KUNA maumivu ambayo binadamu anaweza kuyapata katika maisha yake na kumsababishia kushindwa kuyasahau. Hii inatokana na wakati mgumu anaokutana nao. Lakini ipo dawa ya kuondoa hali hiyo endapo utapingana nayo kwa kuamua kutatua hali hiyo.
Wakati Mungu alipomuumba mwanadamu, alimpa uwezo mkubwa wa kufikiria na kuhisi. Sababu hiyo ndiyo inayomkamilisha binadamu kuwa kamili. Kwa namna moja ama nyingine, binadamu aliye kamili hupatwa na maumivu ya moyo.
Hivi tulivyo na dunia kama ilivyo, hakuna binadamu aishiye bila kupatwa na mateso mbalimbali ya dunia. Hakuna mtu ambaye anaishi bila kukwaruzana na mwenzake, kwa sababu hiyo basi, lazima kuwepo na maumivu.
Wakati unapopatwa na maumivu, unachagua kuyaruhusu au kuyakataa? Ni wewe tu unayeweza kutoa jibu, lakini jibu hilo linaweza kukufanya kuwa huru au mtumwa, kukubali au kukataa, kuongeza ukubwa wa tatizo au kuondoa na kuwa mshindi au muathirika.
Hakuna mwingine anayeweza kusababisha hisia zetu ila ni sisi wenyewe kwa kukubali au kupatwa na hisia. Yeyote anaweza kukudharau, lakini kama hautaliweka moyoni haitakuathiri.
Hakuna atakayekufanya uwe na hasira mpaka utakaporuhusu kuwa katika hali hiyo. Wakati mtu mwingine anapokufanyia kitu cha kukuumiza, kitaendelea kukuumiza kama utakizingatia.
Kama utapatwa na uchungu kwa muda mrefu baada ya kuumizwa, hakuna wa kumlaumu isipokuwa kuilaumu nafsi yako. Ni muhimu kujua namna ya kushughulikia maumivu yanayokupata.
Usiyafiche maumivu yako yanayokupata.
Mfano unapatwa na matatizo makubwa katika maisha na wewe mwenyewe huwezi kuyatatua, kuficha matatizo yako kutakuletea maumivu katika moyo kama vile moto wa volkano unavyolipuka na kukusababishia kufanya vitu ambavyo hukuwahi kuvifanya kutokana na maumivu uliyonayo.
Kutokana na hali hiyo kama umeoa au kuolewa, ni vizuri kukaa chini na mwenzako na kuzungumza naye kwa uwazi juu ya maumivu uliyonayo au zungumza na mtu wako wa karibu ambaye unaweza kumshirikisha hisia zako, nawe utapata matumaini mapya na maumivu yaliyokupata yatatoweka.
Usiondoe au usikwepe matatizo yanayokupata. Kwa asili hakuna anayependa kuumizwa moyo. Ni kweli kwamba tunapopenda, tunajiachia wenyewe mlango wa maumivu.
Lakini pasipo kupenda, tunapata maumivu zaidi. Ni kwa watu wasiopendwa na wasiopenda wanaendelea kuishi katika dunia ya mateso. Kama unateseka na suala la upendo, jambo muhimu la kufanya ni kupenda zaidi. Kwa sababu upendo unaleta uponyaji.
Kumbuka kukwepa matatizo ni kupoteza mwelekeo, simama imara kwenye tatizo lako huku ukitafuta ufumbuzi wake. Kukwepa tatizo ni kujiongezea maumivu moyoni wewe mwenyewe.
Kamwe usiruhusu hisia za maumivu katika maisha yako, unapojeruhiwa moyo wako kwa kusema kuwa kamwe sitamwamini mtu yeyote tena, sitajaribu tena kufanyabiashara, sitamwamini Mungu tena au sitapenda tena.
Usijitwike maumivu ya mtu mwingine, kwani kwa kufanya hivyo kutakuongezea uchungu moyoni mwako. Pia usiyaendekeze maumivu uyapatayo, kwa kuwa ukweli ni kwamba unavyozidi kuyakumbatia maumivu unayoyapata ndivyo unavyouumiza moyo wako.
Moyo wenye majeraha unasababisha magonjwa. Hali ya kuchukia, maumivu na uchungu inasababisha majeraha yasiyotibika. Magonjwa hayo yanasababisha kupata hisia za maumivu. Ili uondokane na hali hiyo ya kupasa kuachilia hali hiyo. Tiba pekee ni kuyaondoa majeraha uliyonayo katika moyo wako.
Watu wengi wanashindwa kuelewa gharama wanazolipa kwa kukaribisha uchungu katika mioyo yao. Mahusiano yaliyovunjika, kupoteza ufanisi, kukosekana kwa amani katika maisha ya ndoa, muendelezo wa matatizo yanayosababisha magonjwa ya akili, kuishiwa nguvu na mwonekano tofauti na hali yako ya kawaida husababishwa na maumivu katika moyo wako.
Kumbuka hasira zisizodhibitiwa hugeuka chuki. Hakuna ugonjwa unaoharibu akili au mwili kama chuki au kinyongo. Kubali au ukatae chuki inaharibu akili kuliko ugonjwa wa kansa mwilini mwako. Inaweza kukusababishia ukafanya jambo usilolikusudia kama vile mauaji.
