Dear Mr. President it is my hope that you are okey. This is another letter for a President. A letter for a President is a voice of a man who has discovered the reason why he was born in Tanzania. It is a voice of a man who wanted to be a President but he discovered another GREAT purpose in life and he fallen in love with it. It is a letter of love in some form. It is a letter of expressing my true love for our nation and its citizens. It is a letter which shows that the highest justification for living is love in some form. If you live or leading people in any position and don’t love them it means you are not fit to lead and to live as well. It is a letter of great cause. It is a letter for a great change in Tanzania and beyond. Dear Mr. President I am aware that on 9th Friday is a day to remember, 50 years of independence in Tanzania. But since we got independence even if we may claim that there are some changes but still there are much to tell regarding life of many Tanzanians. I am aware that the fate of Tanzania belongs to Tanzanians and only developed Tanzanians develop Tanzania. AND I am sure that you are aware that Tanzania is the top beggar after Iraq, Afghanistan. Why this? How do you feel when you go in abroad and people say that this is the President of the top beggar country? Can’t we change this for the next 50 years to come? Dear Mr. President today I will not address this in English as I want to give this message to all Tanzanians, to all of your delegates to everybody, I want this message to reach everyone, I don’t know by which way but send this message to all Tanzanians. This message Mr. President is sensitive, I don’t know for your case but for me it is a sensitive message thus why I am writing it to you in Swahili, I am tired to be called the citizen of the top beggar country, I don’t know for other Tanzanians, I don’t know for your case but we must do something about this. My message is in Swahili and it goes like this: “MIAKA 50 YA UHURU NA UMASKINI WAPI TUMEJIKWAA NA NINI TUFANYE?”

Tangu tupate uhuru miaka 50 iliyopita maumivu ya umasikini na ugumu wa maisha kwa watanzania walio wengi imekuwa kama hali ya kawaida. Toka enzi za uhuru mwaka 1961 mpaka leo umasikini umepata umaarufu kwani umetapakaa maeneo mengi ya vijijini na mijini katika Tanzania. Tukirudi katika ukweli Tanzania si nchi masikini lakini watanzania ni masikini, Tanzania si nchi ya kilalahoi lakini watanzania walio wengi ni walala hoi, Tanzania si nchi iliyoishiwa lakini watanzania walio wengi wameishiwa, Tanzania imejaa ardhi yenye rutuba, bahari, mito, maziwa, misitu na mbuga za wanyama, madini, binadamu wengi wenye vipaji, akili, nguvu na uwezo na hali ya hewa nzuri lakini watanzania walio wengi ni masikini tena masikini sana.
Swali ni kwamba: Iweje tuishi katika nchi iliyojaa utajiri wa aina yake lakini bado ni masikini? Iweje tuishi katika nchi yenye maziwa na asali lakini tuendelee kula mchanga? Iweje nchi zisizo na ardhi wala utajiri kama Singapore ,Malaysia na nyinginezo zilizokuwa katika hali sawa sawa na Tanzania kipindi tumepata uhuru lakini zimepiga hatua kimaisha na zipo juu? Nchi nyingine zilizojuu kiutajiri zina nini zaidi yetu ambacho sisi hatuna? Viongozi Walioweza kuzifikisha nchi hizo huko juu wamefanya nini na wana sifa gani? Watanzania tumekosa nini mpaka tuendelee kuishi katika umasikini? Nani mchawi wetu katika nchi yetu jamani? Wapi tumejikwaa watanzania? Hii ni barua yangu na ujumbe wangu kwa watanzania.
Tukubali au tukatae wachawi wa maisha yetu ni sisi wenyewe na tupo hapa tulipo kwasababu tumejifikisha sisi wenyewe . Maisha tunayoishi yamesababishwa na sisi wenyewe.Tunajimaliza sisi wenyewe na hakuna mtu wa kumlaumu bali ni sisi wenyewe.Tunaweza kuibadili Tanzania kwa miaka hamsini ijayo sisi wenyewe kwani sisi ndio wahusika wakuu wa nchi yetu na ndio waharibifu wa nchi yetu pia.Tunaweza kusema kuwa Tanzania inamalizwa na mafisadi lakini kwa asilimia kubwa Tanzania inamalizwa na watu wanaoweza kufanya kitu kuyabadili hayo lakini wametulia tuli kana kwamba si watanzania au si binadamu wenye uwezo wa kufikiri.
