ILI kufikia malengo halisi ni lazima uwe na haiba ambayo inalingana na viwango fulani. Wachache miongoni mwetu tumezaliwa na haiba inayong’aa na yenye mvuto, lakini inawezekana tukawa tumeruhusu mitazamo hasi na tabia zisizo na mvuto kuweza kuchafua mwonekano ambao haiba yetu inaweza kuwa imeujenga hapo awali.
Hata hivyo bado tunaweza kung’arisha mwonekano wetu wa nje ambao umefifia na kuweza kukuza hisia za wale wote ambao tulikutana nao kama tutapenda kufanya hivyo kwa nia ya dhati.
Nini hasa kujenga haiba yenye mvuto? Kitabu kitakatifu cha Biblia hutoa mwongozo mzuri. "Watendee wengine vile ambavyo nawe ungependa kutendewa,” tamko hilo linaonekana mara kadhaa kwa njia tofauti katika imani mbalimbali za dini pamoja na falsafa mbalimbali.
Kwa usahihi zaidi, msemo huo hujulikana kama kanuni ya dhahabu 'Golden Rule'. Mimi na wewe tunalazimika kuwapo katika dunia inayokaliwa na wengine pia na hivyo ni lazima tutambue namna ya kuishi nao.
Vile tunavyowakabili na kuwatendea watu wote wa jamii na vile ambavyo jamii hiyo inaitikia dhidi yetu kwa kiasi fulani hutegemeana na vile tunavyojisalimisha katika mamlaka ya kanuni hii.
Maisha ni kioo. Vitu vyema huvutia watu wema. Vile ambavyo tunatarajia wengine watuitikie ndivyo ambavyo ni lazima tujieleze.Bila shaka umewahi kusikia ikisemwa kuwa tabia ya mtoto hufunua au kuelezea vile anavyotendewa.
Kama anatendewa kwa upendo atakuwa mwenye kupenda, iwapo anatendewa kwa ukatili na kwa njia ya matusi, basi na yeye atakuwa mkatili na mwenye tabia ya kutukana. Kwa kiasi fulani kuna ukweli ndani yake kuwa tunapa kutoka kwa wengine kile tunachotoa. Na huu ndio msingi wa haiba yetu.
Maisha ni kioo ambacho huakisi mwonekana wako. Kama unatabasamu, basi maisha yataakisi furaha na uchangamfu. Iwapo ni mtu mwenye kisirani na hasira, basi maisha yataakisi hali na picha halisi ya jinsi ulivyo. Kwa asili, kile unachokisema juu ya wengine pia husemwa juu yako.
Huwezi kupata kitu katika dunia hii ambacho hujakipata kutoka kwako kwanza. Asili hujielezea kutokana na mihemuko yako. Kama unafurahi, dunia itafurahi. Kama una uaminifu, basi utaaminiwa. Kama unapenda, basi jua unapendwa. Kama unachukia, jua pia kuwa unachukiwa. Hivyo kimsingi tambua kuwa unachovuna ni kile ulichopanda.
Wanaume na wanawake wengi duniani hutumia kanuni hiyo ya dhahabu ili kujumuisha yale yote waliyoyahitaji kwa kadiri wanavyotembea katika barabara kuyaelekea mafanikio. Mwanamuziki mmoja aliyejulikana kama Leontyne Price alisimulia kisa cha ajabu juu ya namna kanuni hii ilivyobadilisha maisha yake.
Anasema kuwa katika miaka ya 1960 alikuwa ni mwalimu mara baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu cha Ohio. Anasema ingawa alikuwa amefaulu kwa kiwango cha juu, bado alikuwa hajafikia malengo yake. Huku akiwa mwenye huzuni, kufundisha kulionekana kumpatia changamoto kidogo. Aliwapenda wanafunzi wake, japo wakati mwingine alionekana kama mwenye kuchoka. Lakini akafikiri, kwanini iwe hivyo? Wakati akiwa mtoto aliweza kujifunza kusoma maandishi ya muziki kabla hata ya kujua kusoma vitabu. Kuimba ndiko kulikuwa mapenzi yake na sauti ya ndani ikamuita, jambo ambalo lilimfanya anyong’onyee na kukata tamaa kwa kudhani kuwa haliwezekani.
