Maisha ya mwanadamu duniani ni safari ya kutafuta maana ya maisha. Ni kweli tumesikia na kujifunza mengi katika dunia lakini maana ya maisha iliyo halisi na ya kweli ya mwanadamu mhusika hutoka ndani ya binadamu mwenyewe. Kila mwanadamu anao ukweli wa maisha yake ndani yake. Mambo yote tunayoyaona duniani,ugunduzi,vitabu,miziki,filamu na kila kitu kilichopo duniani kilichosababishwa na mwanadamu asili yake ni ndani ya binadamu na si nje. Ndani yako mwanadamu kuna maajabu, ndani yako kuna hazina ya maisha,vipaji,talanta na habari njema ya maisha yako . Ndani yako umebeba hazina ya vipaji vyako.

Kila maisha ya mwanadamu yeyote duniani, yanayo maana pekee. Na kila mwanadamu duniani ni wa pekee. Hakuna mwanadamu duniani kama wewe, hajawahi na hatatokea mwingine kama wewe. Uwepo wako duniani ni kwasababu umebeba maana ya kipekee kuhusu wewe. Kutokana na upekee ulionao duniani, huna mshindani, mshindani wako ni wewe mwenyewe.Historia ya dunia inaonyesha kuwa wanadamu walio wengi duniani wanafichwa mambo ya ukweli na makubwa kuhusu uwezo wao.

Toka enzi za akina Adam Smith, kipindi cha viwanda na utumwa wanadamu wengi, waliishi chini ya viwango kwa kutumika kama mashine zinazoweza kubadilishwa wakati wowote, hii imekuwa sababu kubwa ya binadamu wengi kutokujua ukweli wa vipawa ndani yao na hata kutojiamini kabisa. Hii yote ni mipangoi inayofanywa na baadhi ya binadamu wenye nia ya kuumiliki ulimwengu kwa kuwafanya wanadamu wengine kutojua thamani na vipawa vyao vya ndani. Inasemekana ni asilimia kama 0.25 ya wanadamu wanaoujua ukweli wa maajabu ya mwanadamu ndani. Tunayo mengi ndani yetu, lakini wengi tumetongozwa na mifumo ya dunia inayotufanya wengi tuishi chini ya viwango. Kumbuka kuwa maana ya maisha unaitengeneza mwenyewe, anza kutafuta ukweli wako wa maisha uishi maisha yako.

Vilevile Kutokana na mabadiliko ya maisha, karne hii ya 21 inatabiriwa kuwa karne ya vipawa na maajabu ya ndani ya mwanadamu kwani imedhihirishwa na baadhi ya watu wa kawaida sana ambao wameweza kugundua mambo mengi kwa kutumia vipawa vyao. Na kadri siku zinavyosogea ulimwengu huu utaongozwa na kuendeshwa na binadamu wanaotumia zaidi vipaji vyao na si watu waliolewa na mishahara ya mwezi, dunia hii itamilikiwa na watu walioamka huku wakijua thamani yao na si wale wanaopinga ukweli huu ambao wameamua kubaki kama replaceable(cog) mashine katika makampuni na viwanda, wasiotaka kuvumbua maajabu yao.

Dunia hii ina mengi ambayo hayajaonyeshwa bado na itabaki kuwa na mapungufu siku zote kama wewe hutaamua kuishi kama wewe kwa kutumia vipaji vyako wewe na talanta ulizojaliwa ndani yako.Tunaishi katika dunia ambayo ni rahisi kubebwa na misukumo ya nje na wengi hawaamini ukweli huu kuwa kila mtu ana kipaji, kila mtu ana habari njema ya ndani yake hii ni kwasababu wengi wametongozwa na kushawishiwa na mifumo ya dunia na maisha ya wanadamu wengine na kujikuta kuwa wanaishi si kama wao bali kama nakala.

Watu wote wenye mafanikio duniani, ambao huonekana kana kwamba wamebarikiwa hutafuta maana ya wao kuwa wao,uwezo wao wa kipekee na kutumia upekee walionao na kuishi maisha yao kimafanikio watakavyo wao. Dunia hii inayo nafasi kwa mwanadamu ambaye anatafuta maana ya maisha yake mwenyewe, haijalishi umezaliwa katika familia ya aina gani bali ukikubali ukweli kuwa unayo hazina ya maisha ndani yako basi maisha yako yatapata maana.

Unacho kipaji ndani yako.Hakuna mwanadamu ambaye hakuumbwa na kitu ndani yake, Mungu hakuumba takataka duniani,Mungu aliumba mwanadamu mwenye hazina ndani yake. Kila mwanadamu anao uwezo wa kipekee na kiasili aliojaliwa na Mungu ambao bila yeye hakuna ukamilifu. Uliletwa duniani ili ukamilishe upekee wako. Wewe ni ukamilifu wa dunia, kuishi kama nakala haina tofauti na kuishi kama marehemu anayetembea.

