipo tunachotakiwa ni kujipanga. ‘Watanzania changamkieni biashara Sudani Kusini’ source:Mzizi mkavu jf member

Categories:

Leave a Reply