"Tukubali ukweli kuwa Tanzania haiwezi kusogea kwa kubadilisha hali ya kisiasa tu peke yake, ila kwa kutambua kuwa kila mmoja wetu anayo nafasi yake kwa mfumo wake na anaweza kutengeneza maisha yake mwenyewe kwa msukumo wake wa ndani"
"KILA MTU ANAWEZA"
Safari mpya inaanza ni safari ya mwaka 2012. Mwaka wa Tanzania kutambulika,kuheshimika na kujivunia kuanzia leo. Yaliyopita yamepita na mambo yote ya kesho yanaanza leo. Hivyo basi, leo ni siku muhimu sana ya maisha yetu ya baadaye.. Ni siku ambayo tunaweza kuifanya Tanzania yetu kutambulika,kuheshimika na hata kujivunia.Na Watanzania ndio watakaoifanya Tanzania kutambulika,kuheshimika na hata kujivunia.

Tanzania haiwezi kutambulika wala kuendelea bila watanzania kwasababu Tanzania ni wewe na mimi. Tanzania ni ya watanzania. Tanzania haiwezi kuamka kama Mtanzania hajaamka Tanzania haiwezi kutembea kama mtanzania hatembei. Tanzania inaishi kwa sababu Watanzania wanaishi. Tukitaka kutambulika,kuheshimika lazima kwanza mtanzania abadilike ,na uwezekano huo upo.

Kila Mtanzania anacho kitu ambacho kinaweza kuifanya Tanzania ibadilike. Asiyejua ukweli huu ni muda muafaka wa kutambua hili. Ni ukweli kwamba nchi yetu imekumbwa na skendo za ufisadi na mambo mengine mengi ambayo si mazuri yaliyochangia na yanayozidi kuchangia sana kuirudisha Tanzania nyuma; lakini – pamoja na hali hii - ukweli utabaki palepale kuwa, Tanzania inarudishwa nyuma zaidi na mtanzania ambaye anaweza kufanya kitu, mwenye uwezo wa kuibadili nchi, lakini yupo kimya anasubiri yafanywe au yatokee.

Na hakuna binadamu mwenye dhambi duniani kama binadamu anayeweza kuleta mabadiliko, lakini badala ya kuleta mabadiliko yeye analalamika kwanini lile na hili halijafanywa. Ni fisadi wa mabadiliko na hana tofauti na mafisadi wengine . Mtu yeyote mwenye uwezo wa kuleta mabadiliko, na badala ya kufanya hivyo, anatafuta mtu wa kumlaumu ni fisadi anayezuia mabadiliko Tanzania! ..

Tunapoanza safari ya 2012, tuanze kuchukua hatua binafsi, mimi na wewe tukiamua ,lazima Tanzania ipige hatua. Tuache kusubiri kuletewa mabadiliko, tubadilike sisi kwanza. Tukubali ukweli kuwa Tanzania haiwezi kusogea kwa kubadilisha hali ya kisiasa tu peke yake, ila kwa kutambua kuwa kila mmoja wetu anayo nafasi yake kwa mfumo wake na anaweza kutengeneza maisha yake mwenyewe kwa msukumo wake wa ndani. KILA MTU ANAWEZA!

Na tukiujua ukweli huu hatutalala kusubiri mambo yatokee, hatutasinzia kusubiri Serikali fulani ifanye kazi, bali tutaanza kutembea, kujiendeleza, kujiandaa, kujiimarisha, kujiweka bora na kutafuta kuwa wataalamu katika kile tutakachochagua na mwishowe kuwa sumaku ya maisha mazuri; matokeo ambayo tutatambulika,tutaheshimika na kujivunia kwa kuwa itakuwa ni nguvu zetu wenyewe ambazo zimesababisha mambo yatokee, mengine yote yanakuwa ni ziada tu.

Safari ya kubadilika na kuendelea kwa Tanzania na maisha yake wakazi wake inaanza na wewe na mimi, na kama tusipofanya hivyo tujue tutasinyaa kiuwezo, kifikra, kiakili na kimwelekeo. Na maisha yetu yatasinyaa pia. Na tutakosa wa kumlaumu.Inabidi tufike sehemu tufahamu kuwa dunia hii itaendelea kuongozwa na wanadamu wanaoujua kweli ya kwamba; ‘maisha ya mwanadamu yanaanza na yeye mwenyewe’.

