“YEYOTE anayepata kipato na kujihudumia mwenyewe anapaswa kuwa na bima ya ulemavu,” aliwahi kusema mwanasaiokolojia mmoja wa nchini Marekani aitwaye Simon.
Baraza la Usalama la Taifa nchini Marekani liliarifu kuwa zaidi ya watu milioni 20 walikumbwa na majeraha yaliyowasababishia ulemevu kwa mwaka 2002 pekee.
Hili laweza lisiwe jambo la kawaida hapa kwetu lakini kitu tunachoweza kujifunza ni kwamba tunapaswa kuwa na utaratibu wa kujikatia bima.
Hebu fikiri jambo ambalo linakufanya uwe nje ya kazi kwa siku kadhaa au miezi kadhaa litakugharimu kiasi gani na ni iwapo utapata pesa hizo na itakuwaje utakaporejea katika shughuli zako za kawaida?
Ni wazi kuwa utajikuta umebakia nyuma kwa kiasi fulani lakini kama utakuwa na bima ya ulemavu basi shirika la bima linge gharamia matibabu na ungelipwa malipo ya ulemavu.
Msomaji wa safu hii huu ni ulimwengu wa sayansi na maendeleo na unaweza kujiunga na bima bila ya usumbufu wowote na pasipo kuchukua muda mrefu.
Ni rahisi kufanya hivyo iwapo mwajiri wako hayuko tayari kufanya hivyo waweza kuangalia mfukoni kuwa ni kiasi gani ulichonacho na ukawasiliana na kampuni au mashirika ya bima na kujiunga. Kumbuka kuwa unapojiunga na bima ni vyema ukapata sera za aina ya bima unayotaka kujiunga nayo na zisome vyema na ikiwezekana pata maelekezo kwa mtaalamu kabla ya kuamua kujiunga rasmi na aina hiyo ya bima.
Kutotambua ongezeko dogo la matumizi
Matumizi madogo ya pesa, kama ilivyo kwa uvujaji mdogo katika chombo, yanaweza kumaliza pesa ulizonazo katika pochi yako.
Njia ya kuepuka hilo ni kutambua wastani wa matumizi yako kwa siku, wiki au mwezi na iwapo kuna ongezeko basi tambua ni kiasi gani, na iwapo litaweza kuathiri matumizi yako au la.
Baada ya hapo sasa unaweza kuamua kufanya matumizi hayo au kuaachana nayo au kubadilisha na matumizi mengine. Yapo matumizi kama vocha za muda wa maongezi ya simu, safari zisizo za lazima au idadi ya vinywaji ni baadhi ya vitu ambavyo huongeza matumizi japo kwa sehemu ndogo lakini huwa na mabadiliko makubwa katika hali ya fedha ya mhusika.
“Jaribu kuangalia kumbukumbu zako na angalia pesa ulizonazo na madeni unayodaiwa yanatokana na nini? Utaratibu wa aina hii utakupa hali halisi katika matumizi yako ya pesa na utang’amua athari za ongezeko dogo tu la matumizi,” alisema Berkeley Calif, wa Marekani.
Njia muhimu ya kukwepa hilo ni kujiuliza kuwa je, matumizi yaliyoongezeka yana umuhimu wowote?
Kungojea malipo ya pensheni ili kuwekeza
Hili ni moja ya makosa makubwa yanayofanywa na watu wengi. Wafanyakazi wengi wanashindwa kuwekeza wakati wakiwa kazini na hivyo kusubiri hadi walipwe malipo ya kustaafu. Hali hii inawafanya wengi kujikuta wakistaafu huku hawana kitu na hivyo kutumia malipo ya kustaafu katika kutekeleza mahitaji yao na hivyo kukuta pesa hiyo ikimalizika bila ya kufanya jambo la msingi lililokusudiwa ambalo ni kumtunza mstaafu hadi anakufa.
