Home
▼
ACHILIA MBALI KUSHINDWA KWAKO, SONGA MBELE
KUTOKANA na uzoefu uliopo, unaweza kuelezea hali ya kushindwa katika njia nzuri ambayo itasaidia badala ya kuumiza. Kwanza usiruhusu mawazo ya kuvunja moyo kutoka kwa watu wengine, ambayo yataendelea kukukatisha tamaa katika maisha.
Wenye mawazo hasi wanasema kuwa kushindwa ni aibu. Kushindwa kunakuwepo wakati mtu anaposhindwa kufanikiwa, kushindwa ni yeyote anayeshindwa, kushindwa ni mwisho na jumla ya mambo yote. Zote hizo ni fikra duni. Usiamini mawazo hasi.
Kuna mambo manne ambayo unatakiwa kuyajua juu ya hali ya kushindwa.
Kushindwa si kushindwa kabisa. Unaweza ukawa umeshindwa hapa na pale, au katika maeneo fulani, kamwe usiruhusu nafsi yako kuamini kuwa wewe ni mshindwa. Umekuwa ukishindwa katika maeneo mbalimbali ya maisha. Maisha ni muhimu zaidi ya mambo machache yanayokutokea. Lenga umakini wako katika mafanikio kuliko kushindwa.
Hakuna mtu aliyezaliwa kuwa wa kushindwa. Pasipokuwa na malengo hautaweza kufanikiwa katika maisha yako.
Kushindwa kusiwe mwisho wa kujaribu. Kwa sababu maisha ya ndoa si mazuri, haina maana kuwa ni hali ya kuendelea kushindwa. Ina maana kuwa unatakiwa kujaribu tena kuimarisha ndoa yako bila kukata tamaa. Itafikia mahali itakubidi ukabiliane na hali hiyo, ili wewe na mwenzako muweze kuwasiliana, kuelewana na kujenga upya ndoa yenu. Itakuwa siku mpya kwenu kwa kuwa hali ya kushindwa katika ndoa yenu kwa siku iliyopita haina maana kuwa ndoa yenu haiwezi kuwa mpya tena.
Kwa sababu umepoteza kazi yako jana, haina maana hautafanikiwa kupata kazi nyingine siku ya leo. Kwa sababu umeshindwa kwenye biashara zako katika siku zilizopita, haina maana kuwa hautafanikiwa sasa, kwa sababu umefeli majaribio ya udereva haina maana kuwa hautafanikiwa kabisa kuendesha gari itabidi ufanye jitihada zaidi na zaidi.
Kamwe usiruhusu kushindwa kwako kwa siku ya jana kuondoa uwezekano wako wa kuwa na mafanikio katika siku ya leo au kesho.
Ondoa hofu ya kushindwa ndani ya moyo wako. Ondoa hofu yako kabla ya hofu hiyo kukumaliza. Hakuna hisia kali kama hisia za kuwa na hofu. Inaweza kummaliza mfanyabiashara ambaye anatarajia kupata mafanikio katika biashara zake. Hofu inamfanya mwenye uhitaji wa kupata kazi kuacha kutafuta. Hali hiyo inaleta ulemavu kiutendaji, katika kukabiliana na maamuzi mbalimbali, pia kukusababishia kupata maumivu ya tumbo. Hofu ya kushindwa inawaathiri watu wengi kabla hawajaanza chochote.
Mara zote unatakiwa kuikumbusha nafsi yako kuwa huwezi kupata mafanikio bila kuthubutu. Huwezi mpaka umepata uzoefu ambao utakufanya uwe na malengo makubwa ya kufanikiwa. Mtu mwenye mambo mengi hufanya makosa mengi pia, lakini si kwamba anafanya makosa makubwa zaidi ya wote - si kitu.
Japo umeshindwa katika mambo fulani, haina maana kuwa utaendelea kushindwa tena. Ukweli ni kwamba, nafasi yako ya kushinda ni sasa. Sasa waweza kujua mapema adui ambaye anakusababisha ushindwe na kumkwepa.
Faidi kutokana na makosa yako na songa mbele kwa kujiamini. Tuangalie mfano ufuatao.
