JINSI jamii inavyokuwa na mfumo wa aina fulani kuna uwezekano wa kujenga mizizi inayosababisha mikwaruzano mbalimbali.
Ni vema kuelewa kuwa jamii yoyote ina mfumo wake, hivyo kuwa na baadhi ya watu wanaojikuta hawatendewi haki kama wengine, hali inayochangia kuwapo kwa migongano, mikwaruzo au kutokuelewana.
Hali hiyo hutokea hasa pale kiongozi wa mtaa, wilaya, nchi, eneo, kazi au katika shughuli yoyote inayowashirikisha watu wengi anaposhindwa kuwawakilisha wote kwa usawa.
Kumbuka kuwa kila mwanadamu ana mahitaji muhimu, kwani kila mmoja hupenda kuwa salama na kutambulika. Ikiwa mahitaji yake hayafikii malengo, husababisha maamuzi mabovu kutolewa, amani kutoweka na kutokuelewana.
Tunaweza kuona vyanzo mbalimbali vinavyosababisha migongano katika jamii tunamoishi. Zinaweza kuwa za kisiasa au kijamii. Tunaona kuwa mara nyingi kutokuelewana hutokea pale watu wanapokosa kuelewana katika jambo linalofanana. Endapo kunakosekana usawa katika mojawapo ya mambo, kwa mfano, utofauti wa kipato unaosababisha mifarakano kutokana na rasilimali za nchi kama vile ardhi na maji.
Pia tunaona hali ya kutokuelewana huibuka pale watu wanapokuwa hawana furaha kutokana na watawala wanaowaongoza.
Mara nyingi tumeshuhudia kuwa migongano ya mara kwa mara hutokea wakati kikundi fulani kinapotaka kuwa huru kutokana na utawala uliopo madarakani, madai yao inaposhindwa kuwasilishwa serikalini, serikali inapowadharau na kutowaheshimu au kukutana na mahitaji yao ya muhimu.
Migongano mingine inatokea kuhusu masuala ya dini na siasa. Wakati mwingine husababishwa na kikundi cha dini au siasa kilichohujumiwa. Hata hivyo, migongano yoyote inaibuka wakati watu wanapoumizwa.
Ingawa mara nyingi migongano hiyo huonekana ni kinyume, inaweza kufikiwa muafaka kama utatuzi utapatikana. Pia katika maeneo ya kazi mara nyingi kumekuwa na mifarakano ya mahitaji. Wafanyakazi wanapozidiana katika rasilimali na kutambuliwa kazini, migongano hutokea.
Kwa mfano, utakuta kuwa mkuu wa idara amekuwa akiwapendelea baadhi ya wafanyakazi kwa kuwapa motisha zaidi, hali inayowavunja moyo wafanyakazi wengine na kusababisha migongano.
Pia ufahari au jinsi ya kuishi na watu maeneo ya kazi huleta kutokuelewana kama tu hutajishusha na kuishi maisha ya kawaida katika jamii inayotuzunguka.
Kumbuka kila mtu ana tabia zake binafsi, kunakuwa na tofauti katika kuwafikia watu na matatizo yao. Kama kiongozi jihusishe nao kuelewa mitindo yao ya maisha na jifunze jinsi ya kuepuka migongano inayoweza kusababishwa na hali hiyo.
Kwa mfano, itakapotokea mfanyakazi mmoja anapofanya kazi katika mazingira bora na mazuri wakati mfanyakazi mwingine anafanya kazi katika mazingira yasiyoridhisha, wafanyakazi hao wawili ni rahisi kukorofishana na kutokuelewana, kwa vile mmoja wao ataona kuwa hatendewi haki kwa hilo.
Matatizo mengine huchangiwa pale mtu asipoweza kufikia lengo alilokusudia kutokana na kutowezeshwa na mwajiri wake - kwa upande wa vitendea kazi, hali inayochangia kuchelewa kutekeleza majukumu yake.
Wakati mwingine mwajiri anaweza kukulaumu mara kwa mara kutokana na uzembe wa kampuni hiyo kwa kutoona umuhimu wa kuwa na vitendea kazi vya kutosha, au wakati mwingine idara mojawapo hupewa vitendea kazi na nyingine kukosa. Hiyo huleta hali ya mvutano na kutokuelewana katika maeneo ya kazi.
Shinikizo kutoka kwa viongozi wa kazi huchangia migongano. Kwa kuwa inaweza kutokea watu wawili au zaidi katika kitengo kimoja wanapokuwa na majukumu tofauti yanayotakiwa na bosi wao kwa wakati mmoja.
Kwa mfano, kiongozi wa kazi anapotaka taarifa kamili ikamilike saa tisa alasiri - muda anaotakiwa mfanyakazi mwingine kukamilisha taarifa yake - ambapo wote kwa pamoja wanahitaji kutumia mashine moja kwa kuwa mashine nyingine ni mbovu, kipi ni suluhu? Matokeo yake mgongano unatokea.
