Baba ni zaidi ya kuchangia DNA ya Baba.-Tz Yangu Terminal Clouds Fm, on 4th February,2012. na Haris kapiga and Abella bateyunga

Baba ni zaidi ya kuchangia DNA ya baba ili kutengeneza mtoto mwenye DNA ya baba. Mwanaume inabidi atambue kuwa hatakamilika kuwa baba kama hajajua kuwa baba ni zaidi ya kuzaa, baba ni zaidi ya kuchangia DNA ya baba kumpata mtoto mwenye DNA ya baba bali ni uwepo wake na uhusika wake kama baba wa watoto aliowazaa mwenyewe .Uwepo wa baba ni kuwa mhusika kwa kujua kabisa watoto wanahitaji mwongozo wa baba kimaisha,kifkra,kisaikolojia,kijamiii na hata kiuchumi.

Si kila mwenye maumbile ya mwanaume ni baba na wala si kila mwanaume aliyechangia kuzaa mtoto ni baba bali ni Yule anayejua kuwa yeye ana wajibu katika maisha ya watoto wake wa leo na hata watakaozaliwa kutoka kwa watoto wao kutokana na uhusika na uwepo wao kwa watoto wao wa leo kama baba. Ni rahisi kwa mwanaume kuzaa na kupata mtoto lakini si rahisi kwa mtoto kumpata baba anayehusika na yupo kama baba. Usizae kama huwezi kuwa na kuwepo kama baba.

Kila mwanaume mwenye uwezo wa kuzaa anaweza kuwa mzazi na si baba. Na sio kwamba haiwezekani mzazi mwanaume kuwa baba wa ukweli bali ni kwasababu wengi hawataki kujifunza na kuamua kuwa hivyo. Baba ni zaidi ya kuitwa baba, baba ni zaidi ya mzazi baba ni uwepo na uhusika kama baba. Ni kweli dunia ina mengi, maisha yana mengi ya kujifunza katika malezi ya watoto tunaowazaa wenyewe.

Mama ni mwanamke ambaye huwa karibu sana na mtoto na si kwasababu alizaa peke yake ila ni kwasababu mtoto hutoka tumboni mwake mwenyewe, chakula cha mtoto hutoka ndani yake mwenyewe na humlazimu kuwa karibu sana kuliko baba na hivyo hujenga hisia zaidi kwa motto lakini haimaniishi kuwa uwepo wa baba hauitajiki hapo. Wajibu na nafasi ya mama huwa ni ya mama lakini hawezi kuwa baba hivyo basi uwepo wa baba huwa muhimu zaidi. Ni muhimu mwanaume atambue kwamba kuwa na uwezo wa kuzaa mtoto si uwezo wa kuwa baba. Mtoto anamhitaji baba,mtoto anahitaji uwepo wa baba,mtoto anahitaji mwongozo wa baba,mtoto anahitaji ladha ya baba.

Wengi wanazaa lakini hawaishi na hawapo kama akina baba, hawahusiki kama akina baba. Baba asiyekuwepo katika maisha ya mtoto ni sawa na baba aliyekufa lakini anatembea. Baba asiyekuwepo ni baba anayeangamiza maisha ya binadamu wengine pasipokujua. Mtoto aliyelelewa bila uwepo wa baba huwa na maopungufu Fulani, na mzazi mwanaume aliyezaa na kupotea ni shetani wa pili wa mtoto
Baba asiyekuwepo katika maisha ya mtoto husababisha mengi katika ukuaji wa mtoto, kisaikolojia,kimahusiano,kiuchumi,kimaadili,kiakili na hata kiuajibikaji.

Mtoto anayeishi bila uwepo wa baba huvamiwa na dunia isiyofikiri na wala kusikiliza hisia zao. Wengine hujiingiza katika madawa ya kulevya,bangi na hata katika mahusiano huwa ni shida kwa watoto wa kike kwani wengine hujiingiza vibaya katika mahusiano na wanaume ili waweze kuziba pengo la baba. Uwepo wa baba kwa mtoto ni muhimu sana.