Kama kuna mtu unayemchukia hata kukupatia majeraha ndani ya moyo wako, njia ya kuwa huru si kumwondoa mawazoni unayemchukia, bali ni kuondoa ile chuki iliyopo ndani yako.
Ni vizuri kuyaondoa maumivu kwenye majeraha yako, kwani unapofanya hivyo kwa haraka inakuletea furaha, kuchelewa kuponya majeraha yako kutakusababishia kupatwa na magonjwa mengine usiyoyatarajia.
Njia za kuponya majeraha yako ni kudhibiti mwenendo na matendo yako, pamoja na kuacha kuhoji kile mtu alichofanya au hakukifanya kwako. Iambie nafsi yako kuwa hakuna faida kuhoji kile kitu ambacho umefanyiwa au hukufanyiwa kwa kuwa hutaweza kuibadili tabia ya mtu, bali unaweza kuibadili tabia yako na mwachie Mungu awe hakimu wa mambo yako na si mwingine.
Safisha majeraha uliyonayo. Mfano kuna binti mmoja ambaye alikuwa anaona kuwa mama yake hampendi, hivyo suala hilo lilimsumbua sana kwa kuwa kila alichokifanya mama yake aliona kuwa amekosea, bibi yake aliamua kumweleza kuwa inampasa kuliondoa jeraha hilo ndani ya moyo wake ili aweze kuishi kwa amani.
Alipoongea naye binti yule alianza kupata mabadiliko ndani ya moyo wake na kuanza kupata uchangamfu kwa kuwa aliamua kuachilia mawazo yale yaliyokuwa yanamtesa na kumwomba Mungu amwondolee hali ile. Kila mmoja aligundua kuwa kuna badiliko kubwa ndani ya binti yule tofauti na alivyokuwa mwanzo. Hivyo ni muhimu kuacha kukumbatia mambo yale yanayotesa mioyo ambayo ukiachana nayo unapata suluhisho la nafsi yako.
Njia nyingine ni kujifunza kusamehe. Si njia nyepesi kusamehe ila hakuna njia nyingine ya uponyaji wa majeraha ya moyo katika dunia zaidi ya hiyo. Lakini unapoamua si njia ngumu. Hata yule aliyechokozwa anaweza kusamehe.
Kuna mama mmoja ambaye alikuwa na majeraha moyoni mwake kwa kuwa mume wake alikuwa na tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani kila siku, hivyo mama huyo alikuwa na kitabu chake cha kumbukumbu ambacho alikitumia kuandika zile siku ambazo mumewe aliwahi kurudi nyumbani, muda na dakika aliyofika. Ilikuwa inampa wakati mgumu sana kwa kuwa alikuta ndani ya wiki saba ni siku mbili tu mumewe alizokuwa akiwahi kurudi nyumbani, na kila siku alipochelewa alikuwa na sababu.
Mama yule alijitathimini na kuona kuwa ana upungufu katika maisha yake, hivyo aliamua kumwomba Mungu, pamoja na kuchukua hatua ya kumsamehe mume wake kwa tabia aliyokuwa nayo ya kuchelewa kurudi nyumbani kwa kuwa kila mara ilisababisha hali ya kutokuelewana katika nyumba. Hivyo aliamua kukichana kile kitabu chake cha kumbukumbu na kukichoma moto. Na aliamua kumwonyesha upendo wa ziada mumewe siku zile alizokuwa akiwahi nyumbani. Haikupita muda mrefu mume yule akabadili tabia yake na kuanza kuwahi nyumbani na kubadili mfumo wake wa maisha wa kuchelewa kurudi nyumbani.
Msingi wa maisha mazuri unakuwepo endapo familia itakuwa na amani. Msamaha umebadilisha mahusiano mengi yaliyokuwa yamevunjika, na pia unaponya majeraha ya moyo.
Usiache kuwaombea wale wanaokuchukia. Inapotokea katika maeneo ya kazi akawapo mtu anayekuchukia na kukusababishia kuachishwa kazi yako, unachotakiwa kufanya ni kumsamehe. Utakapofanya hivyo utakuwa na nguvu ya kutafuta kazi nyingine, kinyume cha hapo utabaki unauguza majeraha yako bila kupata njia mbadala ya maisha yako.
Pia usiache kuwafanyia mema wale wote wakuumizao. Nao pia watajifunza kutoka kwako.
Mruhusu Mungu aponye moyo wako uliovunjika. Unaweza kujihisi kuwa hakuna tumaini lingine katika maisha yako, kwani moyo uliovunjika hauwezi kurekebisha mambo yanayokupata. Kama moyo umevunjika vipande vipande ni Mungu tu awezaye kuurejesha tena upya.
Uushinde ubaya kwa kutenda mema. Si mpango wa Mungu wewe kupatwa na mambo yanayokuumiza moyo wako, kwa msaada wake utaanza upya.
Anza kutenda matendo mema kwa wote waliokutendea mabaya, ishi katika mwenendo unaofaa kwa wengine.

Categories:

Leave a Reply