Tanzania inamalizwa na watanzania walio kimya wanaoona maovu na kuyapuuzia eti kwasababu yanayofanywa hayawagusi wao moja kwa moja. Tanzania inaharibiwa na watanzania wanaoweza kufanya kitu lakini bado wamekaa chini wakisubiri mtu mwingine abadili hayo.Tanzania inamalizwa na watanzania hasa vijana wanaolalamika tu kila kukicha bila kuchukua hatua ya kuyabadili yanayowakela.
Watanzania tulikuwa na mategemeo makubwa sana baada ya kupata uhuru mwaka 1961 kwani hata mataifa ya ulaya yalitegemea kabisa kuwa Tanzania ingeendelea kwa kasi sana baada ya kupata uhuru kutokana na rasimali nyingi tulizonazo na watu waliokuwepo. Kufeli kwetu imekuwa ni mshangao kwa mataifa yanayojua utajiri wa Tanzania. Mimi ninakubali kuwa yapo matatizo yanayoikumba nchi yetu Tanzania, na nchi nyingine nyingi barani Afrika lakini ni nchi yetu pekee iliyo nyuma ukilinganisha na nchi nyingine ambazo tulifanana nazo kiuchumi. Huu ukweli usiopingika kuwa ni sisi wenyewe tunaizuia nchi yetu isisonge mbele kiuchumi, lazima ifike wakati tuchukue jukumu wote kwa pamoja kuanzia wakulima,wafanyakazi,wafanyabiashara,wanafunzi na wengine kuibadili Tanzania tunayoitaka iwe MIAKA 50 ijayo.
Mimi ninakubali kuwa Tanzania kuna tatizo kubwa sana katika uongozi, labda kwa njia moja au nyingine hatujawahi kumpata kiongozi anayeweza kuitoa Tanzania hapa ilipo,alikuwepo Nyerere na maono yake lakini alikata tamaa na kuyaachilia mbali. Sijui kwa labda kwa kutokuwa na maono makubwa kwa nchi yetu. Lakini sasa tumeshajua kasoro ya uongozi katika nchi yetu, si suluhisho kama tukiendelea kupiga kelele za lawama lazima tuchukue hatua kimatendo kuanzia katika kuishi kwetu mpaka katika kuchangia kwetu. Unajua imekuwa ni fasheni kwa wanasiasa wa Tanzania kutoa ahadi tamu na kujifanya wao ndio wahusika wa maisha ya kila mtanzania, lakini wakipewa nafasi ndio hao wanakuwa watalaamu wa kusoma ripoti na takwimu ambazo si halisi ukilinganisha na maisha ya watanzania walio wengi.
Ninavyojua mimi ni kuwa kama wanasiasa na viongozi wetu katika nchi yetu wangekuwa ni makini umasikini wa watanzania ungeisha ndani ya miaka mitano tu kwani tuna kila kitu cha kutufanya tufike mbali hata zaidi ya marekani.
Vilevile hatuwezi kuendelea kulaumu tu kama tunataka mabadiliko katika nchi yetu, Lazima watanzania tuchukue maamuzi na uhusika wa maisha yetu sisi wenyewe kwani sisi ndiyo wahusika wakuu wa maisha yetu,watu,mazingira na vitu vinavyotuzunguka vinaweza kubadilika lakini sisi ndiyo wenye uwezo wa kuamua vipi tufanye kulingana na mabadiliko hayo. Hivyo sisi ni wahusika kwa Tanzania yetu na maisha yetu lazima tuchukue maamuzi ya kuibadili Tanzania katika kuishi kwetu. Uwezo wa kuyafanya makubwa tunao, uwezo wa kufika mbali tunao na tunaweza semea popote. Tanzania hii itaendelea kuwa mapungufu siku zote na nchi yenye watu masikini wa kutupwa kama watanzania hatutaamua kuchukua maamuzi ya kubadilisha maisha yetu sisi wenyewe kwa kutumia akili, Imani, vipawa, nguvu na uwezo wetu wote.