Baba asiyekuwepo huacha maswali mengi katika kichwa cha mtoto anayekua ambaye mara nyingi sana hupata majibu yasiyo sahihi ya maswali hayo katika maisha yake. Uwepo wa baba unahitajika ili kuyajibu maswali hayo kwa mtoto. Mama peke yake hawezi kuyajibu maswali hayo.

Ni kweli maisha yana mitihani mingi na yana mengi ya kujifunza.Na Maisha ya ndoa yana changamoto nyingi lakini ni tamu kwa wale wanaojua kuwa ndoa ni makubaliano ya kuishi pamoja kwa kutafuta mazuri ya ndoa na kuyapa nafasi zaidi, na kuyapoteza yale yanayoleta usiku.Wazazi wawili wenye watoto wana wajibu sana katika maisha ya watoto, na baba ni binadamu wa muhimu sana katika familia na maendeleo ya familia.

Baba ni kiungo muhimu katika maisha ya watoto wa leo na wa baadaye, na ni mhusika wa kwanini mambo hayapo jinsi yalivyo katika familia. Baba ni nguzo ya familia, baba ni mkurugenzi mtendaji wa familia, ni raisi wa familia, Ni Mungu wa pili wa familia na zaidi ni mhusika wa kwanza katika maisha ya watoto na mwelekeo wao. Watoto wengi wanaopoteza mwelekeo Tanzania chanzo chake ni akina baba wanaozaa tu na hawapo kama akina baba.

Familia zinazovunjika zinababishwa na baba asiyejua kuwa yeye ni binadamu mhusika wa kwanza wa kuyaweka mambo sawa katika familia. Jambo muhimu ni kwamba baba anayejua kumpenda mama wa watoto ni baba anayeweza kuijenga familia na hata kutoa mwongozo mzuri wa watoto.
Ni kweli maisha yana majaribu na vikwazo vinavyoonekana kama haviwezi kutatulika lakini kwa baba anayejua kuwa baba ni zaidi ya kuzaa basi lazima awe tayari kutafuta jawabu hilo.

Maisha yana majawabu,ndoa ina majawabu, mahusiano yana majawabu lakini huonekana kwa baba anayetaka jawabu. Mpumbavu yeyote anaweza kusema hili na lile haliwezekani lakini mwenye akili na hekima hutafuta njia ya kwanini hili na lile linawezekana. Baba ajue kuwa yeye ni baba anayetakiwa kuhusika kwa mtoto na mama yake kimapenzi,kiuchumi,kijamiii,kimahusiano na hata kiroho. Upendo wa baba kwa mama usio na mawaa hubaki kuwa jawabu kubwa la ndoa na hata malezi bora kwa watoto waliowazaa pamoja.
Na uwepo wa baba ni pale anapoishi maisha ambayo mtoto anaweza kujifunza, na ikumbukwe kuwa mtoto hajifunzi kwa maneno ya ukali ya baba bali kwa matendo yake kwa mama na familia nzima kwa ujumla.

Na kipimo cha mwanaume si umbile na uwezo wake wa kimwili bali ni uwezo wa kuishi kama mwanaume mwenye wajibu kwa watoto, familia na jamii inayomzunguka na anayejua kuwa yeye ni baba anayeongoza meli ya familia isizame. Mama anaweza kufanya mambo anayofanya baba lakini hawezi kuwa baba.Na hakuna mwanamke yeyote duniani anayeweza kuwa baba na hakuna mwanaume yeyote anayeweza kuwa baba. Hivyo basi uwepo wa baba ni zaidi ya DNA ya baba bali ni kuhusika kama baba,kuishi kama baba,kuwepo kama baba na kutoa huduma zote zinazohitajika kama baba. Na kuishi maisha ambayo watoto watajifunza na kujivunia kuwa na baba anayeishi.
source:http://www.treasurehousewithinyou.blogspot.com/

Categories:

Leave a Reply