Home
▼
FIKIRI UWE TAJIRI sefemu ya 2
UMEKUWA ukiruhusu mawazo yako kuwa kizuizi cha mafanikio yako? Kwa kuwa na mawazo hasi, mawazo ya umaskini, ukabila, wasiwasi au woga? Kama ndivyo, badilika. Chukua muda kila siku kufikiria, kuchuja na umakini katika mipango yako unayoipanga. Utaona kuwa fikra zako zina nguvu pamoja na kukua. Kila unapoendelea kufikiria, ndipo mipango yako inapoimarika. Baadaye, utafanikiwa na kuwa mtu mwenye maendeleo.
Kumbuka mawazo ndiyo mwanzo wa mafanikio yako. Unapokuwa na ndoto ya mafanikio kwanza yakupasa kuwa na wazo lako ambalo baadaye unatakiwa kulifanyia kazi, ili utengeneze bahati yako. Kwa kufuata maelekezo hayo utakuza upeo wako.
Ota ndoto kubwa. Wengi wanaweza kukupotosha kutokana na utajiri wa malighafi ulionao na kukudanganya kwa njia nyingi, lakini hakuna mtu anayeweza kukupotosha katika msimamo na kutumia fikra zako.
Wengi wanaweza wasikutendee haki, kama wengi wafanyavyo, wanaweza kukupotosha katika uhuru ulionao, lakini hawawezi kukuchukulia mawazo unayoyawaza. Kutokana na fikra zako utakuwa unashinda siku zote. Unataka kuwa na furaha? Unataka kuwa na amani? Unataka kuwa na cheo, nguvu au utajiri? Fikiri kuwa navyo, utafanikiwa.
Fikra unazowaza ni muhimu kuliko ujuzi ulionao. Ujuzi una mipaka, mawazo yanatawala muda wote, yanaleta maendeleo. Kila mtu binafsi anakuwa na ndoto za mafanikio bila kujitambua. Kwa mfano, wazazi wanapopanga ni jinsi gani watawaendeleza watoto wao, wajasiriamali wanapopanga ni jinsi gani wataendeleza biashara zao hiyo yote ni mifano ya kuwa na ndoto njema ya mafanikio.
Watu wachache wamejifunza kutumia mawazo yao kwa faida lakini wengi wetu mawazo tuliyonayo yanapata kutu kutokana na kutoyafanyia kazi. Hakuna sababu ya kuona aibu katika dunia ya ubunifu.
Kuwa na mawazo ya kufanya jambo fulani ni kitu kizuri katika dunia hii tunayoishi. Kila mmoja wetu ana kiwanda chake cha kuwa na mawazo. Lakini ni wapi mawazo hayo yanapotoka? Ni wapi waandishi, wana sayansi na wabunifu wanapopata mawazo makubwa? Kwa nini baadhi ya watu wengine wanakuwa wabunifu zaidi ya wengine? Ni kutokana na kutumia vizuri mawazo yao.
Kila mmoja wetu, kwa wakati mmoja au mwingine, lazima kujifunza chanzo halisi cha mawazo. Utajiri, unaweza kuupata, inategemeana na ulivyoyaweka mawazo yako. Wazo dogo rahisi linaweza likabadilisha kabisa maisha yako uliyonayo. Pia huwezi ukajua ukubwa wa mafanikio yako mpaka utakapojifunza jinsi ya kuchanganya juhudi zako na mawazo yako. Kwa vyovyote unapotaka mafanikio unajitathmini wewe mwenyewe.
Mwili uliopumzika una nguvu, vile vile akili. Kama unataka kuwa mbunifu na mpokeaji wa mawazo mapya, inakubidi kupata muda kwa mawazo hayo na kuyafanyia kazi.
Jizoeze kila siku kuwa na muda wa mapumziko, chagua chumba kizuri kilichotulia au kiti kizuri ambacho kitakusaidia kutuliza akili kwa urahisi. Unavyoendelea kujifunza kupumzika, utapata mawazo ambayo yatakufikisha katika malengo na matarajio yako.
Mtunzi anafikiri juu ya uimbaji, mchoraji anafikiri juu ya rangi, mwandishi anafikiri juu ya habari na maneno. Kama utachukua wazo moja na kulitendea kazi litakupa matokeo mazuri. Yafanyie kazi mawazo yanayokujia. Kuwa na utayari katika kunasa mawazo yako. Mawazo mengi mazuri yanapotea kwa sababu hayawekwi kwa maandishi.
