ASILI humpatia mtu kazi za kufanya pamoja na changamoto za maendeleo. Kwani sote tunajua kuwa maendeleo yoyote hutokana na juhudi. Na juhudi hiyo ndiyo inayomuimarisha mtu.
Maisha huwapendelea wale ambao wanaweza kuwa na msimamo juu ya kitu fulani, hata pale wanapokumbana na matatizo kwa sababu wakati mwingine ni lazima kupitia ugumu fulani. Hiyo ni sehemu ya changamoto za maisha.
Maisha siku zote ni changamoto. Elewa kuwa wewe si mtu pekee unayekabiliana na vikwazo hivyo katika maisha ya kila siku. Kumbuka unaishi katika dunia yenye changamoto.
Tuangalie mifano michache ya maisha ya watu wengi mashuhuri waliofanikiwa. Kwa mfano, Beethoven alipoteza uwezo wa kusikia kabla ya kutunga nyimbo nyingi ambazo kwazo anakumbukwa hata leo.
John Militon aliandika juu ya mbingu iliyopotea wakati akiwa kipofu.
Abraham Lincoln ambaye alikuwa mmoja wa marais wa Marekani, alilalazimika wakati fulani kukopa pesa kwa ajili ya nauli ya gari moshi kwa ajili ya kwenda kujitambulisha yeye mwenyewe.
Na baada ya kutafuta kazi yenye malipo mazuri kwa miaka mingi, Albert Einstein aligundua nadharia ya ‘relativity’ wakati akifanya kazi kama karani katika ofisi moja. Nadharia hiyo inasema kuwa vipimo vya mwendo nafasi na wakati vinawiana au kukadiriana. Nadharia hii imekuwa mashuhuri sana hata leo.
Marian Anderson ambaye hadi leo amebakia katika historia kuwa mwanamke aliyekuwa na sauti nzuri na nyororo, alipata mafanikio baada ya baba yake kufanya kazi ya kutembeza makaa ya mawe katika mitaa ya Phildephia ili aweze kupata ada ya kumsomesha muziki.
Hakujawahi kuwa na mtu mwenye mafanikio au kipaji ambaye hakuwahi kufahamu juu ya kushindwa hapo kabla, kuchanganyikiwa au kukabiliana na kipindi kigumu.
Wakati ambapo hakukuwa na pesa au ilikuwa adimu, wakati ambapo anakosa mguso wa ubinadamu, wakati mawazo mapya yanapokoma, au wakati mwili wako au hisia zinapokuwa zimefikia ukomo. Ishara ya mafanikio ni uwezo wa kukabiliana na hayo yote na kuyashinda huku yakikuacha wewe ukiendelea kuwepo.
Kuchanganyikiwa, kukata tamaa na wakati mwingine majonzi vinaweza kukuongoza katika furaha na mafanikio. Mara nyingi wale wote ambao hushinda wakati mgumu ni wanaume na wanawake ambao mwishoni hupata mafanikio makubwa na hawa ndiyo ambao wanatuhamasisha.
Katika mada hii, ningependa tujadiliane kanuni ambayo ukiifuata hutashindwa katika maisha yako. Kwa kuifuata kanuni hiyo unaweza kuongeza ubora na utajiri katika maisha yako, hatimaye kukufikisha katika malengo unayoyatarajia.
Pasipo tabia hiyo, huwezi kufurahia utajiri kwa jinsi yoyote ile. Kwa kanuni hii, matarajio mengine yataimarika na kufikia bidii zako na kufanikisha malengo yako yote. Tabia hii itakupa amani katika moyo wako, ambayo kamwe haitapeperusha mawazo yako. Kanuni hiyo ninayoiongelea ni ya msimamo.
Kuwa na msimamo maana yake ni kusadiki, shauku, uvumilivu na ujasiri katika kipindi unachokumbana na vikwazo mbalimbali. Zaidi ya yote inamaanisha kuwa usikate tamaa, usijiondoe na kamwe usikubali kushindwa.
