Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Limited, Reginald Mengi, amewataka wananchi, hususani wenye uwezo wa kipato kutumia sehemu ya mafanikio yao kusaidia kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo ili waweze kukumbukwa kwa mazuri waliyoyatenda ya kimaendeleo pindi watakapoondoka.

Mengi aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akiongoza harambee ya kuchangia upanuzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Nshara, uliopo Machame, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Harambee hiyo ilitanguliwa na ibada ya misa takatifu ya kumshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 50 ya kuzaliwa kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe.

Mengi alisema mara nyingi binadamu hukumbukwa kwa matendo yake mazuri aliyoyatenda kwa jamii na kwamba, mali na utajiri wake havimfanyi kukumbukwa.

Alimtaka kila mmoja kujiuliza sababu za kuwapo duniani na sababu za kuwa katika hali aliyokuwa nayo badala ya kuwa mwingine.

Alisema jambo hilo ni kwa upendo na huruma ya Mungu ambaye ndiye mtoa yote.

Katika mahubiri yake, Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini kati-Arusha, Thomas Laizer, aliitaka serikali iliyopo madarakani iache kufanya mambo ya kudhoofisha nguvu za vyama vingine vya kisiasa kunakoonekana wazi kuwa ni uonevu kwa wengine na badala yake itoe uhuru kwa vyama hivyo.

Alisema endapo serikali haitakuwa makini, amani ya nchi itatoweka kutokana na wananchi kutokukubali uonevu wa waziwazi.

Aliongeza kuwa endapo vyama vingine vya siasa vitaendelea kudhoofishwa na serikali iliyopo madarakani, uhuru wa miaka 50 hautakuwa na maana.

Alisema njia pekee ya kufanya masahihisho ni kuwa wakweli na wawazi kwa vyama vingine na kuongeza kuwa amani na utulivu vitakuwepo endapo haki itaendelea kutendeka.

Katika harambee hiyo, Mengi alichangia Sh. milioni 54 na mfanyabiashara maarufu nchini, Mustapha Sabodo, aliahidi kuchangia Sh. milioni tano wakati Mbowe alichangia Sh. milioni 20. Jumla ya michango yote, zikiwamo fedha taslimu na ahadi, ilifikia Sh. milioni 200.

CHANZO: NIPASHE

Categories:

Leave a Reply