Kijana mmoja alikwenda ofisini kwa rafiki yake, na kumwambia amefeli. Kwa mara ya kwanza amekosa matumaini na malengo ya maisha yake. Kila anachokigusa kinakwenda mrama. “Ninailaumu nafsi yangu kwa ujinga wangu. Hakuna mtu atakayeweza kuniamini tena.”
Katika umri wake wa miaka 27, alifukuzwa katika kazi aliyokuwa akiifanya kutokana na makosa aliyoyafanya.
“Nitafanyaje?” alilia kwa sauti ya huzuni. “Nitamweleza nini mke wangu? Nilikuwa na nafasi katika kazi yangu. Nimepoteza bahati yangu katika kampuni hii. Kwa nini nimeufanya uzembe huu? Sitapata kazi nyingine nzuri kama hii,” alisema kijana huyo.
Baada ya kijana huyo kumweleza rafiki yake mambo yaliyomkuta, rafiki huyo alimwambia kuwa haina haja ya kulia wala kuhuzunika tena kwa kuwa kosa ameshalifanya na kazi ameshafukuzwa. “Jambo la msingi ninaloliona ni kuangalia kwa umakini kosa ulilolitenda na kwa nini umelitenda. Wote tutajifunza kutokana na makosa hayo,” alisema rafiki huyo na kuongeza: “Hivyo yaweke pembeni, sahau yote na songa mbele kufanya mambo yenye mafanikio maishani mwako.”
Ni kweli kila mmoja anafanya makosa. Watu wawili niliowachunguza kwa umakini, wote wamejifunza kutokana na makosa waliyoyafanya. Kuwa mwanafunzi maana yake ni kujifunza. Hivyo kushindwa ni nafasi ya kujifunza jinsi ya kufanya mambo mazuri kwa wakati mwingine, kujifunza ilipo mitego katika maisha na jinsi ya kuepuka. Wengi tunajifunza kupitia kushindwa kwetu zaidi ya mafanikio tunayoyapata.
Kubali makosa yako mwenyewe. Ni jinsi gani mtoto anaanza kujifunza kutembea, anajaribu na kushindwa? Wote tunajifunza, vikwazo vingi vinatokea na kusababisha kushindwa. Tutasema ni hali ya kushindwa? Hapana! Tunatambua ili tufanikiwe yatupasa kusonga mbele.
Fikiria kwamba umepata kazi mpya, na kuna vitu vingi vya kujifunza katika kazi hiyo mpya. Katika siku za mwanzoni, bosi yeyote mwenye akili timamu hawezi kukuachia kazi ile uifanye mwenyewe. Itachukua muda kuweza kuifanya kazi hiyo vizuri. Kila sehemu ya maisha yetu iko namna hii, inachukua muda kujifunza jinsi ya kufanya.
Wakati wapendanao wanapooana, inachukua muda kuwiana tabia na kujifunza jinsi ya kuishi pamoja. Kitu kikubwa ni kukubali kujifunza. Hakuna aliye mkamilifu.
Samehe makosa yako na sahau. Ni muhimu kujifunza kujisamehe. Hakuna njia ya mkato ya kupata furaha endapo utakuwa na kinyongo katika nafsi yako. Chua maumivu yanayokupata kwa mafuta ya ukarimu, paka kwa utaratibu kwenye maeneo yote yenye maumivu. Chochote ukifanyacho, acha kujiumiza mwenyewe kwa kujilaumu.
Jifunze kusamehe wengine. Watu ni watu, si miungu. Ni kama wanadamu wengine kama wewe na mimi.
Usiruhusu kutawaliwa na kilichotokea kwako, bali utawaliwe na hatua utakazozichukua kuanzia hapo ulipo. Usiruhusu mamivu yako yaliyopita, kushindwa kwako kwani kutakurudisha nyuma.
Baadhi ya watu walioathirika na maumivu ndani ya mioyo yao wanasema kuwa hawatakaa wamwamini yeyote maishani mwao, hawatafanya biashara tena au hawataoa au kuolewa tena. Unaporuhusu hali hiyo ya kushindwa unaifanya iingie ndani yako na kukutawala. Usiruhusu yaliyopita yatawale maisha yako sasa. Kilichotokea kimetokea.
Piga hatua kwa kujiamini. Ona yaliyotokea kwako kama vile maji yapitayo darajani.
No comments:
Post a Comment