Ongeza Thamani Yako katika Maisha Yako-Jicho La Tofauti na Haris Kapiga Gospel track Clouds Fm. January 22,2012

Maisha ni shule ya kuishi na kila mmoja ni mwanafunzi wa maisha yake. Na ukichunguza watu wote duniani walioweza kuyafanya mambo ya ajabu na kuonyesha uwezo wao utakuta kuwa wana sifa Fulani za kufanana kwa jinsi walivyoweza kuvumbua mambo yao ya maisha yao katika shule hii. Twaweza kusema labda walijaliwa sana kuliko sisi kutokana na mafanikio yao na uwezo wao wa kufanya mambo kiubora kuvuka mipaka lakini ukweli utabaki palepale kuwa kila mtu ana hazina ya kuyafanya makubwa yake.

Mwanadamu ni kiumbe ambaye ana uwezo usiopimika, ni kweli mazingira yametufundisha mengi lakini mwanadamu ni kiumbe wa ajabu sana. Jinsi alivyo kwa sasa ni kidogo sana ukilinganisha na uwezo alionao ndani yake. Hakuna hata binadamu mmoja duniani ambaye alishawahi kuuishi uwezo wake wote, wengi wanaishi chini ya viwango vyao na si kwamba hawawezi bali hawajajua maajabu ndani yao. Mungu alimuumba mwanadamu kwa upekee wa hali ya juu sana kiasi ambacho hata tunayoyaona yamefanywa na binadamu leo ni kiasi kidogo sana ukilinganisha na uwezo ulio ndani yake. Na ndio maana kila siku mambo mapya yanagunduliwa

Mwanadamu amebeba hazina kubwa ndani yake na wengi wanakufa pasipokulijua hili. Watu wengi duniani wanaishi chini ya viwango vyao, chini ya uthamani wao wamelizika na maisha yenye mapungufu na viwango vya chini na hawataki kuongeza uthamani wao. Ni kweli uwezo tunao ndani yetu lakini hatuwezi kuuamsha bila kutafuta jinsi ya kuongeza kitu ndani yetu kwa kujaribu kujifunza zaidi na zaidi.

Mwanadmu hutanuka kiuwezo na kiuthamani kulingana na jinsi anavyojiongeza. Kila kitu kwa mwanadamu kinawezekana, hakiwezekani kwa sasa kwasababu hajajiongeza kiuwezo ili kukifikia kile kitu kinachoonekana kana kwamba hakiwezekani kwa sasa. Maisha ya mwandamu ni mfumo wa kujiongeza kiuwezo, kiuthamani hakuna hata binadamu mmoja duniani ambaye hana kitu ndani yake, ni kweli anaonekana na kujiona kana kwamba hana kitu kwasababu hajajiongeza kiuthamani na kiuwezo.

Hata uwezo wa kiakili wa mwanadamu huongezeka kila siku kulingana na jinsi anavyojitanua, wengi wamesinyaa kiuwezo na hata kiakili kwasababu wamekubali mazingira yawafanye wasinyae, fursa zipo duniani kwa yeyote anayetaka kujiongeza thamani yake na kujitanua kiuwezo katika kuimba, kazi,biashara na huduma nyinginezo na kufika viwango ambavyo havikuwahi kuwepo duniani

Na ukitaka dunia hii ikukubali amua kuvunja rekodi au kuanzisha rekodi mpya ya kwako kwa kuamua kuwa zaidi ya viwango vilivyozoeleka, lakini yakupasa kujitoa na kuwa rekodi kwa kujitanua kiuwezo. Na hii huja kwa kujifunza zaidi, kusoma zaidi,kufanya mazoezi zaidi, kutafuta zaidi na kuishi zaidi.

Usijilinganishe na yeyote katika hili, kumbuka kuwa mshindani mkubwa katika maisha yako si yule unayefanana naye bali ni wewe mwenyewe, ukiweza kujishinda mwenyewe kwa kutanuka kuvuka viwango vyote kupitia uwezo wako wa kiupekee zaidi ndipo utaweza kuishi na kuongeza thamani yako maishani. Kuwa zaidi, ishi zaidi na ongeza thamani yako zaidi. Chagua kuwa zaidi, chagua kuishi zaidi, dunia ni yako, maisha ni yako na unaweza semea popote.

MUNGU IBARIKI TANZANIA
ASANTENI
By Geophrey Tenganamba
Kwa semina zaidi unakaribishwa siku ya tarehe 29/01/2012 jumapili saa tisa kamili pale Josam House Mwenge katika ofisi za K-Link International bila malipo.Maisha ni ya kwako na uamuzi wako. Kwa mawasiliano zaidi piga simu :0714477218 na 0755306799. Email:gtlivemore@gmail.com
source:http://www.treasurehousewithinyou.blogspot.com/

Categories:

Leave a Reply