Umuhimu wa Huduma bora kwa Wateja-Terminal Clouds Fm, Tz Yangu ya 24th March,2012.

"
"Kumbuka biashara sio siasa, biashara ni ahadi na utekelezaji na sio ahadi na sababu za kwanini imeshindikana hiyo waachie wanasiasa."

"Mafanikio yako duniani katika maisha yanategemeana sana na mahusiano mazuri uliyonayo na yule mtu unayemuuzia ulichonacho. Wote tupo katika biashara ya maisha, lakini watakaotengeneza faida ni wale wanaojua kutoa huduma bora kwa wateja wao."
"

Binadamu wote tupo katika biashara ya maisha. Mafanikio yetu katika biashara ya maisha hutegemea sana na uwezo wetu wa kutoa huduma kwa wateja kupitia makampuni, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali, biashara zetu,vipaji vyetu na mengine mengi. Mteja ndio sababu ya uwepo wa kampuni,taasisi,bidhaa na biashara zote. Biashara yoyote duniani haiwezi kufanywa wala kuishi bila mteja.

Mteja ndio sababu ya mafanikio ya taasisi, kampuni na biashara zote duniani hivyo basi huduma bora kwa wateja ni muhimu sana zaidi ya maelezo. Huduma bora kwa wateja ni moyo wa biashara, hata kama unamiliki duka la aina yoyote mahali popote, saluni, mfanyakazi serikalini na katika makampuni ama biashara ya aina yoyote huduma bora kwa wateja si jambo la kudharau wala kulichukulia kawaida.

Labda inatubidi tufahamu maana halisi ya huduma kwa wateja; HUDUMA KWA WATEJA ni mfululizo wa shughuli kwa mteja kabla, wakati na baada ya kununua bidhaa au huduma ili kuongeza kiwango cha mteja kuridhika , kihisia kuwa bidhaa au huduma imekutana na matarajio yake. Huduma kwa wateja inaweza kutolewa na mtu kama mwakilishi wa mauzo ama huduma au mhusika mwenyewe kulingana na shughuli yake. Utoaji wa huduma bora kwa wateja una nafasi muhimu sana katika maendeleo ya shirika ama mtu binafsi katika biashara ya aina yoyote.

Hivyo basi lazima iwekwe kama sehemu muhimu sana katika maisha ya taasisi,shirika na maisha yetu siku zote katika shughuli za aina yoyote. Mteja ni wa thamani sana katika shughuli ama biashara yoyote, utoaji wa huduma bora huwafanya wajione hivyo kuwa ni wa thamani na warudi tena na tena. Huduma bora kwa wateja si tu kusaidia wateja kupata huduma fulani au kununua bidhaa unayouza ama kuwa na uzoefu mzuri ni zaidi ya hapo, kuvuka matarajio ya wateja, kuwafanya wajisikie vizuri.

Sababu kubwa ya mafanikio katika biashara na hata huduma zozote, hutokana na ujanja, ujanja wa kumfanya mteja arudi tena na tena ama kumshikilia na kumfanya wa kwako siku zote kwa kumfanya ajisikie vizuri kufanya biashara na wewe. Ukitaka kufanikiwa maishani, iwe katika biashara, huduma ama ushauri wa aina yoyote mfanye mteja akupende na zaidi ajisikie vizuri kufanya biashara na wewe, tunaishi katika dunia ya kushindania wateja na ukitaka kushika mkia katika biashara dharau mteja, hata kama una bidhaa nzuri tena original, zinazong’ara kama hujui kujali mteja utashika mkia katika biashara. Hata kama una kiburi cha aina gani usimletee kiburi mteja wako.

Mteja anahitaji kubembelezwa na kujiona wa thamani ili arudi tena; Mambo muhimu ya kuyafanya ili kuboresha huduma kwa wateja ni kama yafuatayo:
1. Ifahamu huduma ama bidhaa yako kwa undani sana.
Unapotoa huduma ama kuuza bidhaa yoyote kwa mteja hakikisha unaijua bidhaa hiyo mbele na nyuma. Hata kama ni mwakilishi wa shirika, ifahamu bidhaa yako. Usiwe mbabaishaji wa biashara unayofanya mwenyewe kiasi ambacho unashindwa hata kujibu maswali ya mteja wako kuhusu bidhaa yako.Hakikisha kwamba hujamwacha mteja wako na swali ambalo halijajibiwa

2. Jifunze Lugha nzuri ya mawasiliano kwa mdomo/kimwili
Mfanye mteja ajisikie muhimu kwa maneno ya busara mwenyewe. Unapotoa huduma toa lugha chanya ya mwili , tabasamu, na mawasiliano ya macho ili kuonyesha unamsikiliza mteja. Acha kuonyesha uso uliozubaa watakukimbia. Maisha ni mchakamchaka changamsha uso na mwili wako kwa kutabasamu ili upendeke na kukubalika halafu utaona biashara ama huduma yako itakavyosonga mbele.Msikilize mteja, cheka na mteja na zaidi mpende kwani ndiye anayekufanya utengeneze kipato chako.

3. Usitoe ahadi usizoweza kuzitekeleza
Acha kudanganya wateja. Toa ahadi ya kitu unachoweza kukifanya. Kila mwanadamu anatafuta mahusiano na mwanadamu mwaminifu. Ukikosa uaminifu duniani watakukimbia wengi, sema ukweli wako wa moyo na fanya kile ambacho uliahidi. Kumbuka biashara sio siasa, biashara ni ahadi na utekelezaji na sio ahadi na sababu za kwanini imeshindikana hiyo waachie wanasiasa.

4. Nenda maili zaidi ya matarajio ya mteja-
Daima tafuta njia za kumtumikia mteja wako zaidi ya anavyotarajia. Katika kufanya hivyo inawasaidia kujua kwamba wewe unajali na itawafanya wajisikie vizuri na kurudi kwako. Kuwa msaidizi, wasaidie kwa hali unayoweza hata kama hakuna malipo, kumbuka kuwa duniani tumekuja kuhudumiana na si kunyonyana, kuwa na moyo wa kutoa huduma zaidi na hata kusaidia utapendeka na kukubarika na biashara yako itasonga mbele sana.

5. Sikiliza malalamiko ya wateja na uyatatue.
Usiyakimbie wala kujitetea, tafuta jibu. Kama mteja hajaridhika na huduma tafuta sababu ni kwanini na nini ufanye. Kama umeuza bidhaa mbovu au iliyovunjika tafuta njia kuibadilisha au hata kurudishwa. Tafuta njia ambayo wateja wanaweza kutoa malalamiko yao na kuyatatua. Kila kitu kinawezekana duniani, usikimbie tatizo lifuate huko huko liliko na kulimaliza.

Mafanikio yako duniani katika maisha yanategemeana sana na mahusiano mazuri uliyonayo na yule mtu unayemuuzia ulichonacho. Wote tupo katika biashara ya maisha, lakini watakaotengeneza faida ni wale wanaojua kutoa huduma bora kwa wateja wao.
MUNGU IBARIKI AFRICA
MUNGU WABARIKI WATANZANIA
source:treasurehousewithinyou.blogspot.com/2012/03/umuhimu-wa-huduma-bora-kwa-wateja.html

Categories:

Leave a Reply