MTU mmoja aliyejulikana kwa jina la Frederick Douglas, alisema kuwa bahati yako ipo mkononi mwako. Na endapo utaitafuta, ni lazima utaiona.
Douglass anamaanisha kuwa mtu yeyote anayependa mafanikio na kuamua kupambana ili kufikia malengo yake, anafanikiwa. Hiyo ni kutokana na jitihada pamoja na bidii anayoionyesha mtu huyo.
Mtu yeyote ambaye hatataka kujikwamua kutoka katika hali ya dhiki aliyonayo, atabakia kuwa maskini na tegemezi. Utajiri wa watu wale wanaofanya jitihada na hata kufanikiwa hautamsaidia mtu ambaye hapendi kujishughulisha.
Kama hautajikwamua katika hali ya dhiki uliyonayo, kuendelea na ujinga wa kutotaka kujifunza ili kuondoka katika tabu yako, wenye akili watatumia juhudi na maarifa yao na kukuzidi katika hali ya kuwa na mafanikio. Kama utakuwa mwenye upumbavu, busara za wengine hazitakuongoza. Kama utapoteza muda na pesa zako, uchumi wa wengine utafikia kikomo na kukufedhehesha.
Unapokuwa na mafanikio yako binafsi unakuwa na nguvu katika kufanikisha mambo yako mbalimbali unayoyatarajia, na ndiyo maana kila mtu peke yake anafanya jitihada za kutaka kujikwamua kutoka kwenye umaskini.
Katika jamii tunayoishi, kila mmoja wetu ni mjasiriamali. Kila mmoja ni rais katika shirika lake. Hivyo atawajibika katika mafanikio na kushindwa kwa ofisi hiyo.
Wewe na familia yako ni wadau katika shirika lako, na ni jukumu lako kuhakikisha kuwa thamani ya mahitaji ya biashara zako yanakuwepo kwa miaka yote.
Wakati unaendelea kuendesha kampuni yako inayoendelea kukua, inawezekana kupunguza mahitaji makubwa kwa kusimamia vizuri pesa ulizonazo, kusimamia vizuri suala la uzalishaji, mauzo na kufanya utafiti.
Pasipokuwa na mtaji wa kutosha, hakuna uzalishaji. Bila uzalishaji, kampuni yako itakuwa haina kitu cha kuuza. Bila bidhaa, shirika lako litasimamisha uzalishaji. Na bila utafiti, washirika wako hawatakuwa na imani ya kuendelea kuwepo katika kampuni hiyo kwa siku zijazo.
Suala la kutumia akili yako ya kuzaliwa ni la muhimu sana. Utafiti unaonyesha kuwa mara nyingi mtu anayefanikiwa ni yule ambaye anatumia akili yake katika kumpatia faida.
Mfano, mtu mmoja alikopa pesa benki na kuweka dhamana kwa kutumia samani zake za nyumbani. Na alitumia akili yake kuwaza biashara atakayoifanya kutokana na mkopo ule. Alianzisha biashara ya kuuza nafaka kwa jumla na sasa hivi mtu huyo ana malori ambayo yanapeleka mizigo nje ya nchi.
Kufanikiwa kwa mtu huyo kusikufanye na wewe ukaanzisha biashara kama yake, kwani unaweza kukwama. Kinachotakiwa ni kuchekecha akili yako na kuamua kufanya biashara ambayo utaimudu.
Mafanikio katika biashara yako na kifedha yanakuja kutokana na uongozi mzuri katika kampuni yako unayoisimamia. Hakuna milango iliyo wazi katika suala la mafanikio, ni lazima ufanye utafiti, uweke malengo na kutimiza ndoto yako uliyoipanga. Japo kuna misuko suko mbalimbali katika kufikia mafanikio hayo.
Ukosefu wa nafasi isiwe sababu ya kutoa udhuru katika mipango yako inayoshindikana kutokana na kuwepo kwa vikwazo mbalimbali unavyoviruhusu wewe mwenyewe.
Kila maisha unayoyaishi yana nafasi nzuri ya mafanikio. George anasema tunaishi katika dunia ambayo wakati wote ina uwezekano wa kuwa na utajiri mwingi.
Maisha ni somo, na kila somo, linapokujia ni nafasi kwako ya kujifunza. Kila biashara unayoipitia ni nafasi kwako ya kujifunza. Unapowaza juu ya watu unaowafahamu waliofanikiwa, hiyo ni nafasi nzuri kwako ya kujifunza kutoka kwao.
Uwepo wako ni upendeleo wa pekee wa kukufanya uongeze bidii katika mipango yako, na pale unapopata bahati hiyo, nafasi yako ya mafanikio inakuja kwa haraka.
Mtu mwenye mafanikio, mvumbuzi na muasisi ni wale wenye ujasiri na wanaweza kusema, ndiyo, ninaweza! Njia ipo pale na nitaitafuta. Wote hao ambao binafsi wameyakubali maisha na changamoto zake na kuzifanyia kazi changamoto hizo katika mafanikio.
Acha kulalamika kutokana na bahati mbaya uliyokumbana nayo au jambo baya lililokupata, amua kuwa na nafasi ya kubadilika.
Kuna kitu kimoja ambacho unaweza kukifanya vyema zaidi ya mtu mwingine. Ni nini hicho? Tafuta mpaka pale utakapopata eneo lako ambalo utafanya vizuri na kuzidi wengine. Halafu upange mipango yako ukinuia kuwa utafanikiwa.
Kamwe usipende kuwa mtu wa kushindwa ila wewe ndiye unayeweza kupata mafanikio. Inawezekana kabisa mtu aliyezaliwa katika familia maskini, akakua katika hali ya umaskini, akasoma kwa shida na matatizo mengi, hatimaye mtu huyo akaja kuwa tajiri mkubwa.
Mifano mingi tunayokutana nayo ni ya watu walioishi katika hali duni, kutokana na hali ile wakaamua kubadilika na kuwa watu tofauti katika dunia tunayoiishi na wengi wao wamefanikiwa, ni matajiri wanaishi maisha ya raha.
Watu hao mara zote wamekuwa wakiwausia watoto wao kuishi maisha ya kujituma na kufanya bidii ili watakapokua waweze kuwa na mafanikio, pia wasitegemee utajiri wa wazazi wao.
Kamwe usikate tamaa, wala kuvunjika moyo. Utavuna kesho kile ulichokipanda leo.
Kila siku unatakiwa kujiuliza: “Siku hii ya leo kwangu ina maana gani?” utakapofanya maamuzi juu ya siku hiyo, utakuwa tayari kwa kutumia uzoefu ulionao wa kufanya jambo lile ambalo umelipanga.
Umepewa saa 24 kwa siku, siku saba kwa wiki, unatakiwa kuwajibika katika siku hizo. Uko huru kufanya kazi katika muda uliojipangia kutokana na uchaguzi wako.
Uamuzi wa mafanikio upo kwako, hivyo usivunjike moyo katika hatua unayoichukua ya kufanikisha malengo yako.

Categories:

Leave a Reply