Na hili jambo ni kuanzia wakulima, wafanyabiashara, wafanyakazi, wasanii na viongozi wote. Ni lazima tuamini kuwa tunaweza kuibadilisha Tanzania yetu. Mazingira yetu yanayotuzunguka kamwe hayawezi kutuzuia sisi kuyafikia malengo yetu na ni kosa kubwa sana kumlaumu mwingine au mazingira kuwa sababu ya sisi kuwa tulivyo sasa kwani tunaweza kuyabadili mazingira au tukishindwa kuyabadili basi tunaweza kubadilika sisi kulingana na jinsi tutakavyofaidika katika hayo mabadiliko tutakayoyasababisha kwani sisi ndiyo wahusika katika jinsi tunavyowaza, hisi, amini na kutenda. Ukweli tunaweza kuyafanya maisha yetu yawe yenye mafanikio kwa kila mmoja na kisha nchi nzima.Kama kweli hatutaki hali tuliyonayo leo ni muda muafaka leo kuchukua hatua tofauti kwa mbinu na njia tofauti, ili tupate matokeo tofauti.
Tanzania bila umasikini inawezekana, lakini haimaanishi kuwa ni rahisi lazima tuanze kubadilika sisi wenyewe, na vipaumbele viwe ni sisi wenyewe kubadilika katika kufikiri kwetu, kutenda kwetu, kusema kwetu, kuamini kwetu na kwa kuona uwezekano huo, kwa kuwa na picha kubwa ya mambo makubwa tunayotaka kuyafikia, ili hata kama hatutayafikia sisi vizazi vingine miaka hamsini ijayo vitaweza kuyafikia, hasa katika kubadilika katika kuishi kwetu ikibidi hata utamaduni wetu.
Nawaomba sana viongozi wajue kuwa nchi hii ipo hapa ilipo kwasababu kuna watanzania waliosababisha ikawa kama ilivyo hivi leo maisha yamekuwa hayana utamu kabisa wa kuishi ,tena kwa njia moja au nyingine na wao wamechangia ikawa jinsi ilivyo, tuache kudanganyana kwa kusoma takwimu ambazo si halisi kuhusu uchumi na maisha ya watanzania walio wengi.


Mimi ninasema kwa uhakika kabisa kuwa kila bindamu mtanzania hakuchagua kuzaliwa Tanzania, lakini aliletwa Tanzania ili afanye kitu fulani kikubwa sana katika maisha, imetokea tu kuwa wengi wetu wamelisahau hili au hawataki kujua kuhusu hili, hakuna binadamu ambaye yupo duniani ili kupoteza muda hapa, na wala hakuna binadamu ambaye yupo hapa ili kuchukua tu mali za wengine na kuleta madhara kwa binadamu wengine, lakini wengi wetu hasa viongozi wamekuwa wachukuaji tu, na hawa hawajui kabisa kwanini wanaishi.

Sawa unaweza kuendelea kujichukulia kodi za walala hoi lakini lazima utakufa tu na si chochote, lakini jambo baya sana kuhusu mchukuaji na fisadi wa walalahoi ni kuwa maisha yake hayana manufaa duniani na akifa duniani kutakuwa ahueni kwani kuishi kwake duniani ni sawa na sumu ya dunia.

Hivyo basi hapa duniani wapo binadamu wengine ambao ni sumu tu kwani hakuna walichochangia duniani, hata katika maisha na uongozi wao zaidi wamekuwa ni hasara kwa Taifa kwa wao kuwepo kwao duniani kwani hata ikitokea wanashika madaraka mambo yanakuwa magumu kama nini kutokana na mabaya wayafanyayo lakini Mungu yupo tu ambaye atayalipa kwaajili ya wanyonge duniani. NAOMBA HILI LIKUMBUKWE.