Nguvu ya kuwa mtu wa msimamo ni tabia iliyoko kwa wanaume na wanawake wengi, ambao wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa. Hahihitaji kuwa na akili sana ya mtu msomi, mwenye kipaji au rasilimali ni vile kuwa na malengo, bidii na uimara ambao utakupeleka kwenye mafanikio makubwa yako binafsi.
Wote waliofanikiwa katika maisha ni wale ambao wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali za kutaka kuwa na mafanikio, ambao hawakupenda kuamini kuwa wana vipaji, lakini ambao wameamua kuwa wanaweza kufanikisha jambo lolote lenye thamani, hiyo ni kutokana na kuwa na msimamo pamoja na jitihada.
Mwanafalsafa Epictetus alichunguza kuwa, “si vitu peke yake vinavyowasumbua wanaume, lakini ni uamuzi kuhusu vitu hivyo.” Maisha ni mwendelezo wa kukua na usafi, yenye changamoto na vikwazo.
Ni njia ya kuchuja udhaifu, uvivu na mambo yote yasiyovutia – yeyote yule asiye imara au anayekataa kujisimamia kwa nia ya kufanikiwa mara zote kanuni hiyo inakuwa mbaya kwake muda wote.
Mtu anayejituma binafsi anapaswa kuelewa kuwa kuna vikwazo mbalimbali mara zote katika maisha ambavyo anastahili kuvishinda. Waliofanikiwa wamekabiliana na changamoto hizo kwa haki na wana nguvu za kutosha, malighafi ya kutosha, na uthabiti unaotosha kuwazuia kuingia kwenye hatari hiyo ya kushindwa.
Uzoefu unaonyesha kuwa, mwanadamu huwa hatulii anapokaribia kuwa na mafanikio na wakati anapojiona anashindwa, hujitahidi kuondokana na hali hiyo ya kushindwa. Hivyo hutulia na kuanza kufikiri malengo yake ya mafanikio.
Anapofikiri kwa utulivu anagundua kuwa kushindwa si kitu, kinachotakiwa ni kuongeza jitihada katika kufikia malengo yake aliyoyapanga kwa kuweka mipango mipya ya kuweza kufanikiwa.
Mara nyingi hali ya kushindwa inatokana na mipaka ambayo watu wamejiwekea katika akili zao, kama watakuwa wajasiri na kupiga hatua moja mbele zaidi, watafanikiwa.
Kwa kawaida, hali ya kushindwa inawaathiri watu wengi katika njia mbili. Kwanza inawasaidia kama changamoto kubwa ya kupata mafanikio au inapunguza nguvu na kuwavunja watu moyo kwa nia ya kujaribu tena.
Walio wengi wamekuwa na matumaini ya mafanikio, wengine kuachilia na kupata dhiki katika nafsi zao kabla ya kujaribu. Pia inasemekana kuwa hali ya kushindwa inamfanya mtu kuwa na mipango mipya katika maisha ya mafanikio.
Somo kubwa katika maisha ni kujifunza ni jinsi gani ya kutumia fursa uliyonayo ya kupata ushindi kutoka katika hali ya kushindwa. Hiki ni kipimo cha kutofautisha wote waliofanikiwa na wote wasiofanikiwa.
Kiongozi hatakiwi kukata tamaa kutokana na kushindwa, lakini wakati wote anatakiwa kuwa na msukumo wa mafanikio. Kwa kuangalia kushindwa kwako, itajulikana kama kiongozi huyo anafaa kuongoza.
Wakati mwingine utakapokabiliana na kushindwa, kumbuka kuwa kila changamoto unayoipata na taabu inachukuliwa kama mbegu yenye faida. Anza kuitambua hiyo mbegu na kuipanda kupitia vitendo. Utagundua kuwa hakuna hali ya kushindwa katika maisha mpaka pale utakapoikubali hali hiyo.

Categories:

Leave a Reply