Migongano mingine husababishwa na hali ya upendeleo kwa baadhi ya wafanyakazi. Utakuta bosi bila uficho wowote anaonyesha hali ya kuwathamini baadhi ya wafanyakazi na kuwadharau wengine.
Ubaguzi katika maeneo ya kazi unasababisha minong’ono, tuhuma, na hatimaye migongano. Hivyo ili kuondoa hali hiyo, kiongozi mkuu wa kampuni anatakiwa kuwa thabiti katika kuhakikisha kampuni yake haiwi na mgawanyiko wowote na kuwafanya wafanyakazi wake wafanye kazi zao kama timu moja imara.
Mingine husababishwa na sera mpya ambazo hazikutarajiwa.
Popote sera za kampuni zinapobadilika, kutokuelewana kunatokea, wafanyakazi wanahitaji kufahamishwa sheria na sera za kampuni, pale mabadiliko mapya yanapotokea hawatakiwi kubahatisha. Vinginevyo vitu visivyotarajiwa vitatokea kama kupeana taarifa potofu.
Njia mbalimbali zinazoweza kumsaidia mkurugenzi wa kampuni, mkuu wa idara au yeyote mwenye dhamana ya kuwaongoza wenzake, jinsi ya kutatua migogoro katika maeneo ya kazi.
Ni vizuri ukatambua kuwa baadhi ya migogoro hatima yake hujenga mahusiano bora zaidi tofauti na ilivyokuwa mwanzo endapo itatatuliwa kwa umakini.
Ukumbuke kuwa migongano katika sehemu za kazi ni sehemu ya maisha na haiepukiki, lakini ni jinsi gani tunaishughulikia inapotokea kama bosi bila kuathiri biashara na shughuli za uzalishaji katika kampuni yako. Kama viongozi kunakuwepo na majukumu imara ya kusuluhisha migogoro kwa haraka.
Viongozi wa kisasa hawaatakiwi kuwa ‘wanyapara’, bali wawe viongozi wanaodhihirisha fani zao, heshima na usawa katika mazingira yoyote na zaidi wanaposhughulikia migongano.
Kwanza yampasa kiongozi atathmini chanzo cha tatizo. Mafanikio ya kutatua tatizo la kutokuelewana kwa kikundi au jamii yanatokana na kuelewa chanzo halisi cha mgongano huo. Ni muhimu sana kuangalia mgogoro kutokana na mtazamo wa kila mmoja unaomhusu.
Kutokuelewa chanzo cha tatizo kutafanya utatuaji wa tatizo hilo kuchukua muda mrefu kutambua aliyehusika na sababu za kuhusika kwake, na sababu zinazofanya tatizo hilo kuwa gumu. Kutegemeana na hali ya tatizo lilivyo, unaweza kuzungumza ‘chemba’ na kila mmoja aliyehusika katika mgongano huo au unaweza kuzungumza nao wote kama kikundi. Kusikiliza ni silaha mojawapo muhimu itakayoweza kukusaidia na kulielewa tatizo.
Pia katika utatuaji wa tatizo unatakiwa kuwa makini na kujua kwa undani chanzo. Kuwa mkweli katika kulishughulikia tatizo. Sikiliza kwa umakini kukuwezesha kutoa mawazo yasiyopendelea upande wowote na kukuwezesha kutatua tatizo. Mruhusu kila mmoja kuwa mhusika katika hatua hizo na hakikisha uko wazi, mkweli na kutenda kwa usawa kama unavyozungumza na mtu binafsi. Usihukumu.
Ainisha njia bora zaidi ya kutatua matatizoMara unapokuwa na vielelezo vya uhakika mbele yako ni kazi yako kuongoza kikundi katika kufikia suluhu au kuainisha njia bora ya utatuzi. Mafanikio ya utatuzi wa matatizo mbalimbali mara zote inahusisha pande zote katika kutathmini tatizo na kipindi cha kutafuta utatuzi.
Muulize mtu binafsi kama anaweza kutoa mawazo ya jinsi ya kutatua tatizo. Unaweza kushangaa ni jinsi watu mara nyingi wanavyokuwa kamini kufikia mwafaka wa tatizo na kuwa na maamuzi yao binafsi.
Kama hawatakuwa na uwezo wa kufanya hivyo, unaweza kutumia njia bora ya kutatua tatizo. Malengo yako ni kuhakikisha unapatikana mwafaka wa usawa na utatuzi wa tatizo lililokuwepo ambalo litaleta utatuzi thabiti katika kampuni yako au kwa mtu binafsi.
Suluhisho
Wakati mwingine linapotokea tatizo, chukua muda na kujiuliza maswali yafuatayo:Nini kinachosababisha migongano katika kampuni yako? Kwa nini wewe au mwingine anahitaji vitendea kazi? Je, mtindo wa mfanyakazi fulani ni tofauti na mtindo wako uliouzowea?

Categories:

Leave a Reply