Watanzania lazima tuishi kwa madhumuni ya kuibadilisha Tanzania na watu wanaotuzunguka katika hali ambayo tutakumbukwa kama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ingawa alikuwa na mapungufu yake lakini aliweza kuyafanya yale ambayo kamwe taifa na dunia haitamsahau.Lazima tujiulize kuwa watu wanaishije na ; hapa tulipo tumefikaje? Wewe umechangiaje? Ufanye kitu gani tofauti leo? Tukumbuke kuwa sisi ni wahusika kwa Tanzania ya leo na Tanzania ya MIAKA 50 ijayo.


Jambo la pili ni kuwa hakuna watanzania wazalendo kabisa katika uongozi serikalini, makanisani, misikitini, makapuni na hata katika vikundi tofauti vya kijamii. Na hili jambo lipo wazi kabisa kwani kila mmoja anajua hili, na imekuwa kama utamaduni wa kila mtanzania, kama wapo wazalendo basi ni wachache sana . Tanzania ya leo tuna watu wengi waongeaji lakini si watendaji, Tanzania ya leo tuna watu wenye sura za huruma lakini si wenye utu hata kidogo, kutokana na hilo hata utendaji serkalini ni mbovu sana kwani hakuna anayeona umuhimu wa kuibadilisha Tanzania kiuchumi.
Wapo viongozi wanaopenda kusoma ripoti lakini si watendaji, kila siku tunasomewa ripoti lakini maisha ya watu wa chini yanazidi kuwa magumu, Na zaidi ya hayo hatuna viongozi wenye maono na wanaoendeshwa na maono ya uongozi, kama wangekuwepo viongozi wa aina hiyo basi skendo kama dowans, Richmond na hata rushwa ingekuwa ni historia katika nchi yetu. Jambo ambalo linaniuma sana ni kuwa wapo wale wanaokula kodi za walala hoi bila hata huruma wala aibu na kuwadharau hao hao wanaowafanya washibe, Jamani taifa letu linahitaji binadamu wazalendo na wenye upendo ili taifa libadilishwe.
Hebu tujiulize sisi wenyewe Tanzania ya leo nani ameifikisha hapa ilipo? Tuache kudanganyana kuwa kuna maisha bora hapa Tanzania, hakuna kabisa na hili jambo linajulikana kwa kila mtanzania anayeishi katika maisha magumu. Kazi kubwa ipo kwa viongozi katika kujenga mazingira mazuri kwa maendeleo ya Taifa letu. Viongozi wetu wamekuwa wakisema kila siku kuwa; tutafanya haya! Tutafika pale! Tutamaliza hili! Na imekuwa ni fasheni kwa viongozi wakubwa wa juu, Tanzania na Afrika nzima.Na ndiyo sababu nchi yetu haisogei popote kihalisia, lakini kitakwimu imepiga hatua.
Kwa kukosa uzalendo, upendo na utendaji mbovu katika serikali yetu, mali asili na utajiri wetu hauwafaidishi watanzania bali zinawafaidisha wageni na viongozi wachache wasiojua kwanini walipewa nafasi za kuongoza na hata sababu ya kwanini wanaishi. TANZANIA IMEKUWA KAMA SHAMBA LA BIBI. Huwa nashangaa sana kuwaona baadhi ya viongozi wa kitanzania wanapoimba wimbo wa: Tanzania nakupenda kwa moyo wote. Inawezekana vipi mtu uimbe wimbo kuwa unaipenda Tanzania kwa moyo wote wakati hujafanya kitu kabisa katika nchi, zaidi unachukua kila kitu kitakachosogea usoni kwako, wapi Tanzania ya watu wazalendo na wenye upendo?
Na simaanishi kuwa ni viongozi peke yake bali ni kila mtanzania ahusike katika hili, inatakiwa ifike muda ambao kila mtu awe na utu kwa binadamu mwenzake, si lazima tuwasubiri viongozi ambao na wao wana ugonjwa wa kukosa uzalendo, ikitokea kila mtu anaishi maisha ya aina hii basi tunaweza kuibadilisha Tanzania tunayoitaka.
Sisi sote ni binadamu na tupo duniani ili kuwa chumvi na mwanga kwa binadamu wenzetu, haijalishi kuwa ni wa kabila au dini gani ili mradi tu ni binadamu basi tunaishi kwaajili ya binadamu , uzalendo unahitajika Tanzania ili kila kiongozi afanye kwa nafasi yake. Inatakiwa ifike wakati kuwa kila kiongozi ajiulize kwanini ni kiongozi na kwanini anaishi, ili ajue ni kitu gani achangie Tanzania.
