WAKATI huu biashara si lelemama hata kidogo, ni wakati wa kujipanga na kujiweka vyema, kuangalia jinsi tutakavyokuza uchumi wetu bila kusubiri kuajiriwa.

Watanzania walio wengi wanapohitaji kuanzisha biashara huanza na mtaji mdogo kutegemea na kipato kwa wakati huo. Hivyo biashara inapokuwa ndogo inahitaji nguvu za ziada ili kufikia mafanikio makubwa kama waliyonayo wafanyabiashara wakubwa kama Reginald Mengi na Said Bakhressa.

Hakuna mfanyabiashara aliyeanza na mafanikio makubwa, wala hakuna aliyekwenda kwa mganga, bali kila mmoja ameanzia chini na baada ya kuweka nia na jitihada alipata mafanikio.

Watanzania tulio wengi tunashindwa kufikia kilele cha mafanikio kwa sababu ya kutokuwa na mbinu muhimu za kibiashara, wengi wetu tumebaki na kasumba ya kusema, kabila fulani ndiyo wanaoweza biashara. Kwa mfano, Wahindi au Wachaga, lakini kumbe kila kiumbe ana uwezo wa kufanya biashara na ikawa yenye mafanikio makubwa.

Mjasiriamali mdogo anahitaji kutengeneza mtandao wa kijamii katika biashara. Hili ni jambo linalofanywa na makampuni hata yakafikia mafanikio makubwa. Mbinu hizo hutakiwa pia kufanywa na wajasiriamali wadogo ili waweze kwenda juu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wajasiriamali Wanawake Tanzania, Dina Bina aliwahi kusema: “Kutengeneza mtandao ni njia kuu ya kuuza biashara, kuwashirikisha ndugu, jamaa na marafiki katika biashara yako kutawafanya waitaje pale wanapokuwa.”

Kwanza kabisa, mjasiriamali mdogo anahitaji kuwa na uhusiano mzuri na watu au wateja, kila mmoja anajua kuwa biashara ni watu, na watu wenyewe ni hao wateja watakaokuja kununua bidhaa zako. Kama hakutakuwa na uhusiano mzuri kati yako na hao wateja wako, ni dhahiri kuwa biashara hiyo itakosa wateja.

Kauli nzuri na wateja vizuri kutawafanya wawe wawazi kwako na kutawaweka karibu na wewe kwa sababu ya mahusiano mapya mazuri.

Baadhi ya wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga, wamekuwa na tabia ya kukera. Hao ni wale ambao mteja anapohitaji bidhaa kutoka kwao na ikatokea kutoelewana katika bei hutoa maneno ya kashfa au dharau kwa mteja. Matokeo yake ni kuwa siku nyingine mteja yule hatakwenda tena kwake kwa kuhofia maneno ya kashfa. Tayari ameshapoteza mteja mmoja.

Si jambo la ajabu kwa Wamachinga kufanikiwa kibiashara na kuwa milionea, lakini watakaovuka ni wale watakaofuata kanuni bora za biashara pamoja na kujenga mahusiano mazuri kwa wateja wake.

Jambo jingine ni kufanya uchunguzi kwanza kuhusu biashara yako. Kwa mfano, muuza vitumbua, kabla ya kupika anahitaji kufanya uchunguzi kujua wateja wanapenda nini na wanachukia nini.
Kufanya uchunguzi kutamfanya mjasiriamali kutengeneza au kuuza bidhaa kutokana na matakwa ya wateja. Lakini bila kufanya uchunguzi, upo uwezekano wa kulimbikiza bidhaa zisizo na wateja kwa sababu hujui wanapenda nini.

Uchunguzi huu, si kwa bidhaa peke yake, bali hata eneo linalofaa kufanya biashara na lenye wateja wengi. Mawasiliano ni jambo jingine muhimu kwa mjasiriamali mdogo hadi mkubwa, bila mawasiliano wateja hawataweza kuujua uzuri wa bidhaa zako kwa sababu watu hutaka kujaribu kile walichokisikia.

Habari mpya inapokuja na kurindima masikioni mwa watu huwafanya wapate hamu ya kuujaribu uzuri wa bidhaa husika. Hapo ndipo tunapoona umuhimu wa mawasiliano katika biashara.

Iwe ni matangazo kwa vibao, kwa mdomo, kwa ujumbe katika simu au vyombo vya habari, alimradi idadi fulani ya watu iwe imepata habari kuwa kuna bidhaa hii na hii na ina ubora huu na huu. Biashara bila matangazo ni sawa na kuifunika taa ya kandili kwa kapu.

Kuna biashara ambazo hazionekani kwa urahisi mpaka zitangazwe. Kwa mfano, wafugaji wa kuku wa majumbani. Hakuna atakayejua kuwa kuna kuku wa biashara bila ya kuweka kibao au tangazo, linalosema: “Tunauza kuku hapa”. Kufanya hivyo kutakuletea wateja bila kutumia nguvu.

Kuipenda biashara yako na kuifurahia ni njia nyepesi ya kuifanikisha. Kama unaipenda biashara hiyo ni dhahiri utafanya juhudi za kina kuhakikisha inayafikia mafanikio. Ukiwa unafanya biashara usiyoridhika nayo au inayokukwaza ni vigumu kujitumikisha ili kuifanikisha.

Mmiliki wa Kampuni ya BeautiesontheGo, Gabriel Chavez anasema: “Biashara huweza kukuendea vizuri na ina uhuru, lakini kuna wakati unakumbana na vikwazo, wakati kama huu unahitaji kufanya uchunguzi na kubadilisha hiki na kile. Pamoja na hayo, uwe na furaha na kile unachokifanya, ukichukia biashara yako na wengine hawataipenda kamwe.”

Biashara mpya hukosa mustakabali mzuri mwanzoni, hivyo basi mjasiriamali mdogo anahitaji kujiweka tayari kukabiliana na hasara. Ajipange kuzikabili hasara hizo na aweze kusonga mbele. Siku zote, kulikimbia tatizo ni tatizo zaidi kuliko kuitatua tatizo.

Kinachohitajika ni ustahamilivu tu. biashara changa huweza kukukosesha usingizi, kukumalizia akiba, lakini inapofikia kilele cha mafanikio ni mafanikio kweli kweli.

Mjasiriamali mdogo anapaswa ajue kupanga bajeti ya fedha zake. Fedha za biashara zisiingiliane na za matumizi. Kwa mfano, unga wa dukani usitumiwe kwa matumizi ya nyumbani bila utaratibu. Kama utatumika basi ni kwa kununuliwa kama wafanyavyo wateja wengine. Watu wengi hawajui kuwa Sh50 katika biashara ni fedha nyingi.

Wajasiriamali wakumbuke kuwa kufilisika kwa biashara yako ni sawa na moto uchomao dhahabu, kwa sababu dhahabu haing’ai mpaka ipite katika moto hivyo huhitaji kukata tamaa. Inuka tena na uendelee. Makosa siku zote ni sehemu ya kujifunzia kwani penye makosa pana makosa

Categories:

Leave a Reply