Wengi tunaweza kufikiri kuwa ni jambo lisilowezekana lakini kumbuka kuwa ili uwekeze ni lazima ujinyime na unaweza kufanya hivyo kwa kutenga asilimia ndogo tu kutoka katika mapato yako au kwa wale ambao si wafanyakazi wa ofisini wanaweza kuweka utaratibu wa kuchangiana na wenzake kwa mzunguko na inapofika zamu yake anaweza kuwa na utaratibu wa kuweka pesa benki hadi atakapoona imefikia kiwango cha kufungua mradi fulani anaweza kufanya hivyo.
Ni rahisi kuanza, angalia mfumo wa mapato yako na jiulize kuwa unaweza kuanza na kiasi gani na uamue kuanza kwa ujasiri.
Kusubiri hadi dakika ya mwisho ndipo ukusanye pamoja mtajiWatu wengi huwa na kawaida ya kutaka wapate mtaji wote wa kuwekeza kwa wakati mmoja. Si ajabu kusikia mtu akisema ifikapo Mei nitafanya jambo fulani, au mshahara wa mwezi ujao nitafanyia jmbo fulani.
Kwa utaratibu huo ndugu msomaji utajikuta ukibakia kupanga kuwa nitafanya jambo fulani ifikapo mwezi au siku fulani na siku hiyo haitafika kamwe.
Nilipanga kuwa mwezi huu nitanunua viatu vya watoto wa shule lakini imetokea dharura…” alisikika mama mmoja akisema.
Mama huyu ambaye ni mfanyakazi wa kipato cha mwisho wa mwezi alishindwa kuwa na utaratibu wa kujiwekea akiba kila anapopokea mshahara wake na akafikiri kuwa anaweza kutenga mshahara wake wote kununulia viatu vya watoto lakini dharura ikamkwamisha. Iwapo mama huyo angekuwa na utaratibu wa kujiwekea akiba, dharura isingeingilia mambo yake.
Kulipa kila mtu na kuweka akiba kilichobakiaKamwe usije ukasema kuwa nitaweka akiba kwa kile kitakachobaki. Iwapo utakuwa na mazoea hayo, basi ni wazi kuwa malengo yako ya kujiwekea akiba yanaweza yakashindwa.
Kuweka akiba ni moja ya matumizi muhimu hivyo hakikisha kuwa unalipa kipaumbele miongoni mwa matumizi yako muhimu.
Amua kuwa asilimia 5 au 10 ya kipato changu ni kwa ajili ya kuweka akiba na hakikisha kuwa una nidhamu wakati wa kutekeleza hilo. Usithubutu kulipa madeni yote na kusema kuwa kitakachosalia ndicho nitakachoweka akiba la badala yake waweza ukaamua kulipa sehemu ya madeni na sehemu iliyosalia unaweza kuonana na wadai wako na ukawaomba ulipe wakati mwingine lakini kuweka akiba ni jambo lisiloweza kuahirishwa kamwe iwapo unataka kufanikiwa katika malengo yako.
Iwapo utakuwa na mazoea ya kulipa madeni na kufanya matumizi mengine huku ukisubiri kinachosalia ili kuweka akiba unaweza kujikuta unastaafu kazi bila ya kubakiwa na kiasi cha kuweka akiba. Kumbuka kesho nzuri huanza leo, hivyo kuweka akiba yenye manufaa kunatakiwa kuanza leo, hivyo msomaji wa safu hii panga na uanze leo kujiwekea akiba.
Kushindwa kusimamia vitega uchumi vyako
Hili ni jambo linalowakabili watu wengi na kufanya waishi katika maisha ya kushindwa kila siku.
Ni vyema kutambua kuwa kuweka akiba ya pesa ni jambo moja na kuwekeza pesa hiyo ni jambo jingine. Kuwekeza ni namna ya kufanya pesa uliyojiwekea akiba iweze kuzalisha faida.
Njia nzuri ya kufanya hivyo ni kuwekeza katika miradi mbalimbali, sababu ya kufanya hivyo ni kuogopa kuwekeza katika mradi mmoja ambao unaweza kufa na kukufilisi kabisa. Kumbuka ule msemo wa kwamba ‘usiweke mayai yote katika kikapu kimoja kwani kikianguka yote yanaweza kupasuka’.