Mimi nasema ni bora binadamu aliyekufa kuliko Yule anayeishi lakini hajui kwanini anaishi, Tusiwe wachukuaji tu hapa duniani. Lazima tujiulize kuwa katika muda tulioutumia kuishi duniani tutakuwa tumechangia nini, sioni umuhimu wa kuwepo duniani kwa binadamu asiyechangia kitu Tanzania, Sioni umuhimu wa kiongozi fulani kuishi na kuongoza katika nchi kama hana anachochangia duniani.Kwanini mtu aendelee kuongoza wakati hata anachochangia hakionekani lazima ifike mahali watanzania tuwe wazalendo na watoaji pia.
Janga kubwa duniani si kifo bali ni maisha yaliyoshindwa kuyafikia malengo, hivyo ukiwa kiongozi wa nchi hata Rais basi ujue kuwa kushindwa kuyafikia malengo ya uongozi wako ni janga kubwa sana zaidi ya kifo chako, kwasababu kama ni kufa wote tutakufa tu lakini muda tulioishi duniani Tanzania tulifanya nini? Hili ni jambo muhimu sana tuliweke akilini. Mimi ninaamini ipo siku miaka hamsini ijayo umasikini kwa watanzania utaisha, na itakuwa ni ukumbusho ambao watoto wa vizazi vijavyo watakuwa wakienda maeneo tofauti ya makumbusho ya umasikini kwenda kuona jinsi gani watanzania walivyowahi kuishi katika umasikini ambao kipindi hicho ni makumbusho tu ya historia ya umasikini kwani kila mmoja atakuwa anafurahia mafanikio, lakini tukiamua iwe hivyo.
Jambo la tatu ni kuwa kuna tatizo katika maarifa, ujuzi na vifaa katika kutumia mali asili za nchi yetu. Na hili ni kutokana na kuwa Tanzania hii haina great thinkers kama wapo hawajapewa nafasi kabisa, na jambo hili linatokana na mfumo wa kufikiri kwetu, Watanzania wengi hawapendi kuumiza vichwa vyao ili kuweza kuleta mabadiliko. Watanzania hawasomi vitabu tena hata viongozi wao wana ugonjwa huo. Watanzania tunaweza kabisa lakini hatutaki kufikiri tofauti na kutumia vichwa vyetu.
Walio wengi hawana ajira na wanashuhudia mafanikio ya nchi nyingine, wengine wameajiriwa kwa ujira mdogo na hawataki kufikiri kuhusu uwezekano wa kufanya mambo makubwa zaidi ya hayo. Sasa nani ataibadilisha Tanzania kama sisi wenyewe wahusika hatutaki kuamua kuibaili kwa njia tofauti. Tanzania hii inahitaji mapinduzi ya maisha, uongozi na biashara na utendaji kwani kwa njia hii tunaweza kuifikisha Tanzania yetu mahali ambapo kila mmoja atajivunia kwa nchi yetu. Inabidi kila mtanzania aishi maisha ambayo laiti kila mtanzania ataishi maisha kama yake basi Tanzania hii itakuwa sit u kisiwa cha amani bali ni kisiwa chenye mafanikio kwa kila mtanzania.
Mwandishi ni Geophrey Tengananmba; mwandishi wa kitabu cha “kichwa chako ni dhahabu ya utajiri” , Nguvu ya kujitajirisha ndani yako na The richest Goldmine in you. Ni mwanamapinduzi wa maisha, mshauri wa maisha na biashara, mwanafalsafa aliye na maono ya Tanzania mwenye shauku ya mabadiliko. Kwa mawasiliano soma blog:www.treasurehousewithinyou.blogspot.com au piga simu : +255714477218 na email:gtlivemore@gmail.com
Thank You Mr. President
Sincerely,
GEOPHREY A . TENGANAMBA, The Great.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
AMEN
SEE YOU NEXT TIME FOR A LETTER FOR A PRESIDENT.

Categories:

Leave a Reply