Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalan
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu, amesema bidhaa zote zitakazoingizwa nchini kuanzia Januari mwakani zitakuwa zimekaguliwa zinakotoka na kuthibitishwa viwango vyake vya ubora vinavyostahili kabla ya kuingizwa nchini.

Alisema hatua hiyo inatokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa yanayohusika na ukaguzi wa bidhaa kwamba, kuanzia Januari Mosi mwakani bidhaa zitakazoingizwa nchini zitakuwa zimekaguliwa na kuondoa kabisa sokoni bidhaa zilizo chini ya viwango.

Msimamo huo wa serikali ulitolewa jana jijini Dar es Salaam wakati Nyalandu alipokuwa akifungua semina iliyoandaliwa na Shirika la Viwango vya Bidha (TBS), iliyowakutanisha wadau mbalimbali kujadili masuala yanayohusu viwango vya ubora wa bidhaa. Alisema mpango huo wa kukagua bidhaa zinakotoka kabla ya kuingizwa nchini utasaidia kuondoa sokoni bidhaa zote zilizochini ya viwango vya ubora wa kimataifa na itasaidia kumlinda mlaji na mtumiaji.

Alisema serikali imeamua kutumia njia hiyo ya ukaguzi wa bidhaa kabla ya kuingizwa nchini ili kukabiliana na uingizaji wa bidhaa zote zilizo chini ya viwango.

Nyalandu alisema mfumo huo wa kukagua bidhaa kabla ya kuingizwa nchini pamoja na mambo mengine, utasaidia kuongeza ajira kwa vijana na wafanyabiashara watafanya biashara zilizo na viwango na kukwepa kupata hasara ya kunyang’anywa na kuteketezwa mali zilizo chini ya viwango. Naye Mkurgenzi wa TBS, Charles Ekelege, alisema ukaguzi wa bidhaa kufanywa zinakotoka utasaidia kulinda mazingira kwa kuwa awali shirika hilo lilikuwa linateketeza bidhaa zilizokuwa chini ya viwango kwa kuzichoma moto.

Miongoni mwa nchi zinazotumia mfumo huo ni, Kenya, Nigeria, Ethiopia, Zambia na Ghana.

CHANZO: NIPASHE

Categories:

Leave a Reply