Wekeza katika maeneo tofauti au kiasi fulani cha fedha ulizojiwekea akiba. Hii itakusaidia kutambua iwapo mradi uliowekeza unaendelea vyema au la, kama unaendelea vyema unaweza kuongeza mtaji zaidi na iwapo mradi haufanyi vyema unaweza kuachana nao na ukafikiria kufungua mradi mwingine. Dhana ya kuwekeza katika maeneo tofauti inalenga kuhakikisha kuwa mtaji wako wote haupotei.
Kuhakikisha uwiano na kumudu vyema vitega uchumi vyako kunaweza kukusaidia kutambua ni wakati gani biashara ni nzuri na ni wakati gani si nzuri. Hili laweza kuonekana jambo dogo lakini ni muhimu sana na halikwepeki, iwe kwa wafanyabiashara wadogo au wakubwa. Wachumi wanasema kuwa uwekezaji katika maeneo tofauti tofauti huleta faida kubwa ikilinganishwa na uwekezaji wa eneo moja kwa wakati mmoja. Kwa mfano, utafiti uliofanywa na taasisi ya biashara ya taifa nchini Marekani mwaka 2005 ulionyesha kuwa watu waliowekeza katika eneo moja waliweza kupata faida ya asilimia 2.5 kwa mwaka ikilinganishwa na 6 kwa wale waliowekeza katika maeneo zaidi ya mawali kwa wakati mmoja.
Angalia mfano huu waweza kuwa wa kufurahisha laikini una mafunzo ndani yake.
Kwanini unakuwa na samani nyingi ndani ya nyumba? Kwanini uwe na kiti na kochi wakati vyote vinatoa huduma moja tu ya kukalia?
Ni rahisi kuwa vinashirikiana kutoa huduma hiyo na hivyo kumpa faida zaidi mtumiaji. Tambua malengo yako na ona jinsi ya kutekeleza malengo hayo kisha jitoe kikamilifu katika kutekeleza malengo yako.
Kutawaliwa na hisia katika vitega uchumi
Yapo makosa makubwa mawili hapa: watu kuwa na mapenzi mazito dhidi ya vitegea uchumi vyao na kujikuta wakati wowote wakielekeza au kujitoa kwa ajili ya vitega uchumi kuliko kawaida au, wakati vitega uchumi vinapoanza kwenda mrama au kombo hutaka kuachana na mambo mengine na kuhangaika navyo hadi vitakaporejea katika hali ya kawaida. “ Hili ni kosa kubwa japo wengi wanaweza kudhani kuwa ni jambo jema na la muhimu,” anasema mwanasaikolojia wa nchini Uingereza Simon.
Hii ni hatari kwani inaweza kukuletea athari ambazo zinaweza kukufanya ushindwe kufanya mambo mengine ya maisha. Simon anasema kuwa katika utafiti alioufanya kati ya mwaka 2000 na 2002 aligundua kuwa watu waliokuwa na mapenzi makubwa na vitega uchumi vyao walipata hasara ya asilimia 30 na 50 baada ya mambo kwenda kinyume na walivyotarajia. Sababu kubwa ilikuwa ni kwamba walikuwa na mapenzi makubwa mno na miradi yao na wakajikuta wakiacha kufanya mambo mengine na kusikitikia miradi yao kuwa haiendi vyema na hatimaye wakajikuta wakipata hasara katika maeneo mengine.
Nini cha kufanya ili kuepukena na hili? Fanya jambo rahisi kiasi hiki, tambua ni wakati gani biashara fulani inakuwa na soko zuri na ni wakati gani hali ya soko si nzuri.
Jambo jingine ni kuhakikisha kuwa unawekeza katika maeneo tofauti na hapa ni kazi au biashara na usije ukawekeza katika mapenzi

Categories:

Leave a Reply