TATIZO la ununuzi wa kahawa mbivu Red Cherry limeendelea kushika kasi wilayani Mbozi huku baadhi ya wakulima wakilalamika kuibiwa kahawa yao ikiwa shambani na watu wasiofahamika.
Taarifa kutoka kwa baadhi ya wakulima katika vijiji vya Hatelele, Isansa, Itaka,Igamba, Bara na Mtunduru zinadai kuwa kutokana na wakulima kutokubali kuwauzia wachuuzi kahawa mbivu hivi sasa kuna kundi la watu wanaovamia mashamba nyakati za usiku na kuvuna kahawa hiyo.
Imedaiwa kuwa kahawa hiyo huvuna na kuiuzia kampuni mmoja iliyopewa leseni ya kununua kahawa mbivu huku serikali ya wilaya na Mkoa vikipinga kuwepo kwa ununuzi wa kahawa hiyo kwa kuwa unamnyonya mkulima.
‘’Ununuzi wa kahawa mbivu unasababisha mkulima apate hasara, mkulima anayeuza kahawa kavu hupata faida kubwa kuliko yule anayeuza kahawa mbivu, huyu anamnufaisha mnunuzi, tunapinga vikali ununuzi wa kahawa mbivu,’’anasema Bw. Adam Kalonge mkulima wa Kahawa katika kijiji cha Hatelele.
Sakata hili la ununuzi wa kahawa mbivu limekuwa ni mwiba mchungu kwa viongozi wa serikali ya wilaya ya Mbeya na mkoa huku taarifa hizo zikijikanganya baada ya baadhi ya viongozi wa wizara kudaiwa kukubali ununuzi wa kahawa mbivu kutokana na maslahi binafsi.
Katika kikao cha Bunge kinachoendelea, Mbunge wa jimbo la Mbozi Mashariki Bw. Godfery Zambi alimnyooshea kidole aliyekuwa Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe kwamba anahusika moja kwa moja katika kuidhinisha ununuzi wa kahawa mbivu kwa baadhi ya makampuni ilhali anajua wazi kuwa kitendo hicho ni kumdhulumu Mkulima.
Profesa Maghembe aliwahi kukutana na wadau wa kahawa mkoani Mbeya katika kikao kilichoketi wilayani Mbozi ambapo wakulima walitoa msimamo wao wa kupinga kutolewa kwa leseni ya ununuzi wa kahawa mbivu ambapo katika kikao hicho, Profesa Maghembe alishutumiwa na wakulima na viongozi wa chama cha Mapinduzi kuhusika moja kwa moja na tatizo hilo
soirce: http://mkwinda.blogspot.com/2012/07/wakulima-waibiwa-kahawa-shambanini.html
No comments:
Post a Comment