Ndugu yangu mdau kama nilivyoahidi kuwa kila weekend nitajitahidi kufanya mahojiano na mtu ambaye amafanikiwa au ambaye anaelekea kufanikiwa,pia kukuletea historia ya mtu ambaye amefanikiwa.
Leo ninapenda kukuletea historia au mahojiano ya ndugu Chinary Herman Kojo a.k.a Bill gates wa Ghana kwa mujibu wa BBC.
Mfanyabiashara wa Ghana Herman Kojo Chinery-Hesse, hujulikana kama Bill Gates wa Ghana,na ni wa kwanza kutajwa katika mfululizo maalum wa vipindi vya BBC "African Dream" yaani ndoto ya Afrika ambavyo vinaangaza wajasiriamali wa bara la Afrika.
Kampuni ambayo Bw Chinery-Hesse aliibuni kwa ushirika miongo miwili iliyopita , SOFTtribe Limited, huenda ikawa haijajitanua duniani kama ile kampuni ya Microsoft lakini imeimarika na kuwa mojawapo wa mashirika makubwa ya programu za kompyuta katika Afrika ya Magharibi.
"siku zote nilitaka kuwa mjasiriamali . Nikidhani ndio njia muwafaka ya kuiendeleza Afrika na kujitajirisha ," ameiambia BBC.

Bw Chinery-Hesse alisamehe fursa ya kujiendeleza kimaisha nchini Marekani alikosoma au Uingereza ambako aliwahi kufanya kazi kwa miaka michache ,na badala yake kuamua kuanzisha biashara nchini Ghana.
Alianza kuandika programu za kompyuta chumbani alikolala katika nyumba ya wazazi wake katika wakati ambapo sio watu wengi walitambua umuhimu wa mapinduzi ya kompyuta barani Afrika.

"ilikua ni vigumu sana. Sikutaka kurejea ng'ambo kwa sababu kugeuzwa kuwa raia wa daraja la pili si kitu ambacho kilinivutia," alisema.
Kampuni yake hatimae ikaanza kuunda programu za kompyuta za uongozi wa biashara na sasa ina zaidi ya wateja 250,mkiwemo mashirika kadhaa ya kimataifa kama vile Ford Foundation, Nestle, na Unilever.

SOFTtribe Limited pia ni mshirika wa maendeleo wa kampuni ya Microsoft katika kanda.
"imekua kama burudani. Si rahisi lakini si kusema haiwezekani. Sidhani kuwa mimi ni mtu mwenye kipaji. Nadhani mtu yeyote anaweza kufanya hayo awe makini na awe tayari kusubiri miaka. Mbinu niliyotumia ni kwamba nilijihusisha katika biashara nikiwa sitarajii kuwa tajiri katika kipindi cha miaka 2 ," Bw Chinery-Hesse aliiambia BBC.

"wakati fulani kwa kipindi cha miezi sita kampuni yetu haikupokea hundi zozote na ilitulazimu kugawana kiasi kidogo cha pesa tuliokua nazo. Kulikua na nyakati ambapo hatukua na fedha zozote kulipa mishahara wakati tulipokua na madeni."
Kwa maoni yake miongoni mwa vitu viwili muhimu katika biashara ni ustahamilivu na uaminifu .

"Katika biashara yoyote;lazima uamini kwamba inanufaisha kote kote. Mtu anaenunua lazima anufaike na wewe pia lazima unufaike,la sivyo haitaendelea ."

Hapana shaka Mojawapo wa sababu za kufanikiwa kampuni yake ni kwamba kuanzia mapema sana aliamua kubuni programu ya kompyuta ambayo imetengenezwa mahsusi kwa mazingira ya bara la Afrika.

"nadhani kuna fursa kubwa sana barani Afrika,hali ya umasikini mkubwa,kuna mengi ambayo hayakufanywa ;lakini hii si sayansi ngumu,ukiwa na nidhamu,usiogope kujitosa. ," Bw Chinery-Hesse anawaambia wengine wanaozingatia kua wajasiriamali.

"inawezekana , na nadhani ingewapasa watu wengine kufanya hivyo, na kama hatutajichukulia hatua ,basi wageni watakuja Afrika kama tunavyoona na watafanya wakitakacho"
African Dream hutangazwa na kipindi cha BBC Network Africa kila Jumaatatu. .
Kila wiki mfanyabiashara aliyefanikiwa ataeleza jinsi alivyoanza na funzo gani wengine wanaweza kulipata kutoka kwake.

Chanzo: http://www.bbc.co.uk/swahili/habari/2011/09/110912_biashara-makala.shtml

http://softtribe.com/

Categories:

Leave a Reply