Mwaka wa 2012 utaongozwa na wanadamu walioamua kuwa wahusika wa maisha yao kila siku. Sawa; serikali ipo, familia ipo, marafiki wapo lakini maisha yako ni yako tu, kufaulu kwako ni kwako tu na usipoanza wewe maisha yako hayatabadilika hata ukilia kuwa kuna mafisadi wanakula mali za umma, au serikali ambayo haikurizishi, wazazi waliokulea kimaskini au wasiokujali – yote haya hayatakusaidia na kamwe hautaona mabadiliko mpaka ubadilike wewe. Ukibadilika wewe na Tanzania inabadilika pia.

Amua basi kubadilika wewe mwenyewe kulingana na jinsi unavyotaka mabadiliko hayo yatokee Tanzania. Na ukitaka mabadiliko kwa mwaka 2012 anza kwa kuyafanya yafuatayo:

Tafuta kujua malengo yako ya 2012;
Yaweke akilini, tengeneza picha ya jinsi utakavyokuwa kutokana na malengo hayo na panga kila siku ufanye nini ili kuyafikia. Na ikibidi yaandike. Uwezekano huo upo ukiamua.Na anza kuyafanya leo usisubiri kesho.

Tafuta sababu ya kupendwa na watu;
Jitengeneze kiasi ambacho utapendwa na kuzungukwa na watu watakaokusaidia kuyafikia uyatakayo na wafanye wafurahi kuwa na wewe.Wanaweza kuwa wateja wako,marafiki zako,waajiri wako,wafanyakazi wako,wasaidizi wako,ndugu zako,wafadhili au wadhamini wako,wafanyabiashara wenzako katika mahali popote ulipo.Fanya mambo ambayo yatawafanya wajue kuwa bila wewe yasingetokea. Uwezekano huo upo kwasababu wapo wengine wanafanya hivyo na tunawaona na kuwasikia,

Tunza muda wako;
Hakikisha kuwa unatumia muda wako vizuri. Ishi maisha kwa manufaa usipoteze muda duniani.Muda ndio maisha yako ya kuishi duniani, wengine wanaendelea amka na wewe ufanye kitu.

Acha kuishi na kufanya yaleyale;
Jifunze na fanya mambo mapya kila siku ambayo hujawahi fanya hata kama ni mapya duniano.Kumbuka kuwa dunia hii itabaki kuwa na mapungufu siku zote kama hutafanya cha kwako cha kipekee ulichonacho. Jisukume kwenda mbele na kuwa huru kuishi kimanufaa. Na jifunze kutafuta uwezekano katika kila kitu kwani kila kitu kinawezekana kwa atakayetafuta njia ya uwezekano.Fursa zipo Tanzania na hakuna nchi yenye fursa za kufanikiwa kama Tanzania amua kufumbua macho uzione, zipo hata ukibisha zipo.

Penda kufanya kile unachofanya;
Moyo wako, akili yako na mwili wako vikubali na kupenda kitu hicho hutachoka kufanya .Na lazima utasababisha kitu.

Kuwa msaada kwa wengine;
Acha kuwanyooshea vidole wengine wewe fanya kwa nafasi yako na kwa muda wako kwa kuwa msaada kwa wengine. KUMBUKA Tanzania inarudishwa nyuma na watanzania wanaowanyooshea wengine vidole wakati wao hawajafanya kitu chochote. Kuwa role model na mentor wa watu. Jitolee ikibidi. Ukifanya hayo lazima dunia itageukia upande wako.Na ukumbuke kuwa ipo nafasi duniani kwa binadamu atakayeamua kujitengenezea nafasi yake.

Kumbuka kuwa Tanzania haiwezi kutambulika bila wewe,haiwezi kuheshimika bila wewe na heshima ya Tanzania inaanza na wewe kimafanikio,kitabia,kiutamaduni,kielimu,kibiashara na kimtazamo. Jifunze kusema kuwa Tanzania ni yako na bila wewe Tanzania haiwezi kuitwa Tanzania. Mwaka 2012 ni mwaka wa Tanzania kutambulika,kuheshimika,kujivunia kwasababu ni wewe ndiye utakayetambulika,heshimika na kujivunia Utanzania kutokana na utakayoyafanya.

MUNGU IBARIKI TANZANIA. MUNGU IBARIKI AFRIKA.

Imeandaliwa na Temino clouds FM Team.

Napenda kuwashukuru sana: Sister Abella Bateyunga, Haris Kapiga na timu nzima ya maanisha na Clouds Fm kwa mchango wanaofanya wa kuibadili Tanzania kupitia Terminal clouds Fm. Mungu awabariki sana.
By Geophrey A. Tenganamba.
source:http://www.treasurehousewithinyou.blogspot.com/2012/01/2012-mwaka-wa-tanzania.html

Categories:

Leave a Reply