Unaweza usiwe na uwezo wa kuimba lakini ukawa na uwezo wa kuchekesha, unaweza usiwe na uwezo wa kufundisha lakini ukawa na uwezo wa kuandika, unaweza usiwe na uwezo wa kucheza mpira lakini ukawa na uwezo wa kuigiza zaidi ya Steven Kanumba, unaweza usiwe na uwezo wa kuchora katuni kama nathani Mpangala lakini ukawa na uwezo wa kuimba, ili mradi tu kuwa wewe ni binadamu basi unao uwezo Fulani wa kipekee ndani yako. Hakuna binadamu aliyeletwa duniani bila sababu, ni dunia tu ndiyo inayotutongoza tulio wengi na kujikuta tunaishi kama nakala.

Wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia icheke, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia icheze,wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia itembee, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia ifikiri, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia isikilize radio,TVs na muziki, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia ing’are na mengine mengi unayoyajua na ambayo mpaka sasa hatujayajua bado lakini yamo ndani yako.

Dunia hii inakuhitaji wewe kama wewe, na mafanikio yako duniani yanakutegemea wewe kama wewe. Hata kama usipokubali ukweli wa uwezo wako wa ndani, haitaondoa maana ya ukweli ulio ndani yako. Kumbuka kuwa utamu wa maisha duniani ni matumizi ya kipaji chako na kusikiliza sauti ya ndani.Ulipewa vipaji ili uvitumie duniani katika biashara,kazi,sanaa,uongozi,ujuzi,masomo na mengine.

Amua kujitafuta mwenyewe, amua kujichunguza mwenyewe utashangazwa mwenyewe utakayoyakuta ndani yako. Tafuta vitu unavyovipenda duniani,tafuta mambo unayoyapenda kuyafanya duniani,tafuta kusikiliza sauti ya ndani,ipende na ipe nafasi huku ukiongea nayo utaweza kugundua kitu ndani yako. Jifunze ujuzi mpya,jifunze mambo mapya,jiongeze mwenyewe,jipanue kiuwezo kila siku ya maisha yako na jiachie bila kuogopa utagundua unachokipenda na hata kipawa chako.

Bila kujionea aibu mwenyewe, jiulize kasoro zako ulizonazo na jinsi ya kuzizuia au kuzipunguza,tafuta kujua mazuri ya kwako huku ukitafuta kuongeza mengine. Ukiona kama kuna kitu kinakufurahisha duniani, usiogope kujaribu,jaribu, jaribu tena ipo siku utagundua wewe ni mzuri wapi.

Sikiliza zauti za dunia lakini sikiliza sana sana sauti yako ya ndani kwani ndiko kutokako chemchem ya uhai wa maisha yako. Jifunze kujiuliza, wewe ni nani? Umetoka wapi? Una nini cha kujivunia duniani? Unataka dunia ikukumbuke vipi? Je uko tayari kuja duniani kama moshi na kuondoka kama moshi, usikumbukwe? Nini unaweza zaidi ya mwingine? Ni nini madhumuni yako duniani?

Kumbuka kuwa wewe ndiye mkurugenzi mtendaji wa maisha yako, mazingira,mifumo,familia na vikwazo vyovyote duniani visiwe sababu ya kuutuliza utu wako. Unazo nguvu zaidi ya nguvu zilizo nje yako za kuwa unavyotaka, kulingana na jinsi ulivyojaliwa. Vipo vitu vinavyoweza kukuzuia hata kukumaliza lakini ni uamuzi wako kusimama kidete kwaajili ya maisha yako na kuonyesha nguvu zilizo ndani yako au kukubali kumalizwa bila ubishi wowote.

Vipo vitu vingi vinavyoweza kukuchanganya lakini ni uamuzi wako kukubali kuchanganywa na kuishi maisha ya bora liende au ili mradi kumekucha mpaka unakufa bila maana au kuamua maisha yako na kusema ama zangu ama zao nitakuwa vile ninavyotaka maishani. Kumbuka kuwa dunia haina huruma kwa mwanadamu aliyekubali kumalizwa,vumilia,jiamini,Jipende,jiendeleze,jikaze ,jionyeshe,jikubali na mwisho wa siku dunia itakukubali tu hata kama kuwe na nguvu zozote mbele yako.

"KUMBUKA KUWA DUNIA HII ITAENDELEA KUENDESHWA NA HATA KUTENGENEZWA NA BINADAMU WENYE UELEWA MPANA WA NGUVU ILIYO NDANI YAO NA SI WABABAISHAJI NA WENYE MAISHA YA MIDADI"

Mungu awe nawe siku zote katika safari yako.
Geophrey Tenganamba; 0714477218
source:http://www.treasurehousewithinyou.blogspot.com/

Categories:

Leave a Reply