Home

Mahusiano Ya Manyanyaso/Abusive Relationship

Mahusiano ni moyo wa maisha, mahusiano hutupa sababu ya kuishi. Kila mwanadamu anahitaji maisha yenye afyana yaliyo na mahusiano mazuri na wengine. Mwanadamu ni kiumbe ambaye maisha yake yameunganishwa na maisha ya wanadamu wengine. Kila mwanadamu anatuhitaji sisi sote na sisi sote tunamhitaji kila mwanadamu. “Each of us need all of us and all of us need each of us” / I am because we are. Furaha ya maisha na maumivu yake huja kutokana na mahusiano yetu. Katika maisha kila mwanadamu anapitia maumivu yake,majaribu yake na mazuri yake kutokana na mahusiano yake na watu walio karibu yake. Wapo wanaoishi maisha ya furaha na wapo wanaoishi maisha yenye machungu kutokana na watu walio karibu yao. Wengi wanaishi maisha yenye maumivu kutokana na mahusiano ya manyanyaso kupitia wapenzi wao, wake zao na waume zao. Mahusiano ya manyanyaso ni pamoja na Unyanyasaji wa kimwili kama vile kupigwa,kulazimishwa kufanya mapenzi,kubakwa na mtu aliye karibu kama rafiki, mume au mke na Unyanyasaji wa kihisia ni kama kuonewa,kutukanwa,kusimangwa,kutishwa,kufeheshwa,kusalitiwa na kudhihakiwa. Unyanyasaji wa kihisia ni hatari zaidi kuliko unyanyasaji wa kimwili kwani huacha makovu yasiyoonekana moyoni , kama wasemavyo wahenga - “Jeraha linaweza kupona mapema kuliko tusi”. Manyanyaso ya aina yoyote si jambo la kulichukulia kimzaha, kwani madhara yake ni makubwa. Manyanyaso majumbani, hutokea mara kwa mara pale mtu mwingine anapojiona ni bora kuliko mwingine kimahusiano kwa kujaribu kumtawala mwingine au kumdhibiti kama anavyofuga wanyama wake, mahusiano ya aina hii ni mabaya na hayatakiwi kukubalika kabisa. Katika mahusiano ya kimapenzi , mara nyingi hutokea mmoja kumnyanyasa mwingine kimwili na hata kihisia kwa kuangalia umri wake, uchumi wake, kabila na hata jinsia yake Na katika hili wanawake huwa ni wahanga na wanaoumia zaidi. Hata wanaume pia hunyanyaswa hasa kwa maneno makali, vijembe na hata wakati mwingine kimwili kutoka kwa wapenzi wao. Ikumbukwe kuwa kila mwanadamu ni wa thamani, anahitaji kuheshimiwa na hata kuthaminiwa. Kama wewe upo katika mahusiano ambayo ni chanzo cha kila unyanyasaji tafadhali tafakari zaidi kuhusu uhalali wako wa kuwa mwanadamu huru. Na kama wewe ndio mnyanyasaji kumbuka kwamba mwenzako pia ni mwanadamu, kumtendea vibaya kwa njia yoyote iwe kimwili,kihisia na hata kisaikolojia si haki na wala si utu hata kidogo. Kamwe usimpuuzie wala kumnyanyasa mtu anayekupenda kwani ipo siku utaamka kutoka usingizini na kukuta umepoteza dhahabu ya thamani wakati ulikuwa busy kuhesabu mawe. Kumbuka kumjali na kumheshimu umpendae ; kamwe usimnyanyase kwani ukimpoteza itakugharimu sana. Wanaume au wanawake wa kweli, halisi na wakamilifu huwa ni wenye upendo na kamwe si wanyanyasaji. Hawana muda wa kutafuta wapenzi wengine wapya kwani wapo busy kutafuta njia mpya ya kudumisha upendo wao. Kumbuka kuwa Upendo wa kweli haufi bali huzidi kukua siku hadi siku. Ni kweli Katika mahusiano, kuna mengi ya kujifunza. Baadhi ya watu watakuja kukujaribu, wengine watakuja kukutumia, wengine watakuja kukufundisha na zaidi ya yote wengine wataaamsha uwezo wako ulio ndani yako na utakuwa bora zaidi, lakini hata siku moja usikubali kuumizwa katika mapenzi kiasi cha kukudhuru kihisia,kisakolojia na nhata kimwili. Kama wewe ni mhanga wa mahusiano ya manyanyaso, jifunze kuwa maisha yanaendelea, hata kama umepitia maumivu ya aina gani maisha bado yanaendelea na kesho yako njema bado ipo . Jambo kubwa na muhimu la kufanya ni kutoka katika manyanyaso hayo kisha tengeneza mahusiano mazuri na wewe mwenyewe, jipende,jikubali na songa mbele,kamwe usikate tamaa na fahamu kwamba kuwa peke yako haimaanishi kuwa wewe ni mpweke, mpende sana binadamu unayekuwa naye ukiwa peke yako. Ndugu zangu, tuanze kuishi maisha ya kuheshimiana kwa kuwa na mahusiano mazuri katika dunia hii yenye majaribu na maumivu ndani yake. Tunaweza sote katika familia zetu, tunaweza sote katika mapenzi yetu,tunaweza sote katika urafiki wetu na tunaweza sote katika jumuiya zetu. Sisi sote ni ndugu, jamii moja,damu moja tumetoka sehemu moja na tunaenda sehemu moja. Tusinyanyasane – tupendane. MUNGU IBARIKI TANZANIA,MUNGU IBARIKI AFRIKA. By Geophrey Tenganamba,Director&Founder of Perfect Path Innovators, www.ppi.co.tz and www.treasurehousewithinyou.blogspot.com , gtlivemore@gmail.com

No comments:

Post a Comment