Tathmini mawazo yako. Mara tu unapomaliza kuyachuja mawazo yako, unachagua yale unayotaka kuyafanyia kazi. Utagundua kuwa nayo yanahitaji kuongezewa ubora wake. Jifunze kutokufunga milango yako ya kuwa mbunifu.
Ni jambo lisilowezekana kati yetu kuwa kinyume na ujuzi tulionao. Mfano mtu hawezi kupita mbele ya gari liendalo kasi kwa kuwa anajua kuwa ataumia, hawezi kuogelea baharini kama anajua kuwa atazama, hawezi kuwa mstari wa mbele katika jambo la hatari kama anajua kuwa atadhurika.
Mafanikio hayahitaji kuwa na kiasi kikubwa cha ujuzi juu ya jambo fulani, lakini unatakiwa kung’ang’ania ili uweze kupata mafanikio hayo kwa ujuzi wowote ulionao.
Mkulima mmoja aliyejulikana kwa jina la Walter na ambaye siku za usoni angependa kuwa mchezaji bora wa mpira wa miguu, alimuuliza rafiki yake kuwa amewezaje kupata sh milioni 10 katika kazi yake anayoifanya kutokana na ujuzi alionao na kuweza kushinda kila dhana ya kushindwa ambayo ilikuwa inaibuka katika utendaji wake?
Rafiki huyo alimjibu kuwa wakati anaanza, alijua anataka kufanya nini na anachotarajia kukipata. Alikuwa na njozi iliyomwezesha kujenga picha katika mawazo yake kulingana na malengo aliyotaka kuyafikia katika maisha yake. Hivyo hiyo ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika maisha yake.
Walter alisema kuwa kuna wakati alisikia umati wa watu ukishangilia katika mawazo yake. Kuna wakati alijenga picha ya sherehe ya kupewa tuzo iliyojaa waandishi wa habari za michezo, wageni na wanamitindo mbalimbali. Ndoto hiyo sasa ameanza kuifanyia kazi, hivyo anaamini atafanikiwa kama rafiki yake huyo alivyofanikiwa.
Inaonyesha watu wengi wamekuwa hawako tayari kutulia na kufanyia kazi ndoto zile wanazokuwa nazo, kwa kuzipa nafasi ndogo katika utekelezaji wake.
Kuna mamilioni ya watu ambao wanaamini wanaangamia kwa umaskini na kushindwa kwa sababu baadhi ya malengo waliyonayo wamekuwa hawawezi kuyafanyia kazi. Bila kujua watu wengi hujitengenezea mazingira mabaya kutokana na mawazo hasi ambayo yanachukuliwa na mawazo na kutafsiriwa kwenda katika vitendo.
Kama mwanamume au mwanamke ambaye amejenga katika mawazo yake utajiri na mafanikio na akafikia mafanikio hayo, ni hivyo pia kwa Wamarekani weusi ambao waliikabili meza ya kushindwa kwa maisha kwa sababu mawazo yao yalikuwa yamejenga picha ya umaskini, bahati mbaya na kushindwa. Lakini kwa sasa Wamarekani weusi hao wamepata mafanikio.
Kwa sasa hivi utaweza kutambua kwamba mawazo ni vitu ambavyo vikifanyiwa kazi vizuri na kutekelezwa vinaweza kuwekwa katika mfumo wa uhalisia. Kama utakuwa na njozi za kupata zaidi na ukazijengea picha hiyo bila kujali utakumbana na vikwazo gain, hiyo itakuwa ni vipaumbele katika maisha yako.
Kama utaruhusu picha ya namna hii kuwa ya kudumu katika ulimwengu wako wa mawazo; utafikiri mawazo ya mafanikio na kuzungukwa na watu wenye mafanikio watakaotia moyo njozi zako.
Utatenga sehemu ya kipato chako kwa ajili ya kujilipa wewe mwenyewe, moja ya hatua muhimu katika kupata utajiri. Utajihusisha katika mpango ambao unaleta mafanikio binafsi na kukufanya uchague lengo la maisha yako.
Pia utatafuta ujuzi na utaalamu kwa wale wote ambao wamefanikiwa. Mwishoni utafanikiwa licha ya kukumbana na vikwazo katika kutekeleza njozi zako.
No comments:
Post a Comment