Vijana wametakiwa kujiamini na kutumia fursa mbalimbali kuonyesha vipaji vyao ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.
Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na wanafunzi 29 kutoka shule mbalimbali za sekondari wanaoshiriki mchakato wa kujiunga na chuo cha kimataifa cha uongozi (ALA), kilichopo Afrika Kusini.
Mengi alisema vijana wanapaswa kuwa na kiu ya kufanikiwa kuliko hata watu wanaowaona kama ndio mfano wa kuigwa.
“Kujiamini na ujasiri ndiyo nguzo muhimu, unapoamini kwamba huwezi kufanya jambo fulani unashindwa kwa sababu akili yako inakujengea mazingira ya kuamini kwamba huwezi…lakini ukiamini unaweza kufanya kitu, akili yako inakuwezesha kufanikisha lile unaloamini, epuka kabisa hofu maana ndiyo adui wa mafanikio,” alisema.
Mengi alisema watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa kuhofia kufanya maamuzi “na ukisharuhusu hofu unajitengenezea sababu nyingi…unajiona labda mimi ni mdogo, maskini au mzee na hatimaye unashindwa kufanya maamuzi,”alisema
Aliwakumbusha vijana hao kuwa kipaji cha uongozi huonekana mapema tangu utoto na kwamba ili kufanikisha ni kuendeleza ndoto hiyo kwa kuwa na dira na mtazamo chanya.
Alisema kiongozi hapaswi kuona matatizo isipokuwa anatakiwa kuyatazama kama changamoto anazoweza kuzitatua.
Aliongeza kuwa vijana wanatakiwa kuwa na macho yanayoweza kuona fursa mbalimbali na kuzitumia kujiletea maendeleo.
Akitoa neno la shukrani, Mkurugenzi wa ALA, Annelene Fisher, alisema lengo la chuo hicho ni kutafuta wanafunzi kutoka nchi mbalimbali za Afrika na kuwaandaa kuwa viongozi bora wa bara hili.
“Tunataka kukuza akina Nelson Mandela, Ellen Johnson Sirleaf na Bill Gates wa Kiafrika,” alisema Fisher.
Julius Shirima ambaye alihitimu ALA mwaka jana, alisema elimu ya Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa kwa kuwa mfumo wa kusoma unaelekeza zaidi kukariri kwa ajili ya mitihani badala ya kujiandaa kimaisha.
CHANZO: NIPASHE :: IPPMEDIA

Categories:

Leave a Reply