"Wanadamu wote walioweza kufanikiwa kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, wananjua ni nini wanakitaka na wanajua kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe katika hilo"


Maisha ya mafanikio duniani ni haki ya kila mwanadamu. Hakuna binadamu aliyeletwa duniani kuja kushuhudia wengine wakifanikiwa huku yeye akiwa katika umaskini siku zote. Kila mwanadamu mwenye pumzi anayo haki,nafasi, uwezo na uchaguzi wa kuwa anavyotaka kulingana na maana ya mafanikio atakayotengeneza na mwenyewe.

Ni kweli tunaishi katika dunia yenye utofauti kimafanikio wapo wenye mafanikio makubwa, wapo maskini na wale wenye maisha ya kawaida. Lakini kwa pamoja yatupasa tufahamu kuwa,  kila mwanadamu anao uwezo wa kufanikiwa , na zaidi ni kuwa  kila mtu anao uchaguzi wa kuamua maisha yake – lakini angalizo ni kuwa mtu yeyote aliyeweza kufanikiwa ametambua kuwa , kuna vichangizi vya mafanikio / success ingredients.
                          
Unachopaswa kutambua ni kuwa , hali ya maisha uliyonayo sasa si kipimo cha mafanikio yako ya baadaye,  unaweza kuwa vyovyote kimafanikio kulingana na utakavyochagua mwenyewe. Ni muhimu kuyajua maisha kwa kujua vichagizi vinavyoweza kutufanya tuishi maisha ya mafanikio na vichangizi hivyo ni kama ifuatavyo:
                           
1.      Fahamu Madhumuni au sababu ya kuwepo kwako: Mwanadamu anayejua dhumuni lake duniani huishi maisha ya maana. Hatukuja duniani kuwepo tu bali kuishi kimafanikio huku tukijua kwanini tunaishi. Ukijua ni kwanini unaishi hutakubali kuishi kiholelaholela huku ukisubiri muda wako wa kuishi duniani kuisha. Dhumuni la wewe kuwepo duniani ni kuishi maisha yenye madhumuni, maisha yenye mafanikio na maisha yanoyonufaisha wengine. Wanadamu wote walioweza kufanikiwa kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, wananjua ni nini wanakitaka na wanajua kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe katika hilo.Ukitaka kutengeneza maisha yenye mafanikio duniani, tafuta kujua dhumuni lako hapa duniani .

2.      Jiamini na amini kuwa unaweza: Wanadamu wote waliofanikiwa duniani waliamini kuwa wanaweza kuibadili dunia. Mwanadamu anayeyarudisha  maisha yako nyuma ni wewe mwenyewe, ukitaka kufanikiwa katika lolote utakalochagua jiamini na amini kuwa unaweza. Hakuna kitu chochote kilichowahi kutokea duniani bila kujiamini. Siyo kwamba hatuyawezi tunayoyapanga, bali hatujatambua kuwa chochote kile ambacho mwanadamu akiamua kukiamini kuwa anakiweza ,kitatokea na kinawezekana. Uwezo mkubwa wa mwanadamu haupo katika umbile lake bali katika kiwango cha kujiamini kuwa anaweza kuwa anavyotaka. Vyovyote vile unavyotaka kuwa jiamini unaweza kuwa hivyo na dunia itakubaliana na wewe kuwa unaweza.


3.     Tafuta unachokipenda na kifurahie.
Kila mwanadamu anayo zawadi ndani yake , zawadi hii huja kama  kitu anachokipenda na kukiweza. Ndani ya mwanadamu vipo vipawa na uwezo wa ajabu wa kuishi maisha ya mafanikio. Kila mtu ana kitu anachopenda, kinachoweza kutumika na kuendelezwa na kuleta mafanikio. Dunia ya sasa ni dunia ya wanadamu wanaojua ni kitu gani wanaweza. Wapo wanaopenda kuwa madaktari, wapo wanaopenda kuwa waimbaji nk. Kila mtu ana kitu anachopenda kinachomfanya acheke akiwa duniani. Tafuta kitu unachokipenda na kiendeleze , kitakuletea mafanikio.

4.      Kuwa mtendaji sana
Maisha ni vitendo na si ndoto pekee, ndoto ni mwanzo tu wa maisha. Maisha ni kuchukua hatua na si kufikiri pekee. Maisha ni kusonga mbele na si kupanga peke yake. Katika yote uliyochagua maishani kuwa mtendaji, usikubali kuyaishi maneno ishi matendo. Anza mahali ulipo kwa kile ulichonacho kwa kuwatumia watu ulionao na maisha yako yataanzia hapo. Zaidi jifunze kuishi vizuri na wanadamu, ukifanya hivyo utayafurahia maisha ya mafanikio.

5.     Kuwa na njaa ya kutafuta maarifa siku zote.
Maisha bila maarifa ni sawa na gari lisilo na mafuta. Ukitaka kutembea na kuishi kimafanikio kuwa na njaa ya maarifa kila siku. Binadamu wote wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta maarifa kwa kusoma vitabu, kuuliza na kujifunaza , na hata  kuhudhuria mafunzo ya kuwaendeleza mara kwa mara. Maisha bila maarifa hayatembei.


6.     Usikate tamaa.
Maisha yana mengi, muda mwingine yale tunayapanga hayaji kama tulivyopanga lakini yote hutokea kwasababu. Mambo yote tunayapitia katika maisha huwa ni hatua ya ukuajia kimaisha. Ukiona biashara yako inafanya vizuri tambua kuwa ni kweli biashara yako inakua, lakini ukiona biashara yako inafanya vibaya tambua kuwa uwezo wako unakua zaidi. Usikate tamaa katika kile ulichochagua, kabla hujakata tamaa jaribu tena. Maisha ni ya kwako usikubali kupoteza hitaji la moyo wako kwasababu ya unayoyapitia. Tafuta njia zaidi, jiendeleze na jipe moyo kuwa siku yako ya mafanikio inakuja.

Nahitimisha kwa kusema kila mtu ana uwezo wa kuchagua kuwa anavyotaka kuwa maishani,Dunia ina mengi ya kuyafanya na kuna kila nafasi kwa mwanadamu yeyote anayechagua kuwa anavyotaka maishani. Chagua maisha unayotaka kuyaishi na uyaishi kweli. Usiogope kujaribu kitu, maisha ya kuogopa kufanya kitu ni maisha yasiyo na maana. Usikubali maisha ya ukawaida na yenye usalama ambayo yatakufanya usiishi maisha makubwa unayostahili. Siri kubwa ya watu wenye mafanikio duniani, ni kuwa hawaogopi maisha - wapo tayari kuumia kwa kuchagua maisha wayatakayo.  Chagua unachotaka kukifanya na ukifanye kweli kwa moyo wote. Jiendeleze kila siku katika ulilochagua kiasi ambacho utavunja mipaka na kuweka rekodi yako. Chagua Kufanikiwa.
source:http://www.treasurehousewithinyou.blogspot.com/

Categories:

Leave a Reply