Gavana wa Benki kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu, amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa asilimia 6.4 kwa mwaka 2011 zaidi ya ilivyokadiriwa kuwa ungekua kwa asilimia 6 kwa mwaka.

Alisema ukuaji huu ni mkubwa hasa katika sekta ya usafirishaji na mawasiliano kwa asilimia 11.3 ikifuatiwa na masuala ya fedha kwa asilimia 10.7, ujenzi kwa aslimia 9.0, biashara kwa asilimia 8.1 na uzalishaji wa asilimia 7.8.

Akitoa mada katika mafunzo elekezi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya inayofanyika mjini Dodoma, Profesa Ndullu alisema mpaka hivi sasa Tanzania bado inakopesheka kinyume na taarifa mbali mbali zisizo rasmi zinazotolewa.

Profesa Ndulu alisema kilimo bado kinaongoza katika kuliingizia Taifa mapato kikifuatiwa na biashara uzalishaji na ujenzi.
Aidha, aliishauri Hifadhi ya Taifa ya Chakula (National Grain Reserve) kuanza kuwa na mkakati wa kuhifadhi mpunga badala ya mahindi pekee kwani

itasaidia kupunguza mfumuko wa bei kwa kuwa mchele ni moja ya nafaka inayotumiwa sana na kaya mbalimbali.

Profesa Ndullu alisema kwa ujumla kushuka kwa thamani ya fedha kumepungua kutoka asilimia 19.7 hadi kufikia 19.0 katika mwaka 2002.
Alieleza kuwa kushuka kwa thamani ya fedha ilitokana na kushuka kwa bei ya bidhaa hasa katika eneo la nishati na mafuta.

Alisema hadi kufikia hivi sasa asilimia 75 ya Watanzania wanategemea kilimo, hivyo ili Tanzania iweze kupiga hatua katika maendeleo, kilimo kimetakiwa kutiliwa mkazo mkubwa.

Naye Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Tume ya Mipango Dk Phillip Mpango, aliwataka viongozi kuongoza kwa mifano na kuondokana na suala la kuongoza kwa nadharia ili kujua changamoto zinazowapata wale wanaowaongoza.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Categories:

Leave a Reply