Japo kwa siri aliazimia kuanza kutazama uwezekano wa kuingia katika uimbaji, na mara akaanza kuzuru kumbi za maonyesho. Siku moja wakati akitoka shuleni aliwakuta watoto wakicheza na alijikuta akiwaangalia kwa muda mrefu. Alipenda watoto lakini pia alipenda kuimba. Hapo alijikuta akiwa njia panda, akiwaza juu ya tamu na chungu na iwapo aendelee kufundisha au aache na kwenda kuimba.
Licha ya walimu wenzake kumsihi sana asiache kazi ya kufundisha, aliamua kutii mapigo na matakwa ya moyo wake na siku iliyofuata aliamua kuwasilisha barua ya kuacha kazi ya ualimu.
Wakati wote alipotafakari juu ya njozi zake Leontyne alijiona kuwa na sifa zinazostahili kuwa mwanamziki nyota lakini alibaki kuwa na swali moja kuwa ataweza kutimiza ndoto hizo?
Baadaye aligundua kuwa ili aweze kutimiza lengo lake anahitaji kuongeza ujuzi na hilo lilihitaji pesa au ikiwezekana mfadhili. Huku akitawaliwa na nia mpya iliyokuwa ndani yake, wazazi wake waliamua kuunga mkono uamuzi wake wa kuimba. Hata hivyo kulingana na kikwazo cha kiuchumi, baba akiwa fundi muashi na mama mkunga, waliweza kutoa msaada wa hali tu na si mali. Ilikuwa ni wazi kuwa bila ya kuhudhuria madarasa ya muziki, kusafiri maeneo mbalimbali, na gharama nyingine, kazi yake ingekuwa ni ngumu. Hata hivyo utashi wa kanuni ya dhahabu hautambui mipaka au vikwazo.
Kipindi cha nyuma hata kabla ya kujiunga na masomo ya Chuo Kikuu Leontyne alikuwa na wakati wa furaha wakati akiwa nyumbani kwao mjini Mississipi pamoja na marafiki zake wa karibu wawili ambao waliishi jirani na nyumba yao. Ingawa wakati na hali ya maisha ilikuwa imewatenganisha, marafiki hawa kwa kipindi kirefu hisia zao na kukumbukana vilikuwa ni vitu vilivyodumu.
Alipofanikiwa kumtembelea rafiki yake huyo huku akitarajia kukutana na ukalimu na furaha zile walizokuwa nazo wakati wakiwa wadogo na karibu alijikuta akilakiwa na mama wa rafiki yake ambaye alikuwa mkarimu na aliyekumbuka urafiki wa mabinti hawa wawili.
Leontyne hakusita kumwelezea mama wa rafiki yake juu ya ndoto na malengo yake, hakusita kuonyesha huzuni iliyokuwa ndani yake kutokana na kung’amua kuwa alilazimika kuanza kufundisha tena baada ya kuona kuwa ndoto yake ya kutumbuiza mamilioni ya watu iko mbioni kuyeyuka.
Kabla Leontyne hajainua mkono wake ili kufuta machozi yaliyokuwa yakitiririka katika macho yake, mama huyo mkarimu aliahidi kumfadhili binti huyo ili kumsaidia kuendelea na masomo yake ya muziki na hatimaye aweze kutimiza ndoto yake ya kuwa muimbaji mahiri.
Hata hivyo msaada wa mama huyo uliambatana na masharti. Alimuambia Leontyne kuwa angemsaidia tu iwapo atakubaliana na wazo kuwa atakapofikia malengo yake na yeye ahakikishe kuwa anakuwa mkono wa msaada kwa yeyote atakayehitaji na angefanya hivyo kwa kumpasia kanuni ya dhahabu, jambo ambalo Leontyne alikubaliana nalo kwa moyo mweupe.
Leontyne ameishi kwa uaminifu na kutimiza makubaliano ambayo alifanya na mama wa rafiki yake na kwa hakika amekuwa msaada mkubwa kwani ameweza kuwasaidia wasanii wengi ambao walihitaji msaada ili waweze kufikia malengo katika maisha yao na kukamilisha njozi ambazo walikuwa nazo.
Na hapo kanuni ya dhahabu ikawa na maana kwake kuwa alipenda kutendewa vyema na wengine kama alivyofanya mama wa rafiki yake na yeye amepaswa kuwatendea wengine hivyo, na hapo ndipo ule msemo wa unachokitoa kwa wengine ni kile ambacho umekipokea kutoka kwa wengine unapotimia.

Categories:

Leave a Reply